Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Mahubiri

Mwaka 2017 ulikuwa ni zawadi safi, lakini umeharibiwa kwa vita!

Papa Francisko: Mwaka 2017 ulikuwa ni zawadi safi sana kutoka kwa Mwenyezi Mungu, lakini mwanadamu ameuchafua kwa matendo ya kifo, uwongo na ukosefu wa haki msingi za binadamu, kinyume kabisa cha maisha ya binadamu, ukweli na udugu. - REUTERS

01/01/2018 10:30

Baba Mtakatifu Francisko amekikunja kilago cha Mwaka 2017: kwa Ibada ya Masifu ya kwanza ya Jioni, Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu, Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu pamoja na Utenzi wa Shukrani kwa Mwenyezi Mungu, maarufu kama “Te Deum”. Ibada hii imeadhimishwa, Jumapili jioni, tarehe 31 Desemba 2017 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na kuhudhuriwa na umati mkubwa wa familia ya Mungu kutoka ndani na nje ya Italia. Baba Mtakatifu baadaye alitembelea Pango la Noeli lililoko kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, ambalo kwa Mwaka huu, linabeba tema ya “Matendo ya Huruma”.

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amesema, hata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mwenyezi Mungu alimtuma Mwanawe na kwamba, maadhimisho ya Ibada ya Masifu ya Jioni ni kielelezo cha utimilifu wa wakati na wala si kwamba, hii ni siku ya mwisho ya mwaka, bali ni kwa sababu imani imewawezesha waamini kutafakari na kusikiliza kwamba, Kristo Yesu, Neno wa Mungu aliyefanyika Mwili, ametimiliza wakati na historia ya mwanadamu kwa kuzaliwa na Bikira Maria, Mama wa Mungu, anayejulikana na Mababa wa Kanisa kama “Theotokos”. Kwa njia ya moyo mnyenyekevu wa Bikira Maria, uliosheheni imani na kwa njia ya Roho Mtakatifu, amefanikisha mchakato wa utimilifu wa nyakati!

Kanisa limerithi na linaendelea kurithi utambuzi huu wa ndani kabisa wa maisha ya mwanadamu unaorutubishwa na moyo wa shukrani, kama njia na jibu muafaka kwa zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ni shukrani inayopata chimbuko lake katika tafakari ya Mtoto Yesu aliyelazwa kwenye Pango la kulishia wanyama; anayewakumbatia na kuwaambata watu wote! Ni Mwana wa Baba wa milele anayemshirikisha mtu mmoja mmoja na kuwaambata watu wote. Katika mazingira yaliyotengenezwa na Roho Mtakatifu, waamini wanathubutu kumtolea Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kutambua kwamba, mema na mazuri yote yanatoka kwa Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Mwaka 2017 ulioyoyoma ulikuwa ni zawadi safi na kamilifu kutoka kwa Mwenyezi Mungu aliyokabidhiwa binadamu. Lakini, kwa njia mbali mbali, mwanadamu ameuharibu kwa matendo ya kifo, uwongo na ukosefu wa haki. Vita ni kielelezo cha kiburi cha mwanadamu kama ilivyo kwa matukio yote ambayo yanakwenda kinyume kabisa cha maisha ya binadamu, ukweli na udugu; mambo ambayo yana athari zake katika utu, jamii na mazingira. Waamini wanapaswa kuwajibika mbele ya Mungu, jirani na katika kazi ya uumbaji. Lakini, kwenye Masifu ya Jioni, Baba Mtakatifu anasema, kipaumbele cha kwanza ni neema ya Kristo Yesu inayong’ara ndani ya Bikira Maria. Lakini, kama Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Roma, anawajibika kuwafikiria wakazi wa Roma.

Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru na kuwapongeza wakazi wa Roma ambao kila siku wanachangia ustawi na maendeleo ya mji; kwa kutekeleza wajibu wao barabara; kwa kuwa na malengo makini na busara wanaposafiri; watu wanaoheshimu maeneo ya hadhara; kwa kuonesha pale ambapo mambo hayaendi sawa sawa; kwa kuwasaidia wazee na watu wenye shida mbali mbali. Haya ni kati ya mambo mengi yanayo onesha upendo kwa mji wa Roma, ushuhuda makini wa elimu bora ya uraia inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kila siku. Kwa njia hii, hata katika ukimya wao, wanashiriki kudumisha mafao ya wengi!

Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza wazazi, walimu na walezi wote wanaotekeleza dhamana na wajibu wao katika mwelekeo sahihi wa maisha, kwa kujitahidi kuwafunza watoto na vijana maana ya uraia, kanuni maadili ya uwajibikaji na zaidi kwa kuwafunda ili waweze kujisikia kuwa ni sehemu ya mji; kwa kujihudumia na kujali ukweli unao wazunguka. Watu hawa, hata kama hawavumi, lakini wamo na ni sehemu ya wakazi wa mji wa Roma. Kwa bahati mbaya, wamo ambao wana kabiliana na hali ngumu ya uchumi, lakini si watu wanao lalama na kumezwa na chuki; lakini wanajibidisha kila siku kutekeleza wajibu na dhamana yao, ili kuweza kuboresha hali hii! Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anasema, waamini wanapomwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa shukrani, wanapaswa kutambua na kuthamini mchango wa “wajenzi wa mafao ya wengi”, wanao upenda mji wao si kwa maneno, bali kwa njia ya ushuhuda wa matendo yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kila siku!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

01/01/2018 10:30