Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa \ Kanisa Ulimwenguni

Jifunzeni unyenyekevu wa watoto ili kudumisha haki, amani na upendo!

Patriaki Tawadros II: Jifunzeni unyenyekevu wa watoto wadogo, toba, wongofu wa ndani, ukweli na uwazi; hekima na busara ili kudumisha haki, amani na maridhiano kati ya watu duniani. - AP

08/01/2018 07:32

Sherehe ya Noeli, yaani kuzaliwa kwa Kristo Yesu, Mwana wa Mungu ni mwanzo wa mwaka mpya, Kanisa linapokumbuka kazi kubwa ya uumbaji iliyotekelezwa na Mwenyezi Mungu katika huruma na upendo wake mkuu na utimilifu wa kazi ya uumbaji ni pale Mungu alipomuumba mwanadamu. Huu ukawa ni mwanzo wa mema yote na uhusiano wa karibu sana na Mwenyezi Mungu, Muumba wa vyote. Pale Adamu na Hawa walipotenda dhambi ya asili, Mwenyezi Mungu akawafukuza kutoka mbele ya uso na uwepo wake. Hawa akawa ni mama wa mataifa na watu wakaenea sehemu mbali mbali za dunia. Hali hii ilipelekea dhambi kuenea kwa haraka duniani. Tangu wakati huo, vita, kinzani, uhalifu na uvunjaji wa haki msingi za binadamu ukaenea kama moto wa mabua! Litania ya vita na majanga yanayomwandama mwanadamu haina ukomo hadi wakati huu.

Hii ni sehemu ya ujumbe wa Noeli kwa Mwaka 2018 kutoka kwa Patriaki Tawadros II wa Kanisa la Kikoptic la Kiorthodox, nchini Misri, iliyoadhimishwa katika mkesha wa tarehe 6 Januari 2018. Anasema, kuzaliwa kwa Mwana wa Mungu, Kristo Yesu, Masiha na Mkombozi wa ulimwengu huko Bethlehemu ni mwaliko wa kusherehea zawadi ya ari, moyo na unyenyekevu unaoshuhudiwa na watoto wadogo katika maisha yao. Ni wakati wa kumshukuru Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa, aliyekingiwa dhambi ya asili, ili aweze kuwa ni Tabernakulo ya kwanza ya Neno aliyefanyika mwili na kukaa kati ya watu wake. Fumbo la Umwilisho linapata ukamilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Kristo kwa wakati wake, atayamimina maisha yake kwa ajili ya ukombozi wa binadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Patriaki Tawadros II anakaza kusema, Noeli ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani unaofumbatwa katika hali ya unyenyekevu kama ilivyo kwa watoto wadogo. Au kama ilivyokuwa kwa wachungaji kondeni, watu ambao hawakuthaminiwa kutokana na hali na mazingira ya kazi zao, lakini wao, wakawa wa kwanza kupewa Habari Njema ya Wokovu, kwa vile tu, walikuwa wanakesha, wanyenyekevu na wasikivu. Kipindi cha Noeli, kiwawezeshe waamini kurejea katika uhalisia wa maisha pasi na makuu wala majivuno! Huu ni muda wa kudumisha imani, matumaini, mapendo na uhakika wa maisha, unaobubujika kutoka kwenye kisima cha huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu, kama ilivyokuwa kwa Mzee Zakaria na mke wake Elizabeth waliopewa zawadi ya Mtoto Yohane Mbatizaji katika uzee wao, kiasi hata cha kumwondolea aibu Elizabeth aliyeitwa tasa, lakini, alikuwa ni mwanamke mchamungu, mwenye imani na matumaini katika maisha yake.

Patriaki Tawadros II anaendelea kufafanua kwamba, Noeli ni muda wa kukuza na kudumisha ukweli na uwazi kama yalivyo maisha ya mtoto mdogo yanayoweza kulinganishwa kama karatasi nyeupe pe! Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa ni mfano bora wa ubikira na utakatifu wa maisha, kiasi hata cha kuwa tayari kutekeleza mpango wa Mungu katika maisha katika hali ya unyenyekevu mkuu. Hata leo hii, walimwengu wanawahitaji mashuhuda wa unyenyekevu, ukweli na moyo mkuu kama alivyokuwa Bikira Maria. Watoto ni chemchemi ya furaha, amani na utulivu wa ndani. Noeli ni wakati wa kuendelea kujikita katika mchakato wa utakatifu wa maisha, kwa kuondokana na dhambi pamoja na vishawishi vyake vyote, ili kudumisha amani, furaha na utulivu kati ya watu wa Mataifa, ili hatimaye, kuondokana na vita, kinzani na migogoro inayopelekea majanga makubwa miongoni mwa familia ya binadamu.

Patriaki Tawadros II anaendelea kufafanua kwamba, waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanahitaji kuambata hekima na busara kama walivyoshuhudia Mamajusi kutoka Mashariki ya mbali, waliongozwa na nyota hadi mjini Bethelehemu, walipomwona Mtoto Yesu wakamfungulia hazina ya: dhahabu, uvumba na manemane, zawadi zenye maana kubwa katika maisha na utume wa Kristo kama: Mfalme, Masiha na Mkombozi wa Ulimwengu. Waamini wakijitahidi kuishi karama hizi zinazofumbatwa na wahusika wakuu katika kipindi cha Noeli, wataweza kushinda kishawishi cha vita, kinzani na migogoro inayosababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao!

Patriaki Tawadros II anasema, katika maadhimisho ya Noeli ya Mwaka 2018, Kanisa la Kiorthodox la Kikoptik nchini Misri linazindua Kanisa kuu katika mji mkuu mpya wa Misri linaloitwa “Kanisa kuu la Kuzaliwa kwa Kristo”. Huu ni mradi mkubwa ambao umetekelezwa na wadau mbali mbali nchini Misri, kwa ajili ya ustawi na maendeleo endelevu ya familia ya Mungu nchini humo. Mwishoni, Patriaki Tawadros II anawaalika waamini kuendelea kusali kwa ajili ya kuombea amani, usalama na utulivu duniani, daima Mwenyezi Mungu akipewa sifa, utukufu na heshima!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

08/01/2018 07:32