2018-01-05 09:46:00

Kardinali Stella: Wakleri kesheni, msije mkajikuta mnamezwa na giza!


Wakleri katika maisha na utume wao, wanapaswa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kristo Yesu, Kuhani mkuu na utambulisho wa mapadre, kwani Kristo ndiye Mwanga wa Mataifa aliyekuja kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, kwa njia ya Fumbo la Msalaba, yaani: mateso, kifo na ufufuko wake. Kanisa ni Fumbo la Mwili wa Kristo! Mapadre wanashiriki kikamilifu katika dhamana na utume wa Maaskofu wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Kumbe, Mababa wa Mtaguo mkuu wa Pili wa Vatican wanataka mapadre kujenga na kudumisha uhusiano wao wa dhati na Kristo Yesu, Maaskofu, Mapadre wenzao na Taifa la Mungu katika ujumla wake. Lengo ni kutekeleza: Ukuhani, Ufalme na Unabii wa Kristo; mambo yanayofumbwa kwa namna ya pekee katika Daraja Takatifu ya Upadre!

Hii ni changamoto ambayo imetolewa hivi karibuni na Kardinali Beniamino Stella, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Wakleri katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa kwa ajili ya Majandokasisi kutoka Ufaransa, wakati wa kongamano kuhusu “Utume wa Upadre tangu kwenye Nyaraka za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, Lumen Gentium yaani Mwanga wa Mataifa hadi Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, Furaha ya Upendo ndani ya Familia, Amoris laetitia”.  Kardinali Stella amewapatia Majandokasisi ushauri wa maisha ya kiroho unaowataka kuchunguza dhamiri kwa unyofu, ari na moyo mkuu, ili kuweza kujiandaa vyema katika maisha na utume wa Kipadre.

Kama ilivyokuwa wakati wa kuzaliwa kwa Kristo Yesu mjini Bethlehemu, hata Wakleri leo hii wanaweza kugubikwa na usingizi wa woga, wasi wasi na ubinafsi kiasi hata cha kushindwa kutambua kwamba amezaliwa kwa ajili yao Mwokozi ambaye ni Kristo Bwana. Kabla ya kuzaliwa kwa Kristo Yesu, takribani miaka elfu mbili iliyopita, watu walitembea katika giza la dhambi na mauti. Wakuu wa dunia waliendelea kuelemewa na ubinafsi wao, wakati ambapo wenye nyumba za wageni, walikuwa wanahangaika kutafuta faida kubwa, katika mazingira kama haya ya “patashika nguo kuchanika” Mwana wa Mungu alikuwa anazaliwa ulimwenguni.

Ni Bikira Maria, Mtakatifu Yosefu na wachungaji kondeni ndio watu waliokuwa wanakesha huku wakiwa na nyoyo wazi, tayari kumkaribisha Mwana wa Mungu katika hali ya unyenyekevu na moyo mkuu, kwa Neno wa Mungu aliyefanyika mwili na kukaa kati ya watu wake! Hata Majandokasisi katika ulimwengu mamboleo, wanapaswa kuwa macho na makini, huku wakikesha, ili wasitumbukie katika majanga yanayomwandama mwanadamu katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Amewataka kukuza na kudumisha uhusiano wao na Mwenyezi Mungu kwa njia ya: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu, Matendo ya Huruma, Toba na Wongofu wa ndani, tayari kuambata huruma na msamaha unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, ili kweli waweze kuwa ni wafuasi amini wa Kristo Kuhani Mkuu katika maisha na utume wao kama Mapadre wa baadaye!

Kardinali Stella amewakumbusha Majandokasisi mambo msingi yaliyobainishwa kwenye “Ratio Fundamentalis Institutionis Sacerdotalis” yaani “Mwongozo wa Malezi ya Kipadre, Zawadi ya Wito wa Kipadre” kuhusu malezi ya mwanzo na endelevu ili kuweza kukabiliana na changamoto katika maisha na utume wa Kipadre. Mapadre wanapaswa kuwa na utambulisho thabiti, kiasi hata cha kumshuhudia na kumtambulisha Kristo Mwana Kondoo wa Mungu anayeondoa dhambi za ulimwengu kwa njia ya maisha na utume wao wenye mvuto na mashiko kama ilivyokuwa kwa Yohane Mbatizaji. Kama Majandokasisi wanapaswa kutambua ni kitu gani wanachokitafuta katika maisha na utume wa Kipadre! Huu ni mwaliko kwa Majandokasisi kujiachilia mikononi mwa Kristo Yesu, ili aweze kuwafunda barabara kadiri ya utume na mahitaji ya Kanisa! Kama wanajitafuta wenyewe na masilahi yao binafsi; kama wanatafuta cheo, madaraka na mali, watambue kwamba, wamekosea njia, kwani Upadre ni huduma ya Neno, Sakramenti na Maisha ya watu wa Mungu, inayopaswa kutekelezwa kwa njia ya majitoleo thabiti, unyenyekevu na moyo mkuu!

Majandokasisi wanapaswa kujenga na kudumisha mahusiano ya karibu na Kristo Yesu, Kuhani mkuu wa Agano Jipya na la milele. Watambue kwamba, wao ni Kristo mwingine katika maisha na utume wao miongoni mwa watu wa Mungu. Wakleri wajenge na kudumisha utamaduni wa kupenda kusoma na kutafakari Neno la Mungu; wawe na moyo wa Sala, Ibada na Uchaji wa Mungu kwa kutambua kwamba, wao wameteuliwa kuwa ni vyombo vya wokovu kwa watu wa Mungu, dhamana inayotekelezwa kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko, mkazo unaotolewa katika mchakato wa uinjilishaji mpya. Lengo ni kuwawezesha waamini kukutana na Kristo Yesu, chemchemi ya furaha ya Injili. Ili kuweza kufanikisha yote haya pasi na kukata wala kujikatia tamaa ya maisha, kuna haja ya kuchunguza dhamiri daima, yaani kujitenga na mambo ya dunia, ili kujiweka mbele ya Mungu, kwa njia ya Sala na Tafakari. Kwa njia hii anasema, Kardinali Stella, Wakleri wanaweza kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani kama vyombo madhubuti vya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.