Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Tafakari \ Tafakari ya Neno la Mungu

Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu

Bikira Maria ni Mama wa Mungu "Theotokos" - RV

30/12/2017 08:12

Tarehe 1 Januari huitimisha Oktava ya Sherehe ya Noeli. Siku hii inapambwa kwa mchanyato wa maadhimisho matatu. Kiliturujia tunaadhimisha Sherehe ya Maria Mtakatifu Mama wa Mungu, katika mfululizo siku maalum za sala mbalimbali za Kanisa leo ni Siku ya kuombea Amani duniani na katika kalenda ya kawaida ya kijamii leo ni siku ya Mwaka Mpya wa 2018.

Antifona ya mwanzo inatupatia kwa ufupi sifa za umama wa Bikira Maria. “Salamu, Mama mtakatifu wa Mungu, uliyemzaa Mfalme mwenye kutawala mbingu na Dunia daima na milele. Maria ni Mama wa Mungu (Theotokos) kwa sababu ya utii wake kwa ujumbe wa Malaika. Utayari na ujasiri wake wa kusema ndiyo ulimwezesha kuchukua mimba na kumzaa Kristo, Mungu kweli na mtu kweli. Tulichoadhimisha siku nane zilizopita ni kuzaliwa kwa Kristo ambaye katika nafsi yake umungu na ubinadamu vimeungana katika namna ya fumbo. Wanatauhidi wengi wamejaribu kulifafanua fumbo hili na kuonesha kwamba katika nafsi ya Kristo asili zote mbili huonekana au huwa pamoja. Katika matukio yote ya kihistoria Yesu Kristo yu katika asili zote mbili, yaani umungu na ubinadamu wake vinakuwepo. Hivyo wakati wa kuzaliwa kwake Yeye anayemzaa ingawa anaeleweka kumzaa Kristo kama wanadamu wengine wanavyozaliwa lakini pia anamzaa Mungu na hivyo tunaiona mantiki ya umama wake.

Somo la pili la Liturujia ya leo linatupatia mwanga. “Ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria, kusudi awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili sisi tupokee hali ya kuwa wana”. Sehemu hii ya maandiko matakatifu inaonesha moja kwa moja kwamba Mungu anazaliwa na mwanamke. Kuzaliwa na mwanamke kunathibitisha ubinadamu wake lakini pia tukitafakari kwamba anayezaliwa ni Mwana wa Mungu hapa tunaiona moja kwa moja namna yake ya fumbo, yaani Mungu anazaliwa mwanadamu kamili katika tumbo la Bikira Maria. Lakini somo hili linakwenda mbele zaidi na kutuonesha sababu za Mungu kuzaliwa na mwanamke: kusudi kutukomboa sisi wanadamu na kutufanya kuwa wana wa Mungu. Kumbe umama wa Bikira Maria ni wa manufaa kwetu kwani tunarudishiwa hadhi tuliyoipoteza sababu ya dhambi, hadhi ya kuwa watakatifu na tunaongezewa cheo kingine cha juu kabisa cha kufanywa wana warithi wa Mungu.

Somo la Injili ya leo linatuonesha namna ambavyo huyu mtoto aliyezaliwa alivyopokelewa na kushirikishwa tamaduni na mila za wakati wake. Kadiri ya taratibu zao mtoto alipozaliwa alifanyiwa mambo kadhaa ambayo kwayo aliingizwa rasmi ndani ya jamii. Kwanza ni kutairiwa na kupewa jina, tukio ambalo lilifanyika siku nane baada ya kuzaliwa (Rejea Lk 2:21). Pili ni kutolewa hekaluni na kutakaswa kwa mama tukio ambao linafanyika siku 40 baada ya kuzaliwa mtoto (Rej Lk 12:2 – 8). Kwa nafasi ya kwanza hii ilimfanya kuwa mmoja wa watu wa jamii yake. Ilimfanya kutoonekana kuwa ni mtu wa ajabu au mtu wa kipekee. Hatua hizi ziliuthibitisha ubinadamu wa Kristo na hivyo kuupatia uzito umama wa Bikira Maria kwamba aliyemzaa ni binadamu kama watu wengine wa jamii yake.

Lakini Injili inatuambia kwamba wakati Wachungaji pamoja na watu wengine wakistaajabu juu ya tukio hilo kwa furaha Maria aliyaweka “maneno hayo yote, akiyafikiri moyoni mwake”. Hapa katika namna iliyofichika tunafunuliwa juu ya umungu wa Kristo na hivyo kumfanya Maria kuwa pia Mama wa Mungu. Wachungaji walishuhudia walichoambiwa na malaika akisema: “Leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana” (Lk 2:11). Baada ya kumwona mtoto na wazazi wake tunaambiwa “walirudi huku wakimtukuza Mungu na kumsifu kwa mambo yote waliyoyasikia na kuyaona”. Habari hii kwao inawafanya kuwa mashuhuda wa kwanza wa kuzaliwa kwa Masiha na hivyo wakatoka kwa haraka kwenda kuitangaza habari hii ya furaha.

Kwa upande wa pili tunaye Mama yetu Bikira Maria ambaye tunaambiwa alikuwa anayafikiri hayo yanayoshuhudiwa na Wachungaji. Bila shaka anarudi nyuma na kuyakumbuka maneno ya Malaika aliyemwambia: “Roho Mtakatifu atakujia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu” (Rej Lk 1:35). Hapa anaunganisha ujumbe huu wa Malaika na ushuhuda wa wachungaji na kuona ukuu wa Mungu ulivyotendeka juu yake. Kwamba yeye binadamu amepata hadhi ya kumzaa Mwana wa Mungu. Hatilii shaka hata kidogo kwamba uzao wake huu wa kwanza unauunganisha kwa namna ya ajabu umungu na ubinadamu na hivyo kuwa sababu ya ukombozi wa wanadamu. Hii ndiyo maana anapewa jina Yesu kama alivyoagizwa na Malaika na ndivyo alivyoagizwa pia Mtakatifu Yosefu katika njozi akiambiwa: “Yosefu, mwana wa Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao” (Mt 1:20 – 21).

Leo pia tunauanza Mwaka mpya wa 2018. Kitabu cha hesabu katika somo la kwanza kinatuonesha baraka ya kikuhani iliyotolewa na Haruni kwa wana wa Israeli. Baraka hii ilitolewa baada ya kutolea sadaka kwa Mungu kuashiria kuhitimisha ngwe moja na kuomba uangalizi na usaidizi wa Mungu kwa ngwe nyingine inayoanza. Baraka hii ilitolewa kila baada ya sadaka ya jioni iliyoashiria shukrani kwa Mungu kwa wema na fadhili zake. Hapa mmoja aliweza kwenda mbele katika hatua nyingine angali akijitegemeza katika baraka na amani itokayo kwa Mungu. Neno baraka toka asili yake katika lugha ya kiebrania barak lilimaanisha kuongezewa, kumiminiwa zaidi, kujazwa zaidi, na neno amani toka asili yake katika lugha ya kiyunani shalom lilimaanisha ujumla wa hali anayokuwa nayo yeye aliyekirimiwa. Ni hali ambayo ilimpeleka mbali zaidi ya vile anavyomiliki, yaani kuuona uwepo wa Yeye aliyemkirimia. Bila shaka hii ndiyo hali ya kila mmoja wetu anapoingia katika Mwaka mpya. Tunamshukuru Mungu kwa wema na fadhili zake kwa mwaka uliopita na kuomba msamaha pale tulipomkosea na pili tunamwomba baraka na amani yake kwa mwaka mpya tunaouanza.

Tunapomshangilia Maria kama Mama wa Mungu na kama nilivyodokeza hapo awali tunaalikwa pia kuombea amani ulimwenguni kote. Leo ni siku ya 51 ya kuombea amani. Tukio hili linaunganishwa na matukio hayo mawili tuliyoyatafakari hapo juu. Katika sala ya kikuhani ya Haruni tumeomba tukisema: “Bwana akuinuilie uso wake, na kukupa amani”. Amani hiyo ambayo ni uwepo kamilifu wa Mungu kati yetu unafunuliwa na fumbo tunaloadhimisha kipindi hiki. Mwana wa Mungu amekuja kwetu na kukaa kati yetu. Yeye ni Emanueli yaani Mungu pamoja nasi. Hivyo amani yetu inakaa pamoja nasi. Usiku wa Noeli tulimshangilia Kristo tukisema: “Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, tumepewa mtoto mwanamume; naye ataitwa jina lake… Mfalme wa amani” (Is 9:6). Yeye ni kweli Mfalme wa amani kwani uwepo wake kati yetu wanadamu anakuwa chanzo cha upatanisho. Mwanadamu aliyekamatwa na kongwa la utumwa wa shetani ni aghalabu kutafuta na kustawisha uelewano na wenzake. Moja ya madhara makubwa na ya moja kwa moja ya dhambi ni kututengenezea kila mmoja utawala wake binafsi. Tunapogongana katika maslahi yetu haya binafsi basi hutokea vita na kutokuelewana. Kristo Mfalme wa amani anatuletea utawala wa Mungu kati yetu na hivyo sote tunaelekezwa katika njia moja. Sote tunapewa kipimo cha aina moja au kisima kimoja cha kuchota maana ya maisha yetu. Hapa ndipo tunapoiona amani ikichipuka. Kwani Mungu anakuwa yote katika yote.

Tumwombe Bikira Maria, mama wa Mungu na mama yetu pia kusudi uwepo wa Mungu udhihirike katika maisha yetu. Yeye aliye Malikia wa amani atuombee kwa Mwanaye Yesu Kristo ambaye ndiye amani yetu halisi kusudi tunapouanza mwaka huu wa 2018 tujazwe na uwepo wake na kuitunza amani kwa manufaa ya jamii nzima ya wanadamu. Ninawatakieni nyote mwanzo mwema wa Mwaka mpya wa 2018.

Mimi  ni Padre Joseph Peter Mosha, 

Vatican News!

30/12/2017 08:12