Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Hotuba

Zaidi ya wakimbizi 5, 000 wamekufa maji wakiwa njiani kwenda Ulaya

Umoja wa Mataifa unasema zaidi ya wakimbizi 5, 000 wamekufa maji wakiwa njiani kwenda Barani Ulaya na Amerika. - REUTERS

02/01/2018 06:34

Umoja wa Mataifa unabainisha kwamba, kuna zaidi ya watu milioni 250 ambao wamelazimika kuzikimbia au kuzihama nchi zao kutokana na sababu mbali mbali. Tangu mwaka 2000, idadi hii imeendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka hadi kufikia asilimia 49% katika kipindi cha Mwaka 2017. Wahamiaji na wakimbizi wengi wanapata hifadhi nchini Marekani ambako kuna wahamiaji milioni 49.8, ikifuatiwa na Nchi za Falme za Kiarabu, Ujerumani na Russia zinazohifadhi wahamiaji zaidi ya milioni 12 na Ujerumani inayotoa hifadhi kwa wahamiaji milioni 9. Kuna nchi kadhaa Barani Afrika kama vile Tanzania zimo katika orodha nchi ambazo zimekuwa ni kimbilio kubwa kwa wakimbizi na wahamiaji Barani Afrika.

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba, katika kipindi cha mwaka 2017 zaidi ya wahamiaji elfu tano walikufa maji wakiwa njiani kuelekea Barani Ulaya na Amerika. Takwimu hizi zimekuwa zikijirudia kwa muda wa miaka mitano sasa kadiri ya taarifa iliyotolewa na Shirika la Kimataifa la Wahamiaji, IOM “International Organization for Migration”.  Kunako mwaka 2013 Jumuiya ya Kimataifa ilipigwa na mshangao mkubwa wakati ambapo wakimbizi na wahamiaji 360 walipofariki maji na kumezwa kwenye tumbo la Bahari ya Mediterannia, kaburi lisilokuwa na alama, ambalo limeendelea kuwa ni chanzo cha maafa kwa wahamiaji na wakimbizi wengi duniani.

Umoja wa Mataifa unabainisha kuwa, zaidi ya watoto 15, 000 wamejikuta wakiwa ni wakimbizi bila ya kusindikizwa na wazazi wala walezi wao, hali ambayo inahatarisha sana ustawi na makuzi ya watoto hawa ambao wengi wao wanatumbukia kwenye biashara haramu ya binadamu na viungo vyake pamoja na utumwa mamboleo. Hawa ni watoto ambao wengi wao wanatoka Barani Afrika. Wimbi la wakimbizi duniani linapaswa kusimamiwa na kuratibiwa vyema, ili kukabiliana na changamoto endelevu badala ya kujenga kuta za utengano kwa baadhi ya wanasiasa wanaotaka kujipatia umaarufu kwa kutumia migongo ya wakimbizi na wahamiaji duniani.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya 51 ya Kuombea Amani Duniani anakiri kwamba, si rahisi sana kwa watu kuweza kufungua sakafu ya nyoyo zao ili kuweza kuwapokea na kuwahudumia watu wanaoteseka na kwamba, hii ni changamoto endelevu inayopaswa kuvaliwa njuga ili kuwawezesha watu kuishi katika hali ya amani na utulivu: kwa kuwakaribisha na kuwahudumia; kwa kuwajibika kikamilifu na changamoto changamani zinazoendelea kujitokeza siku kwa siku, kwa kuzingatia kwamba, kuna “rasilimali kiduchu” ambayo inaweza kutumika katika kuwahudumia watu hawa. Kwa kuongozwa na hekima na busara, viongozi wa serikali wanapaswa kuwakaribisha, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwashirikisha kikamilifu katika maisha ya jamii husika mintarafu uwezo uliopo kwa ajili ya mafao ya wengi, ili hata wao waweze kuwa ni sehemu ya jamii mpya! Viongozi wanayo haki msingi ya kuhakikisha kwamba, watu wao wanapata maendeleo kadiri ya rasilimali iliyopo, ili hatimaye, waweze kufikia malengo yaliyobainishwa!

Mtakatifu Yohane Paulo II wakati wa Maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo, alikumbusha kwa kusema, licha ya “Mbiu kuu ya Malaika” kuhusu amani duniani kutangazwa takribani miaka 2000 iliyopita huko mjini Bethlehemu, lakini bado kuna wimbi kubwa  la vita na madhara yake; kinzani, mauaji ya kimbari na kikabila ambayo yametikisa sana karne ya ishirini na hadi sasa bado Jumuiya ya Kimataifa inaendelea kushuhudia migogoro ya kivita ndani na nje ya mipaka ya nchi mbali mbali duniani. Kiu ya kutaka ajira na maisha bora zaidi; wanafamilia kuungana ndugu zao pamoja na shahuku ya kutaka elimu bora zaidi ni kati ya mambo yanayosababisha watu kuhama nchi zao, bila kusahau: umaskini na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kudadavua hali ya wakimbizi na wahamiaji katika Ujumbe wake wa Siku ya 51 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2018 kwa kusema kwamba, kuna watu wanaotumia njia halali za uhamiaji na wengine wengi wamekuwa wakitumia njia tofauti kabisa, kiasi hata cha kutozingatia usalama hasa pale njia rasmi zinazosuasua au kukwamisha juhudi zao. Wakimbizi na wahamiaji wamekuwa wakipambana na vizingiti kwa kisingizio cha usalama wa taifa, gharama kubwa ya kuwatunza na kuwakirimia wakimbizi na wahamiaji, hali ambayo inadhalilisha utu na heshima ya watoto wa Mungu. Kuna baadhi ya wanasiasa wanaowaogopa wahamiaji na wakimbizi kiasi cha kupandikiza mbegu ya chuki na uhasama; ubaguzi na hofu isiyokuwa na tija wala mashiko badala ya kujenga madaraja ya amani. Kuna kila dalili zinazoonesha kwamba, hata kwa siku za usoni, wimbi la wakimbizi litaendelea kushamiri. Baadhi ya watu wanaliona kuwa ni tishio, lakini Baba Mtakatifu Francisko anawaalika watu hawa kuangalia wimbi hili kwa imani kama fursa ya kujenga amani duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

02/01/2018 06:34