Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa Barani Afrika \ Amani

Kardinali Monsengwo Pasinya alaani ukatili wa Serikali ya Rais Kabila

Baraza la Maaskofu Katoliki DRC lina laani vikali ukatili na kufuru iliyofanywa na Serikali ya Rais Josefu Kabila dhidi ya watu wake. - AP

03/01/2018 10:54

Kanisa linathamini mfumo wa kidemokrasia kwa sababu una wahakikishia wananchi ushiriki wao katika maamuzi ya kisiasa, yanayofanywa wakati wa uchaguzi mkuu na kwamba, viongozi wa kisiasa wanapaswa kutekeleza dhamana na wajibu wao kadiri ya Katiba ya nchi. Demokrasia ya kweli kadiri ya Mafundisho Jamii ya Kanisa, ambacho kimsingi ni chombo madhubuti cha uinjilishaji inajikita katika utekelezaji wa dhamana na majukumu yake kwa mujibu wa sheria za nchi sanjari na kuzingatia kanuni msingi za maisha ya kijamii ambazo ni: ukweli, uhuru na haki.

Waamini walei wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu katika mchakato wa kukuza na kudumisha haki jamii, kwa kusimama kidete kulinda haki msingi za binadamu, haki za kiraia na kisiasa! Maandamano ya amani yaliyofanyika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo, Jumapili tarehe 31 Desemba 2017 ni sehemu ya utekelezaji wa dhamana ya waamini walei katika masuala ya kisiasa na kijamii na kwamba, hii ni sehemu ya Mafundisho Jamii ya Kanisa! Huu ni ufafanuzi ambazo umetolewa na Ubalozi wa Vatican nchini DRC kufuatia mpasuko uliojitokeza kati ya waamini wa Kanisa Katoliki na Serikali ya Rais Josefu Kabila wa DRC.

Taarifa zinaonesha kwamba, watu 8 wamepoteza maisha katika mapambano kati ya waamini wa Kanisa Katoliki DRC na Vikosi vya ulinzi na usalama. Haya yalikuwa ni maandamano ya amani kutaka kumshinikiza Rais Josefu Kabila kung’atuka kutoka madarakani kama sehemu ya utekelezaji wa makubaliano ya Mkataba wa Amani uliotiwa sahihi tarehe 31 Desemba 2016. Hadi sasa hakuna dalili kwamba, uchaguzi mkuu utaweza kufanyika nchini DRC hapo tarehe 23 Desemba 2018, uchaguzi ambao ulipaswa kufanyika mwaka 2017 kama ilivyokuwa imepangwa kwenye Mkataba wa Amani uliosimamiwa kwa kiasi kikubwa na Baraza la Maaskofu Katoliki DRC.

Mktaba huo pamoja na mambo mengine, ulikuwa unaitaka Serikali kuwaachia huru wafungwa wa kisiasa na watu waliokimbilia uhamishoni kurejea ili kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa nchi yao. Licha ya maandamano kufanyika katika hali ya amani na usalama, lakini vyombo vya ulinzi na usalama vilitumia nguvu kubwa kuwasambaratisha waamini hao waliokuwa wanadai haki yao msingi! Kardinali Laurent Monsengwo Pasinya, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Kinshasa, DRC, Jumanne, tarehe 2 Januari 2018 amelaani vikali ukatili uliofanywa na Serikali ya Rais Josefu Kabila dhidi ya waandamanaji hawa pamoja na askari kufanya kufuru kwenye nyumba za ibada. Viongozi wanao wajibu wa kuwahakikishia wananchi wa: haki, amani na upendo, lakini Serikali ya Rais Kabila imefanya kinyume chake. Baraza la Maaskofu Katoliki nchini DRC limekuwa likishutumu uvunjifu wa haki msingi za binadamu; uchu wa mali na madaraka mambo ambayo ni hatari sana kwa demokrasia, ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wengi wa DRC.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News!

03/01/2018 10:54