Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Tafakari \ Tafakari ya Neno la Mungu

Sherehe ya Tokeo la Bwana! Kristo Yesu ni Mwanga wa Mataifa!

Sherehe ya Tokeo la Bwana: Zawadi: Ubani, Dhahabu na Manemane maana yake ni: Umungu, Ufalme na Ubinadamu wa Kristo Yesu, Mwanga wa Mataifa. - AFP

02/01/2018 13:49

Neno “Epifania” linatokana na neno la Kiyunani epiphainein linalomaanisha “yeye anayetokea au kung’ara”. Neno hili limetumika tangu zama za mwanzo za ukristo kumaanisha tokeo la Bwana wetu Yesu Kristo, pale alijitambulisha na kuonekana kwa Mataifa yote. Yeye ambaye bado tupo katika shamrashamra za kuzaliwa kwake anadhihirika au anajifunua si kwa wayahudi tu, jamii ambayo amezaliwa bali kwa mataifa yote. Ndiyo tulivyoagizwa na Zaburi usiku wa sherehe ya Noeli ikisema: “Wahubirini mataifa habari za utukufu wake, na watu wote habari za maajabu yake” (Zab 96:3). Wafalme wa Mashariki wanafika Yerusalemu kuja kumwona na kumsujudia mtoto, ishara ya upana wa utume wake mtoto huyu, yaani kuwa Mwanga hata miisho ya dunia.

Tafakari ya Neno la Mungu inatufafanulia vema ukuu wa Sherehe hii. Somo la kwanza linaanza kwa kuonesha ukuu wa Yerusalemu na umuhimu wake katika fumbo hili kubwa tunaloliadhimisha. “Inua macho yako, utazame pande zote; wote wanakusanyana; wanakujia wewe”. Baada ya kutoka utumwani Babeli, baada ya kukombolewa utumwani Yerusalemu inatajwa kama nuru ambayo inawaangaza mataifa yote. Dunia yote ipo katika giza kwa maana “giza litaifunika Dunia, na giza kuu litazifunika kabila za watu”. Lakini uwepo wa Yerusalemu ni matumaini kwa wote wanaokuwa katika giza kwani wanakusayika kuielekea hii nuru. Usiku wa Noeli tulisema kwamba: “watu wote waliokwenda katika giza wameona nuru kuu” (Is 9:2).

Tunapaswa kwenda zaidi na kujiuliza hiyo nuru inasababishwa na nini? Nabii Isaya anaendelea kutuambia kwamba “maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa” (Is 9:6). Mtoto huyu ni Mwokozi wetu Yesu Kristo. Yeye ndiye anayeufanya mji wa Yerusalem kung’aa na kuwafanya watu toka mbali kuja kumwona na kumsujudia. Kitabu cha Hesabu kinamwelezea Kristo kama nyota itakayozuka hapo baadaye na kuwa mwanga kwa mataifa yote. Neno la Mungu linasema: “Namwona lakini si sasa; Namtazama, lakini si karibu; Nyota itatokea katika Yakobo na fimbo ya enzi itainuka katika Israeli; Nayo itazipiga-piga pembe za Moabu, na kuwavunja-vunja wana wote wa ghasia” (Hes 24:17). Hapa tunaiona hiyo nyota katika muktadha wa ukombozi. Nyota hiyo itaipatia Israeli Nguvu na kuweza kuwashinda adui zake. Ndiyo wale wanaoshindana naye na kumvuta katika uovu.

Somo la Injili linatupatia habari za Wafalme watatu toka Mashariki ambao wanaongozwa na nyota inayoangaza katika Yerusalemu. Wanakwenda Yerusalemu na si mahala pengine kuonesha kwamba ni mahali hapo kama alivyoagua Nabii Isaya Mataifa yote yatafika na kumsujudia Mungu. Wanafika kwa Mfalme Herode na kuuliza: “Yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia”. Wafalme wa Mashariki maarufu kama Mamajusi ni watu maarufu, wataalamu wa nyota  ambao kadiri ya mapokeo walitokea mashariki ya Israeli. Hawa walimtolea mtoto Yesu zawadi ambazo ziliupambanua zaidi unasaba wake. Hawakwenda kumtembelea Mfalme kama wafalme wengine bali waliuona umungu wake.

Zawadi walizomtolea ni dhahabu kutoka Ofiri, ubani kutoka Uarabuni na manemane kutoka Ethiopia. Hizi ni  zawadi ambazo zilikuwa maarufu, zenye thamani na kuheshimika sana sana wakati wa kuzaliwa Yesu. Bila shaka inautimiza uaguzi wa Nabii Isaya tunaousikia katika somo la kwanza: “Utajiri wa mataifa utakuwasilia. Wingi wa ngamia utakufunika, ngamia vijana wa Midiani na Efa; wote watakuja kutoka Sheba; wataleta dhahabu na uvumba; na kuzitangaza sifa za Bwana. Maandiko Matakatifu yanakaza kusema, Mamajusi kutoka Mashariki ya mbali huku wakiongozwa na nyota walifika mjini Bethlehemu, wakamsujudu Bwana na kumtolea zawadi kuu tatu zinazofumbata maana na utume wa Yesu Kristo hapa ulimwenguni. Ubani unadhihirisha Umungu wa Kristo; Dhahabu inatangaza Ufalme wa Kristo na Manemane inaonesha ubinadamu wa Kristo unaokabiliwa na Fumbo la mateso, kifo na ufufuko.

Waraka wa Mtume Paulo kwa Waefeso unasakafia ukweli huu kwamba ahadi ya kuletwa Mkombozi Yesu Kristo, haikuwa kwa ajili ya Waisraeli tu bali kwa ajili ya Mataifa yote. Hivyo migawanyiko yoyote ya kidini au rangi inafutwa na ujio wa Kristo. Yeye anakuwa sababu wa kuwaunganisha wanadamu wote kwa kuwa wote wanaunganishwa katika mwili mmoja wa Kristo, yaani Kanisa. Mtume Paulo ambaye anaheshimika kama Mtume wa Mataifa anaupokea ufunuo kwa njia ya neema. Hivyo katika mantiki hiyo anadokeza waziwazi kwamba hata watu wa mataifa ambao walihesabika kama wapagani katika Israeli wanawezeshwa kuipokea habari njema ya wokovu kwa njia ya mahubiri ya Injili na kuunganishwa katika Yerusalemu mpya yaani, Kanisa kwa njia ya imani. Hivyo nao wanakuwa na haki ya kuurithi ufalme wa kimasiha unaoletwa na Kristo kwani kwa kuja kwake  mwanga mkubwa umeizukia dunia yote.

Kanisa ni Yerusalemu mpya ambayo inaangaza Mwanga wa Kristo kwa watu wote. Kanisa katika Mtaguso mkuu wa pili wa Vatican uliitambua hii haiba yake pale lilipoonesha hamu yake ya “kuitangaza Injili kwa kila kiumbe ili kuufikisha mwanga wa Kristo kwa kila kiumbe, mwangaza ambao unang’ara katika nyua zake” (Mwanga wa Mataifa, n.1). Hapa ndipo tunauchota wajibu wetu wa kikristo katika adhimisho la leo. Sisi tulio wabatizwa ambao tunalifanya jengo hili Kanisa kuwa hai tunapewa hadhi hiyo ya kuwa nuru ya kuwaangazia watu wengine. Kila mmoja katika nafasi yake anaalikwa kuwa nyota au nuru ya kuing’arisha Yerusalemu mpya na hivyo kuwavuta wote kuielekea nuru hiyo. Huu ni wajibu mahsusi katikati ya jamii ambayo ipo gizani.

Kwa asili viumbe vinapokuwa katika giza vinakuwa na hulka ya kujielekeza katika mwanga. Sisi hatupaswi kubaki ndani ya pango lenye giza kama yule anayelezewa na wanafalsafa wa kale Plato. Kristo aliyezaliwa ndani mwetu anapaswa kuuhishwa na kutufanya tung’ae na kuwavuta wengine. Tusifanane na wale waliokuwa katika Yerusalemu ambao bado wamefumbwa macho yao na wanashindwa kuuona mwanga huo. Herode na watu wengine wa Israeli wanawakilisha jamii ya mwanadamu iliyo pinzani katika kuupokea ufalme wa Mungu, jamii ambayo inaukataa ukweli wa Mungu na kumfanya mwanadamu kuwa mkuu na Bwana wa ulimwengu huu. Sisi tuishi kama wana wa nuru kwani Kristo amezaliwa mioyoni mwetu. Mfano wa maisha yetu mema yenye utajiri wa tunu za kikristo ni mwanga wa kuwaangazia watu wote na sababu ya kuwavuta na kukusanyika katika Kristo.

Mimi ni Padre Joseph Peter Mosha,

Vatican News!

02/01/2018 13:49