2018-01-06 10:40:00

Kardinali Monsengwo: Makubaliano yaliyofikiwa hayana budi kutekelezwa


Ubalozi wa Vatican nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo unasema, watu 5 walifariki dunia, Makanisa 134 kuzingirwa na vikosi vya ulinzi na usalama na mapadre 6 walikamatwa wakati wa pilika pilika za maandamano yaliyofanyika tarehe 31 Desemba 2017 ili kumshinikiza Rais Josefu Kabila kung’atuka kutoka madarakani baada ya kushindwa kutekeleza kwa dhati Mkataba wa makubaliano ya amani uliotiwa sahihi kunako mwaka 2016.  Kamati ya Waamini Walei nchini DRC “Comitè Laic de Coordination, CLC, inamtaka Rais Kabila kutangaza hadharani kwamba, hatashiriki tena katika mchakato wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Desemba 2018. Taarifa zaidi zinasema kwamba, kuna baadhi ya Parokia, Ibada ya Misa imezuliwa na kwamba, Makanisa mengi yalifanyiwa kufuru na vikosi vya ulinzi na usalama wakati wa kudhibiti maandamano ya waamini walei, nchini DRC.

Kardinali Laurent Monsengwo Pasinya, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Kinshasa katika mahubiri yake kwenye Kanisa kuu la “Notre Dame du Congo”, tarehe 4 Januari, Kumbu kumbu ya mashujaa wa uhuru wa DRC, amesikika akisema, wananchi waliofariki dunia tarehe 31 Desemba 2017 ni changamoto kwamba, “Pacta sunt servanda” yaani “Makubaliano yaliyofikiwa hayana budi kutekelezwa”. Makubaliano hayakuheshimiwa, wafungwa wa kisiasa bado hawajaachiliwa na kwamba, hata uchaguzi uliopaswa kufanyika mwaka 2017 hakufanyika. Ibada hii ya Misa Takatifu ilihudhuriwa na umati mkubwa wa wapinzani wa Serikali ya Rais Josefu Kabila. Itakumbukwa kwamba, kunako tarehe 4 Januari 1959 wananchi wa DRC walisimama kidete kudai uhuru wao kutoka kwa Wabelgiji. Watu wengi wakamwaga damu yao na hao ndio wanaokumbukwa kila mwaka ifikapo tarehe 4 Januari. Kardinali Laurent Monsengwo Pasinya amewakumbuka mashujaa wa zamani na wale wa nyakati hizi, wanaodai uhuru, demokrasia, ustawi na maendeleo ya wengi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.