Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa Barani Afrika \ Amani

Kard. Onaiyekan vitendo vya kigaidi ni uhalifu dhidi ya ubinadamu!

Vitendo vya kigaidi ni uhalifu dhidi ya binadamu, utu na heshima yake. - AP

05/01/2018 09:59

Kardinali John Olorunfemi Onaiyekan, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Abuja, Nigeria anasema, vitendo vya kigaidi vinavyofanywa na Kikundi cha Boko Haram ni ukatili dhidi ya ubinadamu na kwamba, madhara yake yanajionesha kwa wananchi wote wa Nigeria bila ubaguzi wa kidini, kikabila, kijinsia au anakotoka mtu. Amani na utulivu vimetoweka nchini Nigeria kutokana na kushamiri kwa vitendo vya mashambulizi dhidi ya nyumba za ibada, utekaji nyara, ubakaji na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia! Vitendo vyote hivi vina hatarisha umoja, mshikamano na mafungamano ya wananchi wa Nigeria katika ujumla wao!

Mashambulizi yaliyofanyika tarehe 3 Januari huko Gamboru yamesababisha watu 14 kufariki dunia, wakati ambapo, waamini 17 walipoteza maisha mwanzo kabisa mwa Mwaka 2018 huko “River State”. Abubakar Shekau, Kiongozi mkuu wa Kikundi cha Kigaidi cha Boko Haram katika video iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii anasema Boko Haram inahusika na kwamba, inasadikiwa kuwa kuna zaidi ya watu 700 waliokuwa wametekwa nyara na Boko Haram wamefanikiwa kutoroka.

Kardinali John Olorunfemi Onaiyekan anasikitika kuona kwamba, Serikali iliyoko madarakani ilitangaza kiama kwa Boko Haram, lakini imepita miaka mitatu na Bioko Haram wanaendelea kusababisha majanga makubwa kwa watu na mali zao. Utawala wa sheria na haki msingi za binadamu zinaendelea kutoweka nchini Nigeria na kwamba, wananchi wamechoka na wanaweza kuanza kujichukulia sheria mikononi mwao. Jambo la msingi linalopaswa kuzingatiwa hapa ni kwamba, hivi ni vitendo vya kigaidi ambavyo ni uhalifu dhidi ya utu na heshima ya binadamu.

Kuna makundi na magenge ya kihalifu yanayoendesha kampeni za chuki na uhasama; mauaji na utekaji nyara. Matokeo yake ni kutoweka kwa amani na usalama kiasi cha kuwafanya wakulima na wafanyakazi kushindwa kutekeleza dhamana na wajibu wao barabara. Ukabila ni jambo jingine linaloibuka kwa kasi sana nchini Nigeria, hali inayoleta kinzani kati ya jamii za wakulima na wafugaji. Hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana aliwataka watu waliowateka nyara Watawa Shirika la Moyo Mtakatifu wa Kristo wa Ekaristi, kuwaachia huru watawa waliokuwa wametekwa kutoka kwenye nyumba ya Iguoriakhi, lakini hadi sasa hakuna taarifa yoyote kuhusu kuachaliwa kwako. Watekaji nyara wanataka wapewe fidia, lakini daima fidia imekuwa haitolewe ili kutoendekeza mchezo huu mchafu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.

05/01/2018 09:59