2018-01-03 11:14:00

Vijana wa kiekumene Barani Ulaya "kutinga timu" Madrid, Hispania 2018


Vijana wa Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè kutoka sehemu mbali mbali za Ulaya, hapo tarehe Mosi, Januari 2018 wamehitimisha maadhimisho ya Siku ya 40 ya Vijana wa Kiekumene Barani Ulaya, yaliyoongozwa na kauli mbiu “Njia muhimu za kujichotea furaha ya kweli kutoka katika kisima cha wokovu”. Maadhimisho ya Siku ya 41 ya Vijana wa Kiekumene kwa Mwaka 2018 yatafanyika mjini Madrid, nchini Hispania. Maadhimisho pia yatafanyika katika miji mingine kama vile Hong Kong, nchini China, Lviv nchini Ukraine, Kemerovo, Russia na Graz. Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa mji wa Madrid kuwa mwenyeji wa maadhimisho ya Siku ya Vijana wa Kiekumene Barani Ulaya ambayo kama kawaida yataanza hapo tarehe 28 Desemba 2018 hadi tarehe Mosi, Januari 2019.

Fra Alois Mkuu wa Jumuiya ya Kiekumene ya Taize katika tafakari yake kwa umati mkubwa wa vijana waliokuwa wanahudhuria mkutano huu, amesema kwamba, kuna mambo makuu mawili yanayotishia mustakabali wa amani duniani na familia ya binadamu katika ujumla wake. Mosi ni wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji wanaolazimika kuzihama nchi zao kutokana na sababu mbali mbali ili kutafuta: hifadhi na usalama; amani, ustawi na maisha bora zaidi. Watu hawa wanahitaji kwa namna ya pekee mshikamano wa upendo na huduma, ili waweze kuwa kweli ni marafiki wa jamii inayowapatia hifadhi. Huu ni mwaliko kutoka kwa Kristo mwenyewe anayewataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuvuka mipaka ya woga na wasi wasi usiokuwa na mvuto wala mashiko pamoja na maamuzi mbele ambayo kimsingi yamekuwa ni chanzo cha maafa makubwa katika familia ya binadamu!

Fra Alois anaendelea kufafanua kwamba, athari za mabadiliko ya tabia nchi zinaendelea kuwatumbukiza watu wengi katika majanga ya maisha, umaskini na magonjwa. Nchi zilizoendelea zimechangia kwa kiasi kikubwa katika mchakato mzima wa uchafuzi wa mazingira na hivyo zinawajibika kusaidia utekelezaji wa sera na mikakati ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Kuna mikataba na itifaki za kimataifa ambazo zimetiwa sahihi, lakini bado utekelezaji wake unasua sua kutokana na masilahi ya baadhi ya wanasiasa.

Fra Alois amechukua nafasi hii kuwataka viongozi wa kisiasa, watunga sera, wachumi na wafanya biashara kuchukua hatua madhubuti zitakazosaidia kupambana na baa la umaskini duniani; uchafuzi wa mazingira pamoja na kuibua teknolojia rafiki kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Changamoto hizi mbili zinatishia amani, ustawi na maendeleo ya binadamu na hivyo, kumnyima furaha ya kweli inayobubujika kutoka katika undani wa maisha yake. Ili kuweza kutekeleza yote haya kuna haja ya kuwa na ujasiri, imani na matumaini; kila binadamu akijitahidi kutekeleza wajibu na dhamana yake ndani ya jamii. Amewataka vijana kutoka Barani Ulaya kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya maadhimisho hayo kwa Mwaka 2018 -2019.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.