2018-01-09 07:08:00

Dhamana ya wanadiplomasia ni kukoleza majadiliano, haki na amani!


Balozi Armindo Fernandes do Espìrito Santo Vieira, kutoka Angola, Dekano wa Mabalozi na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican, katika hotuba yake  aliyoitoa mbele ya Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 8 Januari 2018 amemtakia afya njema na mafanikio katika utume wake kwa ajili ya uinjilishaji na kwamba, huduma ya kidiplomasia kwa namna ya pekee ni chombo cha majadiliano ili kukabiliana na changamoto zinazotishia amani duniani! Amempongeza Papa Francisko kwa jitihada zake za kufariji, kutia moyo na kuwapatia watu matumaini ya Kikristo kama njia ya ujenzi wa leo na kesho iliyo bora zaidi.

Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana inayoongozwa na kauli mbiu “Vijana, imani na mang’amuzi ya miito” itakayoadhimishwa mwezi Oktoba, 2018, Maadhimisho ya Siku ya 32 Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 huko Panama kwa kuongozwa na kauli mbiu “Tazama mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema” pamoja na Siku ya Familia Duniani kwa Mwaka 2018 pamoja na Sinodi ya Maaskofu wa Amazzonia ni kati ya matukio makuu yanayofumbatwa katika maisha na utume wa Kanisa sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kama ulivyofafanuliwa na kuchambuliwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako, juu ya utunzaji wa nyumba ya wote.

Balozi Armindo Fernandes do Espìrito Santo Vieira anafafanua kwamba, matukio yote haya yanapania kwa namna ya pekee kabisa kujenga na kudumisha mafungamano ya kijamii, utunzaji bora wa mazingira na utekelezaji wa Mkataba wa Paris wa Mwaka 2015 kuhusu mazingira kama unavyoendelea kufuatiliwa na Jumuiya ya Kimataifa katika mikutano yake mbali mbali. Amempongeza Baba Mtakatifu kwa hija zake za kitume huko Fatima kama hujaji wa imani; Colombia kama hujaji wa upatanisho, haki na amani; Myanmar na Bangaladesh kwa kukazia haki msingi, utu na heshima ya binadamu; kwa kuendelea kuwa mashuhuda na vyombo vya haki, amani na upatanisho kati ya watu wa Mataifa.

Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu kumalizika kwa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia na changamoto ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia ni mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika mchakato wa amani kama chanzo kikuu cha kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa, ili kukuza na kudumisha haki msingi za binadamu, huduma makini kwa wakimbizi na wahamiaji duniani. Jumuiya ya Kimataifa inakabiliwa kwa kiasi kikubwa na changamoto ya amani pamoja na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji. Mwaka 2017 umekuwa ni mwaka ambao uligubikwa na vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, inayoitaka Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika mchakato wa majadiliano yanayosimikwa katika ukweli, uwazi, ustawi na maendeleo ya wengi.

Mabalozi na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa wanasikitika kusema kwamba, bado kuna vita na kinzani sehemu mbali mbali za dunia, lakini wana matumaini makubwa kwamba yote haya yanaweza kupatiwa ufumbuzi wa kudumu. Furaha ya kweli inaweza kububujika kutoka nyoyoni pale tu, watu wanapojifunza kuwa wema zaidi, dhamana na utume unaopaswa kutekelezwa na wanadiplomasia hasa pale wanapokumbana na matatizo na changamoto katika maisha. Kuna matumaini ya kuwa na dunia bora zaidi. Wamemtakia heri na baraka katika hija yake ya kitume huko Chile na Perù; afya njema na mafanikio katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.