Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Hotuba

Hotuba ya Papa Francisko kwa Mabalozi mjini Vatican kwa Mwaka 2018

Papa Francisko katika hotuba yake kwa mabalozi na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa amezungumzia kuhusu changamoto zinazopaswa kufanyiwa kazi na Jumuiya ya Kimataifa kwa ushirika. - AFP

08/01/2018 11:40

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwa wanadiplomasia wanaoziwakilisha nchi zao kama mabalozi pamoja na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa, kama sehemu ya mapokeo ya kutakiana heri na baraka kwa Mwaka Mpya 2018, Jumatatu, tarehe 8 Januari 2018 amekazia umuhimu wa mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa katika kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazoendelea kuibuka kila kukicha! Vatican kwa upande wake inapania kukuza na kudumisha: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi: kiroho na kimwili. Jumuiya ya Kimataifa kwa mwaka 2018 inaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 100 tangu kusitishwa kwa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia iliyosababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao na kwamba, kuna haja ya kujenga na kudumisha amani duniani inayofumbatwa katika ukweli, haki, mshikamano tendaji na uhuru mambo msingi yanayobainishwa kwenye Tamko la Haki Msingi za Binadamu, ambalo, kwa Mwaka huu, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 70 tangu kuchapishwa kwake!

Baba Mtakatifu amekazaia umuhimu wa mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu kama msingi wa kukuza na kudumisha amani duniani. Dhamana hii inaweza kutekelezwa kwa njia ya majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kuheshimiana na kuthaminiana. Amegusia changamoto ya amani huko Mashariki ya Kati na katika baadhi ya nchi za Kiafrika. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu amefafanua tunu msingi za maisha ya kifamilia, changamoto zinazozikabili familia, yaani umaskini, vita na wimbi kubwa la wahamiaji pamoja na kazi za suluba wanazofanyishwa watoto wadogo. Baba Mtakatifu anabainisha mambo msingi yanayoweza kutumiwa na Jumuiya ya Kimataifa katika kupambana na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani yaani kwa: kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha. Amezishukuru nchi mbali mbali zinazojitahidi kutoa hifadhi na huduma endelevu kwa wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia na kwamba, kuna haja ya kulinda na kudumisha haki msingi za binadamu na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Baba Mtakatifu Francisko ameanza hotuba yake kwa kuwashukuru na kuwapongeza mabalozi na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican. Amesikitishwa na kifo cha Balozi Guillermo Leòn Escobar Herràn, kutoka Colombia, kilichotokea siku chache kabla ya kuadhimisha Siku kuu ya Noeli kwa Mwaka 2017. Huu ni ushuhuda wa mshikamano wa dhati kati ya Vatican, Kanisa na Jumuiya ya Kimataifa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Amepongeza itifaki iliyotiwa sahihi kati ya Vatican na Jamhuri ya Watu wa Congo pamoja na Russia kuhusu kufutwa kwa hati za kusafiria za wanadiplomasia.

Vatican inapenda kuendeleza ushirikiano na serikali mbali mbali kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, ushuhuda ambao umeoneshwa na Baba Mtakatifu mwenyewe katika hija zake za kitume huko Misri, Ureno, Colombia, Myanmar, Bangaladesh na Ureno ambako ameshiriki Jubilei ya Miaka 100 tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Fatima yaani: Francis, Yacinta na Lucia, ambao kati yao, wawili tayari wametangazwa kuwa ni watakatifu na mchakato wa kumtangaza Lucia kuwa Mwenyeheri tayari umeanza. Huu ni ushuhuda kwamba, majadiliano katika ukweli na uwazi yanawezekana ili kujenga na  kudumisha ukweli na haki.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 100 tangu kusitishwa kwa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, iliyopelekea pia kuzuka kwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia, changamoto ni kukuza na kudumisha majadiliano katika ukweli na uwazi ili kuganga na kuponya madonda ya vita, kinzani na mipasuko mbali mbali ya kijamii, huu ukawa ni mwanzo wa kuundwa kwa Umoja wa Mataifa. Mahusiano na mafungamano ya kijamii hayana budi kufumbatwa na kuratibiwa katika: ukweli, haki na mshikamano tendaji; kwa kutambua na kuheshimu haki asili, haki msingi, utu na heshima ya binadamu pamoja na haki sawa mambo msingi katika uhuru, haki na amani, kama yanavyobainishwa na Tamko la Haki Msingi za Binadamu, lililotiwa mkwaju na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 10 Desemba 1948, miaka sabini iliyopita! Kipaumbele cha kwanza ni utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; uhai unaopaswa kulindwa na kuendelezwa, sanjari na kujikita katika mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu: kiroho na kimwili.

Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuheshimu haki msingi za binadamu dhidi ya kile kinachodaiwa kuwa ni “Haki Mpya” ambazo kimsingi zinasigana na tamaduni, mila na desturi za mataifa mengi. Uhuru wa kweli hauna budi kudumishwa dhidi ya utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za utoaji mimba na kifo laini; biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo; mambo yanayokwenda kinyume cha Injili ya uhai. Kumbe, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuhakikisha kwamba, watu wengi zaidi wanapata huduma ya afya na dawa muhimu katika mapambano dhidi ya magonjwa duniani.

Ili kudumisha uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, kuna haja pia ya kujikita katika ujenzi wa amani kama chachu ya maendeleo endelevu ya binadamu. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kutekeleza Itifaki ya Udhibiti wa Ulimbikizaji na Matumizi ya Silaha ya Kinyuklia kwa ajili ya usalama wa familia ya binadamu! Vatican itaendelea kujikita katika mchakato wa kusimamia: ukweli, haki, upendo na uhuru mambo yanayobainishwa kwenye Waraka wa Kichungaji, “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani” uliochapishwa kunako mwaka 1964. Vatican ina laani utengenezaji na matumizi ya silaha kali zaidi duniani zinazoendeleza Vita Kuu ya Tatu ya Dunia, inayopiganwa sehemu mbali mbali za dunia.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Korea itajikita katika suluhu ya amani, ili kudumisha amani nchini Korea na ulimwengu katika ujumla wake. Baada ya vita ya muda mrefu, walau sasa amani na utulivu vimeanza kurejea tena nchini Siria, changamoto ya kwanza kabisa ni kujenga nyoyo za watu, ili kuaminiana na kuthaminiana hata kabla ya kuanza ujenzi wa majumba. Kuna umuhimu wa kujikita katika ujenzi wa miundo mbinu itakayodumisha utawala wa sheria, siasa na amani, kila raia akijitahidi kutekeleza dhamana na wajibu wake. Wakimbizi na wahamiaji waliopatiwa hifadhi huko Yordan, Lebanon na Uturuki, wasaidiwe kurejea makwao na kwamba, Lebanon itabaki kuwa ni mfano bora wa kuigwa katika mchakato wa kuheshimiana na kuishi kwa amani na utulivu.

Majadiliano katika ukweli na uwazi ni muhimu sana kwa Iraq, ili kuanza kutembea katika njia ya upatanisho, haki, amani na ushirikiano kama ilivyo hata kwa Yemen na Afghanistan. Israel na Palestina, wanapaswa kuheshimiana mintarafu Itifaki ya Umoja wa Mataifa kwa kutambua kwamba, Yerusalemu ni Mji Mtakatifu kwa dini ya Kiyahudi, Kikristo na Kiislam. Majadiliano ni njia pekee itakayoziwezesha nchi hizi mbili kuishi kwa amani! Majadiliano yanapaswa kuendelezwa pia huko Venezuela, Sudan ya Kusini, DRC, Somalia, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, nchi ambazo haki ya maisha iko hatarini kutokana na uporaji wa rasilimali, vitendo vya kigaidi na uporaji; mambo ambayo yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na umaskini wa hali na mali na badala yake, watu wajenge madaraja ya udugu kwa kujikita katika maendeleo endelevu ya binadamu!

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake, anakazia umuhimu wa familia kama kitovu na msingi wa jamii, inayopaswa kulindwa na kudumishwa na serikali husika. Familia inajengwa kwa njia ya mahusiano thabiti kati ya mwanamke na mwanaume yanayofumbatwa katika uaminifu na udumifu! Lakini, leo hii kuna sera na siasa zinazotaka kupindisha ukweli huu, kiasi hata cha kushabikiwa ndoa za watu wa jinsia moja. Umaskini, wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi ni kati ya changamoto zinazoendelea kuzikumba familia mbalimbali duniani.

Baba Mtakatifu katika ujumbe wake wa kuombea amani duniani kwa mwaka 2018 anakaza kusema wakimbizi na wahamiaji ni watu wanaotafuta amani. Ni watu wanaolazimika kuzikimbia nchi zao kutokana na sababu mbali mbali, kumbe wanapaswa kupewa hifadhi. Anazishukuru nchi ambazo zimekuwa mstari wa mbele katika kuwahifadhi wakimbizi na wahamiaji duniani huko Asia, Afrika na Amerika. Kwa namna ya pekee, anaipongeza Italia, Ugiriki na Ujerumani kwa kujitosa kimasomaso kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji.  Jumuiya ya Kimataifa inaendelea kujizatiti ili kupitisha mikataba inayolenga kuokoa maisha ya wakimbizi kwa kuwapatia njia halali na zinazo ratibiwa vyema. Baba Mtakatifu anapenda kukazia kwa namna ya pekee kabisa umuhimu wa kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji katika uhalisia wa maisha ya jamii inayowapokea!

Kuhusu Haki Msingi za Binadamu, Baba Mtakatifu amekazia uhuru wa mawazo, haki ya kupata fursa za kazi ili kumwezesha mtu kutekeleza dhamana na wajibu wake katika jamii pamoja na kupata muda wa mapumziko ili kuitakatifuza Siku ya Bwana. Amesikitishwa na uvunjwaji wa haki msingi za watoto kwa kufanyishwa kazi za suluba zinazo sababisha athari kubwa kwa ukuaji wa watoto kisaikolojia. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kusimama kidete kupambana na hatimaye kufutilia mbali kazi za suluba. Anakazia haki msingi za binadamu kama sehemu ya dhamana ya kiutu na kimaadili, kwa ajili ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Mwishoni, Baba Mtakatifu amezungumzia kuhusu umuhimu wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote  kwani majanga asilia yamekuwa ni sababu ya maafa makubwa ka watu na mali zao sehemu mbali mbali za dunia. Lakini, ikumbukwe kwamba, athari za mabadiliko ya tabianchi ni matokeo ya kazi za binadamu, kumbe, kuna haja ya watu kuwajibika pamoja na kutekeleza kwa vitendo Mkataba wa Paris wa Mwaka 2015 juu ya udhibiti wa mabadiliko ya tabianchi unaopania pamoja na mambo mengine kupunguza hewa ya ukaa inayosababisha madhara makubwa katika afya. Baba Mtakatifu anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa ulimwengu ulio bora zaidi kwa njia ya huduma na  mshikamano shirikishi kama alama ya matumaini katika ulimwengu mamboleo. Anawatakia mabalozi wote furaha, matumaini na amani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 

08/01/2018 11:40