2018-01-02 07:23:00

Patriaki Bartolomeo I: waamini wa dini mbali mbali dumisheni umoja!


Viongozi wa kidini wanapaswa kushirikiana kwa karibu sana na viongozi wa serikali, wanasiasa na viongozi wa kijamii, ili kujenga na kudumisha utamaduni wa mshikamano, ambao ni muhimu sana katika kukuza na kudumisha utu, heshima, ustawi na maendeleo ya wengi. Haya yamesemwa hivi karibuni na Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox katika ujumbe wake kwa washiriki wa mkutano wa kimataifa kuhusu “Mwaka wa Mshikamano wa Kiislam: umuhimu wa majadiliano ya kidini na kitamaduni”.

Mkutano huu umefanyika huko Baku, nchini Azerbaigian. Katika ujumbe huo, anafafanua kwa kina na mapana dhamana na mchango wa viongozi wa kidini katika masuala ya kijamii, hususan katika kipindi hiki cha utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Hakuna mshikamano wa dhati pasi na majadiliano katika ukweli na uwazi ili kupambana fika na changamoto ya misimamo mikali ya kidini inayoendelea kuibuka miongoni mwa waamini mbali mbali duniani. Viongozi wa dini hawana budi kukuza na kudumisha mchakato wa majadiliano ya kidini, yatakayosaidia kujenga na kuimarisha umoja, upendo na mshikamano miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali duniani.

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anakumbusha kwamba, Mababa wa Sinodi Kuu ya Kanisa la Kiorthodox iliyoadhimishwa kunako mwaka 2016, kama sauti ya kinabii, walikazia umuhimu wa majadiliano ya kidini kama chachu ya maendeleo endelevu ya binadamu, haki, amani na upatanisho kati ya Watu wa Mataifa. Mama Kanisa kwa upande wake, anapenda kuhakikisha kwamba, amani itokayo juu mbinguni, inamwilishwa katika uhalisia wa maisha ya binadamu. Amani ya kweli, hailindwi kwa mtutu wa bunduki wala kwa makombora ya masafa marefu na mafupi, bali kwa njia ya upendo unaotafuta ustawi, mafao na maendeleo ya wengi. Mafuta ya imani yanapaswa kutumika kwa ajili ya kuganga na kuponya majereha ya jirani na wala si kwa ajili ya kuwasha moto wa chuki na uhasama kati ya watu!

Mshikamano wa kweli ni msingi madhubuti wa tunu msingi za maisha ya kijamii yanayofumbatwa katika: uhuru wa kweli, upendo, haki na amani. Ni nguzo imara inayotetea utu, heshima na haki msingi za binadamu dhidi ya mipasuko na kinzani mbali mbali inayoweza kujitokeza ndani ya jamii. Amani na utulivu wa familia ya Mungu katika ulimwengu mamboleo inafumbatwa kwa namna ya pekee kabisa katika utamaduni wa mshikamano wa dhati pamoja na majadiliano ya kidini yanayofanywa na waamini mbali mbali ili kujenga upendo unaowaunganisha na kuwashikamanisha watu licha ya tofauti zao msingi!

Dini zisaidie pia mchakato wa utunzaji bora wa mazingira, nyumba ya wote kwa kuwajibikiana na kusaidiana. Patriaki Bartolomeo wa kwanza anasema, vijana wa kizazi kipya wanayo haki ya kuwa na ulimwengu bora zaidi usiogubikwa na misimamo mikali ya kidini na kiimani. Ulimwengu usiokuwa na uchafuzi na uharibifu wa mazingira; vita, kinzani na mipasuko mbali mbali ya kidini, kijamii, kisiasa na kikabila, mambo ambayo yanahatarisha sana haki msingi za binadamu, ustawi na maendeleo ya wengi. Ulimwengu kwa hakika, unapaswa kusimikwa katika utamaduni wa mshikamano. Kutokana na kinzani mbali mbali za kidini sehemu mbali mbali za dunia, kuna haja ya kuendeleza majadiliano katika ukweli na uwazi na waamini wa dini ya Kiislam, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya Watu wa Mataifa. Hii ndiyo changamoto iliyotolewa na viongozi wa Kanisa katika mkutano wa amani duniani uliofanyika kwenye Chuo Kikuu cha Al-Azhar, kilichoko Cairo, Misri, na kuhudhuriwa pia na Baba Mtakatifu Francisko, mwezi Aprili, 2017.

Majadiliano ya kidini yanatambua na kuthamini tofauti msingi za tamaduni kati ya waamini wa dini mbali mbali; yanapania kukuza na kudumisha: haki, amani na maridhiano kati ya watu, ili kujenga utamaduni wa mshikamano, ushirikiano, umoja na udugu kati ya watu na tamaduni zao. Majadiliano ya kidini, yanatambua na kuthamini imani za watu kwa kuheshimiana na kuthaminiana. Kwa njia hii, majadiliano ya kidini yanasaidia kuondokana na maamuzi mbele na hali ya kudhaniana vibaya ambayo imekuwa ni chanzo cha chuki, uhasama, nyanyaso na madhulumu ya kidini sehemu mbali mbali za dunia Majadiliano ya kidini ni chemchemi madhubuti ya mshikamano kati ya Watu wa Mataifa na wala si tishio la utambulisho wa dini na imani za watu. Huu ni utajiri unaowasukuma waamini kushikamana kwa pamoja ili kukabiliana na changamoto mamboleo katika ukweli na uwazi; utu na heshima ya binadamu vikipewa msukumo wa pekee kabisa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.