Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Habari \ Habari za Kimataifa

Bi Henrietta Fore, Mkurugenzi mkuu wa UNICEF aanza kazi rasmi 2018

Bi Henrietta Fore ametetuliwa na Umoja wa Mataifa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa UNICEF. - EPA

02/01/2018 11:42

Bi Henrietta Fore, aliyeteuliwa hivi karibuni na Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Guterres kuwa Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, tarehe Mosi, Januari 2018 ameanza kazi yake rasmi. Anasema,  amepewa heshima kubwa na Jumuiya ya Kimataifa kuweza kuliongoza Shirika hili muhimu sana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watoto duniani. Anapenda kushirikiana na wadau mbali mbali katika kulinda na kudumisha maisha ya watoto sehemu mbali mbali za dunia.

Ni wajibu wa UNICEF kuhakikisha kwamba, haki msingi za watoto zinalindwa na kuendelezwa pamoja na kuwajengea uwezo wa kukuza na kutumia mapaji yao kwa ajili ya mafao ya jamii nzima! Katibu mkuu wa Umoja wa Umoja wa Mataifa amemteua Bi Henrieta Fore kutoka Marekani, baada ya kupata ushauri kutoka kwa Baraza kuu la UNICEF. Bi Fore ni kiongozi mwenye ujuzi na uzoefu mkubwa katika masuala ya uongozi hasa katika masuala ya huduma za kijamii, kwani amewahi kuwa Mkurugenzi mkuu wa USAID kati ya mwaka 2007 hadi mwaka 2009. Amewahi kuwa ni mshauri wa mambo ya nchi za nje nchini Marekani kati ya mwaka 2005 hadi mwaka 2007.  

Bi Fore amewahi kuwa mkurugenzi wa “United States Mint”  kati ya mwaka 2001 hadi mwaka 2005. Amewahi pia kuwa Mkurugenzi mwambata katika sekta ya uwekezaji binafsi na “Millennium Challenge Corparation”. Kwa ufupi ni kiongozi mwenye uzoefu mpana sana katika huduma za kijamii. Tarehe 31 Desemba 2017 Bi Henrietta Fore ameng’atuka kutoka katika nyadhifa nyingine zote ili aweze kujielekeza zaidi katika uongozi kwa Shirika la UNICEF linalokabiliana na changamoto mbali mbali katika ustawi, maendeleo na makuzi ya watoto wadogo. Mkurugenzi mpya wa UNICEF ameolewa na kubahatika kupata watoto wanne! Alifanikiwa kupata Shahada ya uzamivu katika historia kutoka Chuo cha Wellesley na alibahatika pia kupata shahada ya uzamili katika masuala ya uongozi wa umma kutoka Chuo Kikuu cha “Northern Colorado” nchini Marekani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.

02/01/2018 11:42