Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Tafakari \ Tafakari ya Neno la Mungu

Sherehe ya Tokeo la Bwana ni Siku kuu ya ufunuo wa mwanga wa Kristo!

Sherehe ya Tokeo la Bwana ni Siku kuu ya Mwaga, ambao ni Kristo anayejifunua kwa watu wa Mataifa. - AFP

03/01/2018 14:24

Epifania ni Sherehe ya mwanga na mwanga huo ni Yesu Kristo, mwanga unaoangaza.  Mwangaza huo umewaangaza watu wote na unaendelea kuangaza.  Ni sikukuu ya mafumbo ya utoto wa Yesu – KKK 528. Mamajusi ni watu wenye busara wa mashariki ambapo baada ya kuiona nyota na kwamba Bwana amezaliwa, walienda Yerusalemu kumwabudu.  Zawadi walizochukua zilipatikana huko kwao – Yer 6,20.  Mababa wa kanisa waliona kuwa dhahabu ni mfano wa ufalme wa Kristo, uvumba ulionya umungu wake na manemane ikionya mateso yake.  Mamajusi walimsujudia Kristo na ndivyo walivyotumia maneno ya Mungu juu ya Masiya kwamba mataifa watambwabudu Mungu wa Israeli Hes 24, 17.

Ni mwanga kwa watu wote wanaomwendea Mungu wakiongozwa na imani ya huyo Mungu mwenyewe.  Katika somo la kwanza leo – Isaya 60: 1-6  -  tunapata habari juu ya utukufu wa Bwana unaong’aa Yerusalemu (ambao Neno wa Mungu utatokea)  mahali ambapo patakuwa ni makutano ya watu wote ili kumtukuza Mungu na kumtolea ubani na manemane. Leo, somo hili linadhihirisha wazi hilo.  Watu kutoka sehemu mbalimbali wakiwa na vitu mbalimbali wakienda kumtukuza Mungu.  Tunasikia habari juu ya nuru, mwanga na utukufu wa Bwana: wana na binti kutoka mbali, utukufu wa bahari na utajiri wa mataifa,  misafara ya ngamia na watu kutoka Medina wakichukua dhahabu ubani na manemane wakiutangaza ukuu wa Mungu.  Hii ndiyo Epifania ya kweli.

Katika somo la pili: Waefeso  3:2-3,5-6, tunaona kuwa kwa Waebrania walioteuliwa kwanza na kwa wapagani waliokuja baadaye wote wameitwa katika imani moja kumfuata Kristo na kugawana urithi wa milele pamoja naye.  Wokovu wa Mungu ni kwa ajili ya ulimwengu mzima.  Somo hili linazungumzia juu ya ufunuo wa siri ya Mungu ambayo Mungu alidhamiria tangu awali.  Ni mpango ambao makuhani wa kale waligusia lakini hawakujua maana kamili ya mpango huo.  Mpango huo ulikamilika tu kwa njia ya Yesu Kristo.  Katika waraka kwa waefeso  1:3-10, tunasoma juu ya wingi wa neema ya Mungu isiyopimika.  Epifania ufunuo wa Mungu kwa njia ya Kristo ndiyo maana kamili ya Maandiko Matakatifu.

Katika somo la Injili leo: Mt. 2:1-12, tunaona kuwa kutokujali na ujinga wa walimu na wakuu wa sheria, hofu na wasiwasi wa Herode imekuwa maangamizi kwao.  Jibu sahihi la mamajusi – tumeona nyota yake mashariki na tumekuja kumwabudu limekuwa wokovu wao.  Wanatoka mbali na wanapata wokovu.  Ila walio karibu hawatambui kuwa mwokozi amezaliwa na wanaangamia milele.  Somo hili lina tukumbusha kuwa ufunuo haukutokea kama hamu ya Mungu kujitosheleza bali kwa ajili yetu.  Mungu anapenda kuwa hata sisi tuuone utukufu huo hivyo tuinuke tumwelekee kama mamajusi walivyofanya.  Yahitaji pia bidii yetu.  Tujitoe sisi wenyewe kwake kama zawadi.  Hakika hatuna budi kumshukuru Mungu siku hii ya leo pamoja na Mtume Paulo kama anavyoandika katika waraka kwa Wakolosai 1:3,12-2, twamshukuru Mungu, Baba yake Bwana wetu Yesu Kristo siku zote tukiwaombea tukimshukuru Baba aliyewastahilisha kupokea sehemu ya urithi wa watakatifu katika nuru.

Maana nyingine ya Epifania ni kujionyesha au kujifunua kwa maana hiyo ya kigiriki na katika dini yao, ilikuwa desturi kwa mmoja wa miungu  kumtokea mmoja  wao. Katika maandiko matakatitifu neno hilo halipo. Bila shaka ni kuepa kuoanishwa na neno hili la kipagani. Kiyunani neno Epifania laelekezwa kwa Yesu  na kazi yake ya wokovu  mpaka siku ya mwisho. Katika 2Tim 1:10 – tunasoma hivi; lakini sasa kwa tokeo la mwokozi  wetu   Kristo Yesu neema  hiyo imefumbuliwa  kwa maana  ameshinda mauti  na ametangaza uzima wa milele  kwa Injili. Katika Tito 2:11 – maana ya neema ya mungu  iwaokowayo  wanadamu  wote imefunguliwa na  katika Tito 3:4- lakini wema wake mwokozi wetu  mungu  na upendo wake kwa mwanadamu alipofunuliwa alituokoa.

Katika Kanisa jina hili Epifania  limeonekana  karne ya 3 likitumiwa na  kwa Yesu hivyo,  hatari ya kuhusishwa na upagani ikaisha. Kwa kweli Yesu ndiye  ufunuo wa Mungu. Kanisa la mashariki likawa la kwanza  kusherehekea sikukuu ya tokeo la Bwana  likiunganisha na ubatizo  wa Yesu pale  Yordani. Itakumbukwa kuwa pale  katika tukio hilo  sauti toka mbinguni  ilisikika ikasema  huyu ndiye mwanangu mpendwa wangu  niliyependezwa naye  msikilizeni yeye – Mk1:11. Mungu kwa mara ya kwanza  anajifunua kuwa  yeye ni nani  na anajifunua  kwa njia ya Yesu  Kristo,  Mwanae wa pekee!.

Kanisa la Magharibi kwenye karne ya 4 likahusisha  hija ya mamajusi  na tokeo la Bwana  jinsi ilivyo katika Injili yetu ya leo. Mamajusi siyo Waisraeli hivyo wanawakilisha watu wote. Mungu amejionyesha kwa watu wote hata sisi tuliopo hapa na kwa namna ya pekee  ndiyo maana tupo  hapa  kusherehekea  sikukuu hii ya tokeo la Bwana. Tumshukuru Mungu kwamba  hata leo anaendelea kujionyesha kwetu. Mamajusi waliona nyota ambayo kwayo Mungu aliwaelekeza kwenda kwa motto Yesu. Leo tunapenda kuwomba Mwenyezi  Mungu   ili mimi, wewe  na sote tunaoliita jina lake  Mungu  tuwe kweli  ile nyota  ambapo watu watuonapo   katika maisha yetu  ya kumcha Mungu  waweze kutamani kumpenda  na kumtumikia yeye zaidi  ya vitu  vingine  vyote na watufuate  kama Mamajusi  ili wafike kwa Kristo.                                                                                                                                                                                                                                                             

Matokeo ya ufunuo wake Bwana ni kwamba tunawajibishwa  kuweka wazi  ushindi na utukufu wake  mbele ya dunia yote. Tunamshukuru  Mugu kwamba hata leo anaendelea kujionesha kwetu. Mamajusi waliona nyota  ambayo  kwayo Mungu aliwaelekeza  kwenda kwa Mtoto Yesu.  Katika 2Tim. 4:1-8 tunasoma – kwa ufunuo wake Kristo tunapata amri ya kuhubiri neno la Mungu ili upate taji la haki. Mwandishi mmoja anatuangalisha kuwa haitoshi tu kuujua ukweli bali zaidi sana ni jinsi gani tulivyojiandaa kutembea na kuishi ukweli huo tulioufahamu.  Haitoshi tu kujua bali yahitajika kuishi kwa imani hicho tulichokijua

Tumsifu Yesu Kristo.

Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.

Vatican News!

 

03/01/2018 14:24