2017-12-31 08:30:00

Mshikamano na Wakristo wa Misri kutokana na mashambulizi ya kigaidi


Patriaki Tawadros II wa Kanisa la Kikoptik la Kiorthodoxnchini Misri, kwa ujasiri mkubwa anapenda kusema, hakuna tukio ambalo litaweza kuwapokonya Wakristo furaha ya kuzaliwa kwa Kristo Yesu, Mwana wa Mungu. Mapambano dhidi ya vita na vitendo vya kigaidi yanajikita katika majadiliano yanayofumbatwa katika misingi ya ukweli na uwazi; kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Inasikitisha kuona kwamba, kuna watu wanataka kuchafua usalama, amani na utulivu kwa kutumia dhana mbaya ya dini. Kimsingi, dini inapaswa kuwa ni chombo cha haki, amani, upendo na maridhiano kati ya watu na wala si vinginevyo!

Patriaki Tawadros II ameyasema haya kufuatia mashambilizi mawili ya kigaidi yaliyofanyika mwishoni mwa juma huko mjini Helwan na Cairo, nchini Misri na kusababisha watu kadhaa kupoteza maisha na wengine wengi kujeruhiwa. Anawataka waamini kusimama kidete katika imani na matumaini, wakati huu wanapojiandaa kuadhimisha Fumbo la Umwilisho, hapo tarehe 7 Januari 2018. Kutokana na mashambulizi haya, watu wengi wameanza kuwa na hofu na wasi wasi ya mashambulizi wakati wa kipindi hiki cha Siku kuu ya Mwaka Mpya 2018 na Noeli ya Kanisa la Kiorthodox.  Ulinzi na usalama vinaendelea kuimarishwa nchini Misri hasa wakati huu, Kanisa la Kiorthodox linapojiandaa kuzindua Kanisa kuu la Kiorthodox huko Cairo, tukio ambalo linatarajiwa kuhudhuriwa na Rais Abdel Fattah Al Sisi wa Misri.

Wakati huo huo, Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Majadiliano ya Kiekumene amelaani vikali mashambulizi haya ya kigaidi kwa kusema, kwamba,  zawadi kubwa ambayo Wakristo wanaweza kutoa ulimwenguni ni ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Wakristo nchini Misri wanapambana na hali ngumu ya maisha, lakini wameendelea kuwa ni mashuhuda wa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Kuna uhusiano mzuri kati ya Patriaki Tawadros II na Baba Mtakatifu Francisko na kwamba, hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Cairo, imeimarisha mchakato wa majadiliano ya uekumene wa damu, huduma, maisha ya kiroho na sala!

Naye Askofu mkuu Bruno Musarò, Balozi wa Vatican nchini Misri ansema kwamba, Serikali ya Misri inaendelea kuimarisha ulinzi na usalama kwa ajili ya Makanisa! Jambo la kushangaza wengi ni utamaduni wa kusamehe unaoshuhudiwa na Wakristo huko Misri. Viongozi mbali mbali wa kidini na kiserikali wamelaani sana mashambulizi haya ya kigaidi na kwamba, wanapenda kuonesha mshikamano wao wa dhati na Wakristo huko nchini Misri.

Kwa bahati mbaya anasema Askofu msataafu Anba Antonios Aziz Mina wa Jimbo la Guizeh, nchini Misri kwamba, kuna baadhi ya watu wanadhani kwamba, Wakristo wamezoea kushambuliwa kila wakati, kiasi kwamba, mioyo yao imegeukwa kuwa kama jiwe! Lakini, watu wanapaswa kukumbuka kwamba, kuna idadi ya watu wanaofariki dunia pamoja na majanga makubwa yanayosambaza majonzi na simanzi kwa watu mbali mbali, kiasi cha kuwapokonya amani, utulivu na usalama. Mashambulizi ya kigaidi yanapania kuwapokonya Wakristo furaha ya Noeli, ili kuwajengnea hofu, mashaka na huzuni moyoni! Muujiza mkubwa ambao Wakristo wanaweza kuushuhudia huko Misri ni kuendelea kuwa ni chemchemi ya furaha, imani na matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake! Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kutoa nafasi ya pekee kwa matukio yanayopania kujenga na kudumisha amani duniani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.