2018-01-02 11:24:00

Papa anawatakia watu wote amani na baraka za mwaka mpya 2018!


Mara baada ya sala ya Malaika wa Bwana, tarehe Mosi, Januari 2018 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Baba Mtakatifu Francisko, ameendelea kusema kwamba,katika mwanzo wa mwaka 2018 anayo shauku ya kuwatakia wote kila jema katika mwaka mpya. Na zaidi kumshukuru Rais wa Jamhuri ya nchi ya Italia kwa matashi mema aliyompatia usiku wa tarehe 31 Desemba 2017, akiwa anatoa ujumbe wa matashi mema kwa wananchi wote wa Italia kwa mwaka mpya. Baba Mtakatifu anasema kuwa,watu wote waongozwe na utulivu na amani pia kuangazwa na baraka za Mungu.

Ameshukuru kuanzishwa kwa mambo mengi ya sala na matendo ya amani ambayo yameandaliwa sehemu mbali mbali za dunia kwa sababu ya tukio la Maadhimisho ya Siku ya Amani Duniani. Kwa namna ya pekee maandamano ya kitaifa ambayo yalifanyika katika kilima kimoja mjini Roma yaliyoandaliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia (CEI) wakishirikiana na Caritas ya Italia, Pax Christ na Chama Cha kitume Katoliki cha Vijana. Amewasalimia washiriki wote na kuwatia moyo waendelee mbele kwa furaha katika jitihada hizo za mshikano, hasa katika sehemu za pembezoni mwa miji kwa ajili ya kuleta amani ya kuishi. Halikadhalika kwa mahujaji wote kutoka sehemu mbalimbali za dunia kwa namna ya pekee kutoka  New York, bendi ya muziki kutoka Califonia na kikundi cha Pro Loco cha Massalengo. Kwa wote amemalizia akiwatakia  matashi mema ya mwaka2018  wa amani na neema ya Bwana na ulinzi wa umama Maria, Mama Mtakatifu wa Mungu.

Sr Angela Rwezaula
Vatican News

 








All the contents on this site are copyrighted ©.