Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Hotuba

Padre Raymond Tapiwa Mupa ateuliwa kuwa Askofu wa Jimbo la Chinhoyi

Papa Francisko amemteua Padre Raymond Tapiwa Mupa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Chinhoyi, Zimbabwe. - AFP

30/12/2017 11:06

Baba Mtakatifu Francisko amemteua Mheshimiwa Sana Padre Raymond Tapiwa Mupa, CSs.R, kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Chinhoyi, lililoko nchini Zimbabwe. Kabla ya kuteuliwa kwake, Askofu mteule alikuwa ni Mkuu wa Shirika la Mungu Mkombozi, Kanda ya Harare, Zimbabwe. Askofu mteule alizaliwa tarehe 28 Aprili 1970 huko Tamirepi, Jimbo Katoliki la Masvingo. Baada ya masomo yake ya falsafa, kunako mwaka 1996 alijiunga na Shirika la Mungu Mwokozi na kuendelea na majiundo ya kitawa na hatimaye, kuweka nadhiri zake za daima mwaka 2001 na tarehe 4 Agosti 2001 akapewa Daraja Takatifu la Upadre, huko Harare, Zimbabwe.

Tangu wakati huo, katika maisha na utume wake kama Padre amekuwa Paroko usu, wakati ambapo aliendelea na masomo ya falsafa na hatimaye kufuzu kujipatia Shahada ya Uzamili katika falsafa kutoka “St. Augustine’s College”, kilichoko Afrika ya Kusini. Kati ya mwaka 2005 hadi mwaka 2007 aliteuliwa kuwa Paroko na kati ya Mwaka 2007 hadi mwaka 2010 aliendelea na masomo ya juu zaidi katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Alfonsianum na kujipatia tena Shahada yaUzamili katika Taalimungu maadili. Kati ya mwaka 2010 hadi mwaka 2014 amekuwa Jaalimu wa maadili na Sheria za Kanisa kwenye Chuo cha “Holy Trinity”, kilichoko Harare, nchini Zimbabwe. Kati ya Mwaka 2014 hadi mwaka 2015 aliteuliwa kuwa Makamu wa Gombera, Chuo cha “Holy Trinity” na baadaye akachaguliwa kuwa Mkuu wa Shirika la Mungu Mkombozi, Kanda ya Harare, Zimbabwe, utume ambao ameendelea kuwa nao hadi alipoteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Chinhoyi, Zimbabwe.

Na Padre Richard. A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

30/12/2017 11:06