2018-01-06 12:00:00

Papa: Sherehe ya Tokeo la Bwana: Kuona nyota, kutembea na kutoa hazina


Mamajusi kutoka Mashariki ya mbali waliiona nyota mashariki, wakaondoka kwenda Yerusalemu na walipomwona Mtoto Yesu wakamtolea tunu: dhahabu, uvumba na manemane. Huu ndio msingi wa mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Tokeo la Bwana, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, tarehe 6 Januari 2018. Anasema, baada ya kuiona nyota, wakaondoka, bila shaka kuna watu wengi waliiona ile nyota lakini hawakujishughulisha kunyanyua macho yao mbinguni, kwani kawaida ya mwanadamu anapenda kuridhika na mambo ya dunia kama vile afya njema, fedha na starehe.

Baba Mtakatifu anapenda kuchukua nafasi hii kuwauliza waamini ikiwa kama bado wana uwezo wa kuinua macho yao juu angani; kama kweli bado wanaota na kumtamani Mwenyezi Mungu katika maisha yao, tayari kuwakirimia upya wa maisha, au pengine, wanajiachilia kuburuzwa na wimbi la maisha kama “kuti kavu”!. Mamajusi walithubutu, wakaondoka kuifuata ile nyota, changamoto kwa waamini kuwa na ari na moyo mkuu katika maisha! Je, inawezekanaje, umati mkubwa wa watu waliiona ile nyota lakini wakashindwa kuifuata? Mamajusi walipoiona nyota ya Mtoto Yesu mashariki, waliondoka na kuifuata kwani hii ni nyota angavu, inayowaalika watu na wala haipofushi macho wala kumpotosha mtu!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, katika maisha kuna nyota zing’aazo, zinazoleta mvuto, lakini mara nyingi zinampotosha mtu! Nyota kama hizi ni mafanikio ya “chapuchapu”, fedha, ujuzi, sifa na anasa inayotafutwa kwa udi na uvumba! Lakini zote hizi ni nyota zinazodumu kwa kitambo kidogo na hatimaye, kufifia kabisa katika maisha. Lakini, Nyota ya Kristo iko na inadumu daima, inamwongoza na kumsindikiza mwamini katika maisha kwa kumhakikishia amani na furaha kubwa, lakini inayomtaka mwamini kufanya jitihada za kutembea na kusonga mbele.

Baba Mtakatifu anasema, kutembea ni tendo muhimu sana lililowawezesha Mamajusi kumwona Kristo Yesu. Hii ni nyota inayohitaji maamuzi yatakayomfanya mwamini kuanza “kuchapa mwendo” kwa kuondokana na mizigo isiyokuwa na tija wala mashiko katika ramani ya maisha ili kupata utulivu wa ndani. Kristo Yesu anapatikana kwa wale wote wanaojitaabisha kutoka na kutembea, bila kusubiri bali kuthubutu “kuchanja mbuga”. Kwa wale wanaomtafuta Kristo Yesu, hawana budi kuondokana na anasa za dunia hii pamoja na uhakika wa maisha.

Papa Francisko anasema, kumfuasa Kristo Yesu hakuna protokali inayotakiwa kufuatwa, bali ni hija ambayo inapaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu. Mwenyezi Mungu aliwakomboa watu wake kutoka utumwani, akawataka kufuata nyota, inayowapatia uhuru na furaha kuu na hivyo kuondokana na woga usiokuwa na mashiko, uvivu na kudhani kwamba, tayari mtu amefika ukomo wa safari yake. Kuna haja ya kutubutu ili kukutana na Mtoto Yesu, ili kuonja huruma na upendo wake mambo ambayo yanapaswa kushuhudiwa katika maisha ya waamini!

Kutembea ili kuiendea nyota si lelemama yataka moyo kweli kweli! Mfalme Herode alishikwa na wasi wasi juu ya hatima ya ufalme wake, akawakusanya wakuu wa makuhani na waandishi, lakini yeye hakunyanyua mguu wake na matokeo yake ni  kufadhaika na Yerusalemu pamoja naye, kwani waliogopa upya uliokuwa unaletwa na Mungu. Huu ndio mtindo wa makuhani wakuu na waandishi wa watu; wanafahamu, lakini hawatendi, changamoto hata kwa waamini wa nyakati hizi. Wanapenda kuzungumza, lakini wavivu kusali; wanapenda kulalamika, lakini, wanashindwa kutenda mema. Lakini, Mamajusi wanaonesha maneno yao kwa njia ya matendo na wanapomwona Mtoto Yesu wana mwabudu na hatimaye, wakaondoka kwenda zao kwa njia nyingine.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Mamajusi walipomwona Mtoto Yesu wakamtolea tunu: dhahabu, uvumba na manemane. Mamajusi hawa wanatoa zawadi hizi bila kutarajia kurudishiwa chochote kwani wamepewa bure nao wanatoa bure. Hii ni kwa sababu, Kristo amejinyenyekesha na kujifanya kuwa mdogo kwa ajili ya ndugu zake wanaoteseka! Hawa ndio wale wenye njaa, walio uchi, wageni, wafungwa na maskini. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili, ili kuwatofautisha na watoza ushuru na watu wa mataifa wanaopendana wao kwa wao. Baba Mtakatifu anawataka waamini leo kutoa sadaka ambayo kwa hakika itakuwa ni chemchemi ya furaha katika maisha yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.