Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Tafakari \ Tafakari ya Neno la Mungu

Siku kuu ya Ubatizo wa Bwana: Kuzaliwa upya kwa maji na Roho Mtakatifu

Siku kuu ya Ubatizo wa Bwana inafunga rasmi kipindi cha Noeli na kufungua kipindi cha mwaka wa Kanisa. - AFP

06/01/2018 15:14

Dominika ya Ubatizo wa Bwana ni siku ya kiliturujia yenye tabia ya kipekee. Hii ni siku ambayo katika kalenda ya kiliturujia inaunganisha vipindi viwili kwa pamoja. Kwa upande mmoja inahitimisha kipindi cha Noeli na kwa upande wa pili kinaanzisha kipindi cha kawaida cha mwaka wa kiliturujia. Kwa maneno mengine leo ni Dominika ya kwanza ya Mwaka B wa Kanisa. Hivyo siku hii inakuwa na sifa ya bawaba ambayo huunganisha mlango pamoja na mhimo wake na kuufanya kuwa imara. Kristo aliye mhimo wa safari nzima ya mwaka wa kiliturujia anakuwa pia ni mlango wa kutuingiza katika ufalme wa Mungu na anaunganishwa katika maisha ya kawaida ya kikristo ambayo huadhimishwa katika Kipindi cha kawaida cha mwaka.

Mara nyingi huwa tunajiuliza kwa nini Kristo anabatizwa? Je, Yeye aliye mtakatifu alihitaji kweli ubatizo wa toba? Injili ya Dominika hii haituambii wazi lakini tujisumbue kidogo na kuzisoma Injili nyingine zinazoelezea mkutano wa kwanza kati ya Yesu na Yohane Mbatizaji na namna alivyomtambulisha. Yesu Kristo alikuwa anaelekea kuanza utume wake wa hadharani. Kulikuwa na umuhimu kwa mtangulizi wake Yohane Mbatizaji kumtambulisha kwa watu hadharani. Yohane Mbatizaji kama katika Injili ya leo alikwishaanza kumwelezea kuwa anayekuja nyuma yake ni mkuu zaidi yake. Kitendo cha Yesu kwenda kubatizwa kilimpatia fursa kuwaambia watu waliokuwa wanamsikiliza kuwa ndiye huyu ambaye nimekuwa nikiwaambia. Lakini pia katika namna ya kujificha tunaona Yohane mbatizaji ambaye alitokea katika kabila la Lawi ambao ni uzao wa Aroni (Rej Lk 5:1) anatimiza wajibu wake wa kikuhani kwa namna ya juu zaidi kwa kuionesha Sadaka Kuu kabisa, yaani Sadaka itakayotolewa na Kristo pale alipomtambulisha akisema: “Tazama, Mwanakondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu” (Yoh 1:29)

Yohane Mbatizaji alionesha wazi kuutambua ukuu wa Kristo na jinsi ambavyo hakustahili kubatizwa katika toba. Yohane alisema “mimi nahitaji kubatizwa na wewe” ila Kristo alimjibu “kubali hivi sasa; kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki” (Mt 13:14 – 15). Fumbo zima la umwilisho linaashiria unyenyekevu wa Kristo anayeamua kujisawazisha nasi katika udhaifu wetu. “Kwa kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi” (Waebr4:15). Yesu alikubali kubatizwa ubatizo wa toba ili kujifungamanisha tangu mwanzo na mwanadamu mdhambi. Aliwaonesha kwa namna nyingine namna wale watakaokuja kwake na kubadilishana naye dhambi zao kwa uadilifu wake Kristo. Ndiyo maana akamwambia Yohane mbatizaji “kubali hivi sasa; kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki”. Ndiyo namna ambayo ninapaswa kupitia ili kwa kujifananisha na huyu mwanadamu katika hali yake ya udhaifu nitapata fursa ya kumtoa katika udhaifu wake. Nitakapotembea naye na kumfanya anione kuwa ni sehemu muhimu ya maisha yake ya kawaida nitaweza kumwongoza vyema kwenda katika njia ya haki.

Kristo alipobatizwa na Yohane hakukupunguza ukuu wake; Yohane mwenyewe alimtambulisha na kujinyenyekesha mbele yake. Yohane Mbatizaji anatuambia katika Injili ya leo akisema: “Yuaja nyuma yangu aliye na nguvu kuliko mimi, ambaye mimi sistahili kuinama na kuilegeza gidamu ya vitatu vyake. Mimi nawabatiza kwa maji; bali yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu”. Yohane anakiri kwamba anakosa hata hadhi ya kulegeza kamba za viatu vyake, anakosa hadhi ya kuwa mtumishi wa Kristo. Kisha anaendelea kuonesha ukuu wake kwa namna ya ubatizo wake, yaani anabatiza kwa Roho Mtakatifu. Tangu mwanzo katika lugha ya Biblia Roho Mtakatifu anaonekana katika kuvipa uhai viumbe vya Mungu. Ubatizo wa Kristo unaonesha kupata uhai mpya wa kimungu ambao huondolewa na dhambi. Si suala la kubaki katika toba tu bali na kupata upya wa maisha au kuzaliwa upya katika Roho Mtakatifu.

Mwanatauhidi maarufu wa nyakati zetu hizi Hans Urs von Balthasar anatupatia maelezo mazuri juu ya muunganiko uliopo katika ya ubatizo wa Yohane Mbatizaji na ubatizo wa Kristo. Von Balthasar anasema: “Injili inayoelezea Ubatizo wa Bwana, inatueleza kufunguka kwa mbingu kutokana na utiifu wake Kristo wa kukubali kushiriki ubatizo wa maji ambao uliashiria mwisho wa Agano la Kale na mwanzo mpya wa Agano lingine kwa kitendo cha Roho Mtakatifu kumshukia Kristo na wakati huo huo Mungu Mwenyezi akimthibitisha kwa maneno kuwa ndiye Mwanae mpendwa: Kristo anakuwa mfano wa wote ambao baada yake watapokea ubatizo wa kikristo: wote watampokea Roho Mtakatifu kutoka mbinguni na watazaliwa upya na kuwa wana wa Mungu. Kwa tukio la ubatizo wa Yesu, maji ya ardhini hayatakuwa tena jambo la hiari, bali yanapokea maana mpya kwani yataunganishwa kwenye fumbo la Utatu Mtakatifu katika Sakramenti ya Ubatizo: kile kilichoonekana ni ishara ya nje tu, sasa kinageuka na kuwa sehemu muhimu ya sakramenti, kimsingi kinakuwa sehemu isiyobadilishika kwa kila mmoja anayepaswa kuzaliwa upya kwa maji na kwa Roho (Yoh 3:5) kwa kupokea maisha ya kimungu”. Hivyo ubatizo wa Yohane unahitimisha Agano la kale na ubatizo wa Kristo unatuingiza katika Agano jipya ambapo tunasafishwa kwa maji na kufanywa upya katika Roho Mtakatifu. Sakramenti ya ubatizo inatupatia neema ya utakazo na kutufanya wana wa Mungu.

 “Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe”. Hadhi hii anayopewa Kristo inapaswa kuonekana kwa wabatizwa wote. Mbingu kufunguka ni ishara ya kuunganika Mungu na wanadamu, kielelezo cha mwanzo mpya wa mwanadamu. Kristo ndiye kielelezo cha upya huo wa maisha. Katika Injili sauti toka mbinguni imesema: “Wewe ndiwe Mwanangu mpendwa wangu; ninyependezwa naye”. Ni maneno ambayo tunayasikia pia katika somo la kwanza na zaidi linatufafanulia namna anavyotenda huyu mwana mpendwa. Nabii Isaya anamwelezea kama Yeye aliyejaa Roho wa Mungu na anatenda kwa unyenyekevu, ukimya, upole, ujasiri wa kupambana na uovu na utii wa kuyatimiza mapenzi ya Mungu, yaani kumkomboa mwanadamu.

Kitabu cha Matendo ya Mitume kinamwelezea Kristo namna alivyotenda baada ya kupakwa mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu. Utume wake ulijikita katika kuitangaza habari njema na kuwaponya walioonewa na ibilisi “kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye”. Hapa ndipo tunapouona muunganiko wa Sikukuu ya leo na kipindi cha kawaida cha liturujia cha mwaka. Baada ya Kristo kuzaliwa ndani mwako katika ubatizo unafanywa kuwa mwana mpendwa wa Mungu na hivyo unatumwa katika maisha ya kawaida ya kila siku ili kuwa mmisionari kwa kuitangaza hari njema na kuwarudishia nguvu na matumaini watu walioingia katika giza. Ubatizo wa Kristo unatukumbusha wajibu wetu wa kikristo na namna ambavyo tunapaswa kuutimiza wajibu huo tumekwisha kuelezewa katika somo la kwanza.

Tuishangilie vema sikukuu ya leo na tujiweke tayari kwa kuingia shambani kutimiza nyajibu zetu. Kila mmoja wetu katika nafasi yake ndani ya familia, katika jumuiya na ndani ya jamii kwa ujumla. Pia mahali pa kazi na katika huduma mbalimbali za kijamii. Twende tukaitangaze Injili na kuwaponya watu wote waliotekwa na ibilisi. Tukumbuke daima kwamba katika Ubatizo Kristo anatufanya kuwa viumbe vipya. Tunafanywa kuwa wana wa Mungu.

Padre Joseph Peter Mosha.

Vatican News!

06/01/2018 15:14