Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa Barani Afrika \ Amani

Kardinali Kutwa: Amani ni chachu ya maendeleo endelevu ya binadamu!

Kardinali Jean Pierre Kutwa anasema, amani ya kweli ni chemchemi ya maendeleo endelevu ya binadamu! - REUTERS

04/01/2018 08:38

Amani ni chachu ya maendeleo endelevu ya binadamu; wakimbizi na wahamiaji ni watu wanaotafuta amani, hifadhi, usalama, ustawi na maendeleo yao kiroho na kimwili; amani ya kweli inapata chimbuko lake kutoka katika sakafu ya maisha ya watu kwa kuambata na kuzingatia haki msingi za binadamu na maridhiano, ili kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi! Huu ni muhtasari wa ujumbe wa Mwaka Mpya wa 2018 kutoka  kwa Kardinali Jean Pierre Kutwa, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Abijan, nchini Pwani ya Pembe. Anaitaka familia ya Mungu nchini humo kushikamana kwa dhati katika mchakato wa kutafuta, kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati yao.

Anawakumbusha umuhimu wa kutafakari tena na tena ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya Siku ya 51 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2017 anayekazia umuhimu wa kusikiliza kilio cha wakimbizi na wahamiaji na kukipatia majibu muafaka kadiri ya hali na uwezo walio nao! Anasema, hawa ni watu wanaotafuta amani baada ya kupambana na hali ngumu katika maisha yao! Hii ni changamoto pia kwa familia ya Mungu nchini Pwani ya Pembe kufanya upembezi yakinifu ili kubaini mambo ambayo yanakwamisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu, ili yaweze kutafutiwa ufumbuzi wa kutosha. Bado kuna kundi kubwa la wananchi wa Pwani ya Pembe wanaotafuta fursa za ajira na maisha bora zaidi, kiasi cha kujikuta wakilazimika kuziacha familia zao.

Kardinali Jean Pierre Kutwa anakumbusha kwamba, Pwani ya Pembe ni nchi ambayo hivi karibuni imevuka vikwazo vya kinzani na mipasuko ya ndani iliyo sababisha vita na machafuko nchini humo. Kumbe, Serikali inapaswa kudhibiti kikamilifu biashara ya silaha na umilikaji wa silaha unaoweza kuhatarisha amani, ustawi na mshikamano miongoni mwa wananchi wa Pwani ya Pembe. Kamwe, watoto wasibebeshwe silaha na kupelekwa mstari wa mbele kama chambo cha vita, kwani kufanya hivi ni kuwapoka watoto matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi.

Kardinali Jean Pierre Kutwa katika ujumbe wake kwa Mwaka Mpya wa 2018 anaitaka Serikali, vyombo vya ulinzi na usalama, Bunge na Mahakama kuhakikisha kwamba, vinatekeleza dhamana na wajibu wake barabara na hivyo kuondokana na mambo yanayokwamisha mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu: Anasema, uchu wa mali na madaraka ni hatari sana kwa amani, mshikamano na mafungamano ya kijamii. Familia ya Mungu nchini Pwani ya Pembe haina budi kushikamana kwa dhati kama kielelezo amani na utulivu, mambo msingi yanayoweza kuwavutia hata watu kutoka nje ya nchi yao. Ustawi, maendeleo na mafao ya wengi vipewe kipaumbele cha kwanza badala ya kutaliwa na ubinafsi ambao umekuwa ni chanzo cha majanga makuuu katika maisha ya wananchi wa Pwani ya Pembe. Nchi hii ni mali ya wote na kamwe haiwezi kubinafsishwa na watu wachache kwa ajili ya mafao yao binafsi. Kumbe, kila wananchi anapaswa kutekeleza dhamana na wajibu wake katika kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu, kama kweli wanataka kuona Pwani ya Pembe iking’ara na kucharuka kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News!

04/01/2018 08:38