2018-01-04 08:20:00

Papa Francisko nchini Perù: chemchemi ya furaha na matumaini


Umoja, upendo na mshikamano ni kati ya bashasha zinazobubujika kutoka katika nyoyo ya familia ya Mungu nchini Perù, inayo amini katika ushirika wa watakatifu yaani: katika mambo matakatifu na kati ya watu watakatifu. Huu ni ushirika na umoja katika imani, Sakramenti za Kanisa, mapendo pamoja na karama mbali mbali ambazo Mwenyezi Mungu amewakirimia waja wake. Haya yamesemwa na Kardinali Juan Luis Cipriani Thorne, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Lima, nchini Perù, wakati huu Perù inapojiandaa kwa ajili ya ujio wa Baba Mtakatifu Francisko nchini humo kuanzia tarehe 18 – 21 Januari 2018 na kutembelea miji ya Lima, Puerto Maldonado na Trujillo, baada ya kutua na kutembelea nchini Chile kuanzia tarehe 15 hadi tarehe 18 Januari 2018.

Kauli mbiu inayoongoza hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Perù“ ni Umoja wa Matumaini”. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa njia ya video mapema mwezi Agosti, 2017 aliitaka familia ya Mungu nchini Perù kushikamana katika umoja wa matumaini. Kardinali Juan Luis Cipriani Thorne anasema kwamba umoja huu unajikita katika maombezi ya watakatifu yanayowainua waamini kutoka katika udhaifu na unyonge wao wa kibinadamu kutokana na bidii yao ya kidugu! Umoja huu unapaswa kububujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu linaliwachangamotisha kushirikiana kati yao kama familia moja ya Mungu katika Kristo Yesu.

Familia ya Mungu nchini Perù ina ibada kubwa sana kwa watakatifu kama Rose wa Lima, Martin de Porres, Bikira Maria wa Miujiza pamoja na wengine wengi ambao majina yao bado hayajaandikwa kwenye orodha ya watakatifu wanaotambuliwa rasmi na Mama Kanisa! Huu ni utajiri mkubwa wa maisha ya kiroho unaofumbatwa katika maisha na utume wa Kanisa Amerika ya Kusini. Itakumbukwa kwamba, watakatifu wa kwanza kabisa kutoka Amerika ya Kusini ni waamini wa Kanisa la Perù.

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako juu ya utunzaji wa mazingira” anakazia umuhimu wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ili kuweza kulinda na kudumisha kazi ya uumbaji dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi zinazowatumbukiza watu katika majanga asilia na umaskini mkubwa wa hali na kipato! Kardinali Juan Luis Cipriani Thorne anasema kuna haja kwa watu kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Tema hii itafafanuliwa kwa kina na mapana, Baba Mtakatifu atakapokutana na kuzungumza na wenyeji wa misitu ya Amazzonia. Uharibifu wa mazingira ni tishio kubwa kwa usalama, ustawi na maendeleo ya watu wengi duniani.

Mazingira ni kati ya changamoto kubwa zitakazojadiliwa na Mababa wa Sinodi ya Maaskofu wa Amazzonia, mwezi Oktoba 2019 ili kuliwezesha Kanisa kuibua mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji kwa wananchi mahalia wa eneo hili ambao wamesahauliwa na kwamba, uharibifu wa misitu unatishia usalama, maisha na ustawi wao kwa siku za usoni! Baba Mtakatifu Francisko ana upendo mkubwa kwa familia ya Mungu nchini Perù pamoja na moyo wao wa ibada ni kati ya mambo yanayomfurahisha sana! Itakumbukwa kwamba, hii ni ziara ya tatu kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro kutembelea nchini Perù. Kwa mara ya kwanza, Mtakatifu Yohane Paulo II alitembelea nchini Perù kunako mwaka 1985 na kurejea tena nchini humo kunako mwaka 1988 wakati wa maadhimisho ya Kongamano la Ekaristi Takatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.