2017-12-30 09:22:00

Wamissionari 23 wameuwawa kikatili katika kipindi cha Mwaka 2017


Taarifa ya Shirika la Habari za Kimissionari, Fides inasema kwamba, kuna wamissionari 23 waliouwawa kikatili wakati wakitangaza na kushuhudia  Habari Njema ya Wokovu, sehemu mbali mbali za dunia katika kipindi cha Mwaka 2017. Kwa muda wa miaka nane sasa, Amerika inaongoza kwa mauaji ya wamissionari duniani na kwamba, mwaka huu kuna wamissionari 8 waliouwawa. Bara la Afrika linashika nafasi ya pili kwa mauaji ya wamissionari10 na Barani Asia, wameuwawa wamissionari 2.

Mashirika ya Kipapa ya Kazi za Kimissionari linasema kwamba, tangu mwaka 2000 hadi mwaka 2016, takwimu zinaonesha kwamba, kuna wamissionari 424 waliuwawa kikatili na kati yao kuna Maaskofu 5. Uchunguzi unaonesha kwamba, wamissionari wengi wameuwawa katika matukio ambayo yanahusiana sana na ujambazi, utekaji nyara na wizi katika maeneo ya Kanisa. Umaskini na hali ngumu ya kiuchumi, utepetevu wa kanuni maadili na utu wema; uchafuzi wa mazingira ni kati ya mambo ambayo yanahatarisha zawadi ya maisha. Lakini, ikumbukwe kwamba, wamissionari hawa ni watu wanaojisadaka kwa ajili ya huduma ya Neno la Mungu linaloshuhudiwa katika huduma makini katika sekta mbali mbali za maisha ya binadamu kama kielelezo cha matumaini ya Kiinjili. Fides linahitimisha taarifa yake kwa kusema kwamba, katika takwimu hizi hakuna dalili za mauaji kutokana na chuki ya imani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.