Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Nyaraka

Ujumbe wa Papa Francisko kwa Siku ya 51 ya Kuombea Amani Duniani 2018

Papa Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya 51 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2018 anasema, wakimbizi na wahamiaji na watu wanaotafuta amani duniani. - AFP

30/12/2017 07:51

Utukufu kwa Mungu juu mbinguni na amani duniani kwa watu wenye mapenzi mema, ni ujumbe makini uliotolewa na Malaika wakati wa Noeli ile ya kwanza kwa watu wote, lakini hasa kwa wale wanaotamani zaidi amani duniani kwa nyakati hizi. Hawa si wengine bali ni wakimbizi na wahamiaji, ambao kwa sasa ni zaidi ya wahamiaji milioni 250 na kati yao kuna wakimbizi milioni 22.5 walioenea sehemu mbali mbali za dunia. Hawa ni watu wanaotafuta mahali salama ili waweze kuishi kwa amani na utulivu, kiasi hata cha kuthubutu kuhatarisha maisha yao kwa safari ndefu ambazo zimejaa magumu na mahangaiko makubwa; ni watu wanaokubana na uzio wa nyaya za umeme na kuta zinazowakatisha tamaa ya kuweza kufikia lengo la maisha yao! Ni watu wanaokimbia nchi na makazi yao kutokana na: vita na baa la njaa; nyanyaso mbali mbali na vitendo vya ubaguzi, dhuluma, umaskini pamoja na uharibifu mkubwa wa mazingira.

Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya 51 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2018 sanjari na Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu, inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe Mosi, Januari. Maadhimisho ya mwaka 2018 yanaongozwa na kauli mbiu “Wahamiaji na wakimbizi ni watu wanaotafuta amani”. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa mwaka 2018 anajielekeza zaidi katika tafakari ya mambo msingi yanayosababisha wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani; umuhimu wa kutafakari changamoto hii ya Jumuiya ya Kimataifa kwa kutambua kwamba hata wao ni sehemu ya familia kubwa ya binadamu, wanazo haki zao msingi na kwamba, hata wao wanaweza kuchangia ustawi na maendeleo ya nchi wahisani.

Kumbe, kuna haja ya kukazia zaidi umuhimu wa kuwakaribisha, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwashirikisha katika maisha ya jamii inayowakirimia wanapokuwa ughaibuni! Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa utekelezaji wa Mkataba wa Kimataifa kuhusu usalama wa wahamiaji wenye mpangilio thabiti na kwamba, kuna haja ya kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa binadamu wanaoishi katika nyumba ya wote!

Baba Mtakatifu Francisko anakiri kwamba, si rahisi sana kwa watu kuweza kufungua sakafu ya nyoyo zao ili kuweza kuwapokea na kuwahudumia watu wanaoteseka na kwamba, hii ni changamoto endelevu inayopaswa kuvaliwa njuga ili kuwawezesha watu kuishi katika hali ya amani na utulivu: kwa kuwakaribisha na kuwahudumia; kwa kuwajibika kikamilifu na changamoto changamani zinazoendelea kujitokeza siku kwa siku, kwa kuzingatia kwamba, kuna “rasilimali kiduchu” ambayo inaweza kutumika katika kuwahudumia watu hawa. Kwa kuongozwa na hekima na busara, viongozi wa serikali wanapaswa kuwakaribisha, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwashirikisha kikamilifu katika maisha ya jamii husika mintarafu uwezo uliopo kwa ajili ya mafao ya wengi, ili hata wao waweze kuwa ni sehemu ya jamii mpya! Viongozi wanayo haki msingi ya kuhakikisha kwamba, watu wao wanapata maendeleo kadiri ya rasilimali iliyopo, ili hatimaye, waweze kufikia malengo yaliyobainishwa!

Mtakatifu Yohane Paulo II wakati wa Maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo, alikumbusha kwa kusema, licha ya “Mbiu kuu ya Malaika” kuhusu amani duniani kutangazwa takribani miaka 2000 iliyopita huko mjini Bethlehemu, lakini bado kuna wimbi kubwa  la vita na madhara yake; kinzani, mauaji ya kimbari na kikabila ambayo yametikisa sana karne ya ishirini na hadi sasa bado Jumuiya ya Kimataifa inaendelea kushuhudia migogoro ya kivita ndani na nje ya mipaka ya nchi mbali mbali duniani. Kiu ya kutaka ajira na maisha bora zaidi; wanafamilia kuungana ndugu zao pamoja na shahuku ya kutaka elimu bora zaidi ni kati ya mambo yanayosababisha watu kuhama nchi zao, bila kusahau: umaskini na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kudadavua hali ya wakimbizi na wahamiaji katika Ujumbe wake wa Siku ya 51 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2018 kwa kusema kwamba, kuna watu wanaotumia njia halali za uhamiaji na wengine wengi wamekuwa wakitumia njia tofauti kabisa, kiasi hata cha kutozingatia usalama hasa pale njia rasmi zinazosuasua au kukwamisha juhudi zao. Wakimbizi na wahamiaji wamekuwa wakipambana na vizingiti kwa kisingizio cha usalama wa taifa, gharama kubwa ya kuwatunza na kuwakirimia wakimbizi na wahamiaji, hali ambayo inadhalilisha utu na heshima ya watoto wa Mungu.

Kuna baadhi ya wanasiasa wanaowaogopa wahamiaji na wakimbizi kiasi cha kupandikiza mbegu ya chuki na uhasama; ubaguzi na hofu isiyokuwa na tija wala mashiko badala ya kujenga madaraja ya amani. Kuna kila dalili zinazoonesha kwamba, hata kwa siku za usoni, wimbi la wakimbizi litaendelea kushamiri. Baadhi ya watu wanaliona kuwa ni tishio, lakini Baba Mtakatifu Francisko anawaalika watu hawa kuangalia wimbi hili kwa imani kama fursa ya kujenga amani duniani.

Wakimbizi na wahamiaji ni sehemu ya familia moja ya binadamu, wenyeji wanaowakaribisha na kuwakirimu wote kwa pamoja wanayo haki ya kufurahia mema ya dunia kama Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayobainisha: kwa kukazia mshikamano unaoratibu haki na amani mambo msingi yanayodumisha maisha ya watu. Miji inapaswa kuwa ni mahali pa kukuza na kudumisha mshikamano, udugu, wema, ukweli na haki; mambo msingi yanayosaidia ukuzaji wa amani. Baba Mtakatifu anakaza kusema, hata wakimbizi na wahamiaji wanao utajiri na amana wanayobeba katika maisha yao: wanao utamaduni na kipaji cha ugunduzi; ni watu wanaojiojituma na kujisadaka sana, kiasi hata cha kuchangia ustawi na mendeleo ya nchi wahisani hata zile ambazo zina rasilimali “kiduchu” hata kuweza kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji kwa kiwango kikubwa! Kumbe, viongozi wa serikali wanapaswa pia kujenga utamaduni wa ukarimu kadiri ya uwezo wa nchi zao, huku wakisukumwa na ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kwa watu wanaowaza na kufikiri katika mwelekeo kama huu anasema Baba Mtakatifu Francisko wanaweza kutambua kwamba, wanapandikiza na kukuza mbegu ya amani duniani na hatimaye, wakimbizi na wahamiaji watakuwa ni “vitalu” vya amani.

Baba Mtakatifu anakazia mbinu mkakati unaopaswa kufanyiwa kazi na Jumuiya ya Kimataifa kwa kuhakikisha kwamba, inatoa fursa kwa watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa, wakimbizi na wahamiaji: kwa kuwakaribisha kwani kwa kufanya hivi, watu wengi wamewakaribisha Malaika hata bila ya wao kutambua! Utu, heshima na haki zao msingi zinapaswa kulindwa na kudumishwa na wote. Kuna haja ya kuwa na mikakati ya maendeleo endelevu kwa wakimbizi na wahamiaji: kwa kuhakikisha kwamba, watoto wao wanapata elimu bora ili kuwajengea uwezo wa kujadiliana kwa kina na mapana. Mwishoni, wakimbizi na wahamiaji wanapaswa kushirikishwa kikamilifu katika maisha ya jamii mpya inayokarbisha, ili kutajirishana kwa njia ya ushirikiana na huduma makini.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, Umoja wa Mataifa katika kipindi cha Mwaka 2018 utatoa muswada na hatimaye kutoa Mkataba wa Kimataifa kuhusu; usalama, taratibu na kanuni za uhamiaji na Mkataba wa pili utawahusu wakimbizi. Mikataba hii inapaswa kusimikwa katika: huruma, mwono mpana na ujasiri, ili kutumia kila fursa inayojitokeza kwa ajili ya kudumisha mchakato wa ujenzi wa amani duniani, ili kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kudumisha majadiliano na uratibu ili kuwahudumia vyema wakimbizi na wahamiaji. Kitengo cha wakimbizi na wahamiaji cha Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu kimechapisha mbinu ishirini zinazoposwa kuvaliwa njuga na Jumuiya za Kikristo pamoja na jamii nzima katika ujumla wake. Hii ni sehemu ya mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji kwa ajili ya Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha Ujumbe wake wa Siku ya 51 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2018 kwa kusema kwamba, ikiwa kama wakimbizi na wahamiaji watashirikishwa kikamilifu, “ndoto ya amani duniani” inaweza kutimia, kwa watu kujenga umoja wa familia ya binadamu ulimwenguni. Jambo hili si nadharia inayoelea kwenye ombwe! Kanisa linamkumbuka Mtakatifu Francis Xavier Cabrini, kwa kutimiza miaka 100 tangu alipofariki dunia. Ni mwanamke wa shoka, aliyesimama kidete kwa ajili ya huduma kwa wahamiaji, kiasi cha kutangazwa kuwa ni Msimamizi wa wahamiaji. Amewafundisha watu jinsi ya kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwashirikisha wakimbizi na wahamiaji katika sera na mikakati ya maendeleo endelevu, kiasi hata cha kupandikiza mbegu ya amani kwa wale wanaojenga amani duniani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.

30/12/2017 07:51