2018-01-06 14:39:00

Siku kuu ya Ubatizo wa Bwana: Mshikamano na binadamu mdhambi!


Tunasherehekea leo ubatizo wa Bwana ambapo kadiri ya mwinjili Yohani ni mwanzo wa utume wa kimasiya wa Yesu Kristo. Mwanzo wa utume huu wa kimasiya, utakamilika katika kifo na ufufuko, ondoleo kamili la dhambi - Yoh 1:29. Somo la kwanza laeleza utume wa Yesu kama Masiya anayetoa neema. Huyu ni mtumishi wangu ninayependezwa naye nimeweka roho yangu juu yake, ataleta amani kwa mataifa. Somo la pili - Mt. Petro amwonesha Yesu katika ubatizo wake kama mpakwa mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu,  hivyo, yuko tayari kufanya kazi na kuponya wote waliotingwa na dhambi.   Katika Injili Yesu anapokea ubatizo ili kutimiza sheria kadiri ya taratibu za Kiyahudi. Katika tendo hili linatoka tamko - huyu ni mwanangu mpendwa wangu, msikilizeni yeye. Kwa sababu ya dhambi ya asili kila azaliwaye huwa na dhambi ambayo hufanya maisha ya neema kukosekana.  Katika Uyahudi, ibada mbalimbali za utakaso zilifanyika na Yesu alijifananisha na baadhi ya hizi ibada kama;

  1. Kutahiriwa – Lk. 2:21
  2. Kutolewa hekaluni – Lk. 2:22-23
  3. Ubatizo - Mt. 3:13-17

Aidha ubatizo wakati huo ulikuwa na maana tofauti.

  1. kutakaswa
  2. Kujiweka sawa na Mungu
  3. Kuonesha imani kwa Mungu
  4. Kama alama ya toba
  5. Kupata uanachama katika jamii ya kiyahudi. Yesu anaingia hapa. Yesu alipata ubatizo ili ajifananishe na Uyahudi, ili akubalike pindi akianza utume wake kati yao kama mmoja anayeamini katika dini yao. Yohana alitoa ubatizo wa toba – Mt. 3:13-17. Yesu alikuwa kama sisi isipokuwa dhambi – Fil. 2,7; Ebr. 4:15, Rom. 8:3. Yesu alipokea ubatizo ili kujiweka sawa na Mungu, kuzaliwa katika familia ya Mungu – Mt. 3:14 – leo hii ili kuingia katika familia hiyo ya Mungu, twahitaji ubatizo.

Je,  Yesu alihiaji kubatizwa? Siyo. Ila kwa tendo hili alionesha ushirika nasi. Pia aliweka mwisho wa ubatizo wa maji na kuanza ule wa Roho. Hakuja tu kufunua umungu wake kwetu, amekuja pia kujifunua kwetu kama mwanadamu. Ni Mungu kweli na mtu kweli. Ubatizo wake ni wokovu wetu. Anafanana nasi ila bila dhambi. Anageuza hali yetu toka ubinadamu tu na kuupa hadhi ya kimungu. Hivyo nasi kwa ubatizo tunakuwa wapendwa wake Mungu. Na kama alivyofanya Yesu baada ya ubatizo wake, nasi tunaitwa kutangaza kwa maisha yetu yote ufalme wa Mungu.

Ubatizo wa Kristo waonesha ni zaidi ya kuoshwa kwa maji au kusafishwa. Mbatizwa huzaliwa upya kwa njia ya Roho Mtakatifu. Kwa tendo la ubatizo wa Yesu utukufu wa Mungu ulifunuliwa kwa Roho Mtakatifu kushuka juu yake - huyu ndiye mwanangu mpendwa  msikilizeni yeye. Inakamilisha fundisho la Yohani Mbatizaji - yeye ajaye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na moto, Mt 3:11. Tujikumbushe pia mwaliko wa Yesu kwa Nikodemo - mtu asipozaliwa upya katika maji na Roho Mtakatifu hataingia ufalme wa mbinguni Yoh 3:3-5. Yesu hakubatiza ye yote – Yoh. 4:2 - ila ubatizo aliopokea ni tofauti na ule aliowafundisha wafuasi wake kufanya. Aliwaalika wabatize kwa Roho - Mt. 28:19 na hapa kuna tofauti na aina ya ubatizo uliofanyika wakati wake. Kwa njia hii wafuasi walitoa sakramenti ya ubatizo kwa waongofu wote kabla ya kujiunga na imani na kuabudu pamoja nao - Mdo. 2:37-39 - wito wa uongofu - waliposikia hayo walichomwa moyo na wakamwuliza Petro na mitume wengine tufanye nini enyi ndugu? Petro akawajibu, tubuni na kila mmoja wenu abatizwe kwa jina lake Yesu Kristo mpate kuondolewa dhambi zenu; nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu. Kwa maana ahadi hii imefanywa kwa ajili yenu na watoto wetu na wale wote wa mbali atakaowaita kwake Bwana Mungu wetu. Kwa ubatizo wake Kristo, umewekwa msingi wa namna mpya ya kupata neema. Mbatizwa huanzisha uhusiano mpya na UTATU MTAKATIFU.

KKK 1213 – tunaona kuwa - Ubatizo mtakatifu ni msingi wa maisha yote ya Kikristo, lango la kuingilia uzima katika roho (vitae spiritualis ianua) na mlango unaowezesha kuzipata sakramenti nyingine. Kwa njia ya utabizo tunafanywa huru toka dhambi na tunazaliwa upya kama watoto wa Mungu, tunakuwa viungo vya Kristo na tunaingizwa katika Kanisa na tunafanywa washiriki katika utume wake: ubatizo ni sakramenti ya kuzaliwa upya kwa maji katika neno. Katika Mdo. 10:37-38 tunasoma kuwa - mmejua yaliyotokea katika uyahudi wote kuanzia Galilaya baada ya ubatizo aliouhubiri Yohani jinsi Mungu  alivyompaka mafuta Yesu wa Nazareti kwa roho mtakatifu na nguvu. Na jinsi alivyozunguka katika nchi yote akitenda mema na kuwaponya wote walioonewa na shetani kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye.

Mwinjili Yohane anashuhudia kwa neno hili – Yoh. 5:3-9 - humo walilala wagonjwa wengi, vipofu, viwete na wenye kupooza. Pale palikuwa na mtu mmoja aliyekuwa mgonjwa tangu miaka thelathini na minane. Yesu alipomwona amelala huko, akajua ya kuwa amekuwa na hali hiyo muda mrefu, akamuuliza je wataka kuwa mzima? Mgonjwa akamjibu, Bwana sina mtu wa kunishusha bwawani yanapovurugika maji. Kila ninapojaribu kushuka mwingine anakuwa amekwisha shuka kabla yangu. Yesu akamwambia; simama jitwike godoro lako, mara yule akawa mzima akajitwika godoro lake akaenda. Hivyo, ubatizo unatuunganisha na Kristo na katika muungano huu tunapata nguvu ya kuendelea mbele na kutenda mema katika Kristo Bwana na mwokozi wetu. Tunapata neema ya kuishi kama watoto wa Mungu katika imani - Gal 2:20-  si mimi tena ninayeishi bali ni Kristo anayeishi ndani yangu. Muda ninaoishi bado mwilini ninaishi katika imani inayomtegemea Mwana wa Mungu ambaye amenipenda na kujitoa kwa ajili yangu.

Wabatizwa hawana budi sasa kuishi neema hii kila siku ya maisha yao  huku wakiepuka dhambi - Yoh 8:34-36. KKK 1227; kadiri ya Mtakatifu Paulo mtume, kwa ubatizo, mwamini hushiriki mauti ya Kristo, huzikwa pamoja naye na kufufuka pamoja naye. Tulipobatizwa katika Kristo Yesu, tulibatizwa katika mauti yake basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima- Rom. 6:3-4, Kol 2:12. Wabatizwa wamemvaa Kristo – Gal. 3:27. Kwa njia ya Roho Mtakatifu Ubatizo ni kuoshwa kunakotakasa kunakotakatifuza na kuhesabia haki - 1 Kor. 6: 11-12:13.

Ndugu zangu, Siku kuu hii hutupa nafasi ya kutakafari ubatizo wetu. Ubatizo ni zawadi iliyotolewa kwetu kwa mapenzi ya Kristo. Katika Mk. 16:16 – tunasoma - aaminiye na kubatizwa ataokoka. Yesu aliweka sakramengi kama njia ya wokovu. Mungu anapenda watu wote waokoke na watambue yaliyo kweli -  Tim. 2:4.

Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S








All the contents on this site are copyrighted ©.