2018-01-04 08:54:00

Kardinali Omella: mambo msingi ya kuzingatia kwa Mwaka 2018


Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu sanjari na Siku ya 51 ya Kuombea Amani Duniani, iliyoadhimishwa, tarehe Mosi, Januari 2018 amewataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuhakikisha kwamba Mwaka 2018 unakuwa kweli ni mwaka wa amani inayofumbatwa katika ukarimu, upendo na mshikamano kwa wakimbizi na wahamiaji; bila kuwasahau maskini. Kamwe familia ya Mungu isiyazimishe matumaini ya wakimbizi na wahamiaji ya: kupata usalama, hifadhi na maisha bora zaidi.

Kwa upande wake, Kardinali Juan Josè Omella, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Barcellona, Hispania anasema, mwaka 2018 upambwe kwa matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kama mwendelezo wa maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu, uliofunga rasmi kunako mwaka 2016. Matendo haya yawe ni sehemu ya sera na mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji zinazojikita katika toba na wongofu wa shughuli za kichungaji; ari na mwamko wa kimissionari. Huu ni utekelezaji wa mpango wa shughuli za kichungaji Jimbo kuu la Barcellona kwa kipindi cha miaka mitatu utakaozinduliwa rasmi wakati wa maadhimisho ya Sherehe ya Pasaka kwa mwaka 2018. Lengo ni kuimarisha imani kwa Kristo Mfufuka na Habari Njema ya Wokovu!

Mwaka 2018, Shirika la  Wamissionari wa Huruma ya Mungu linaadhimisha Jubilei ya Miaka 800 tangu lilipoanzishwa na Mtakatifu Petro Nolasco kwenye Jimbo kuu la Barcellona kwa ajili ya huduma kwa wafungwa, ambalo lilikuwa ni hitaji muhimu sana la kijamii kwa wakati ule, changamoto endelevu hata kwa nyakati hizi. Lengo ni kuhudumia familia ya Mungu, kujenga na kuimarisha mafungamano ya kijamii kama kielelezo makini cha imani tendaji inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu!

Changamoto ya tatu ni kuhakikisha kwamba, familia ya Mungu ndani na nje ya Jimbo kuu la Barcellona inajielekeza zaidi katika mchakato wa kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa na kimataifa. Lengo ni kudumisha amani katika maisha ya watu binafsi, familia na jamii katika ujumla wake. Watu wengi wana kiu ya amani inayofumbatwa katika: ukweli, haki, upendo na uhuru wa watoto wa Mungu. Mbiu ya amani iliyoimbwa na Malaika kutangaza kuzaliwa kwa Mwokozi, ndiye Kristo Bwana iendelea kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu kwa kudumisha amani na maridhiano kati ya watu. Kristo Yesu, Mfalme wa Amani atawale katika nyoyo za watu, ili amani ya kweli iweze kudumu katika maisha ya waja wake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.