2017-12-30 14:39:00

Familia ya Mungu nchini Tanzania dumisheni: haki, amani na maridhiano


Askofu Mkuu Beatus Kinyaiya wa Jimbo kuu la Dodoma, anawataka watanzania kujenga utamaduni wa haki, amani na maridhiano kati ya watu yanayofumbatwa katika ukweli na uwazi kama chemchemi ya amani ya kweli, umoja na mshikamano wa kitaifa! Kristo Yesu, Neno wa Mungu aliyezaliwa mjini Bethlehemu ni chemchemi ya haki, amani, upendo na mshikamano kati ya watu wa mataifa. Watanzania wametakiwa kulinda na kudumisha amani si kwa maneno tu, bali kwa kuhakikisha kwamba, matendo yao ya kila siku yanafumbata kwa namna ya pekee, misingi ya haki, msamaha wa kweli na upatanisho; mambo msingi yanayoweza kuganga na kuponya majeraha ya chuki, uhasama na kinzani ambazo hazina mashiko wala tija kwa ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wengi!

Watanzania wasitumie mianya ya sherehe kwa ajili ya kukomoana, bali iwe ni fursa ya kujenga na kudumisha umoja, upendo, udugu na mshikamano wa kweli! Kipindi cha Noeli, kiiwezeshe familia ya Mungu nchini Tanzania kuwa ni shuhuda na vyombo vya haki, amani na maridhiano, ili kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya kifamilia, kiroho na kiutu! Wazazi na walezi, wajitahidi kuwa karibu zaidi na watoto wao katika kipindi hiki cha likizo, ili kuwasaidia katika majiundo yao: kiroho na kimwili! Wazazi watenge muda wa kukaa na kuzungumza na watoto wao, kwa kutambua kwamba, familia ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kweli! Wazazi wawasaidie watoto wao kujenga utamaduni wa maadili na utu wema; kwa kujiheshimu na kuwaheshimu watu wengine ndani ya jamii; kwa kuzingatia mila na tamaduni njema za kitanzania na kiafrika ili kuondokana na tabia ya kuiga mambo ya kigeni ambayo yanaendelea kusababisha kumong’onyoka kwa misingi bora ya kimaadili na utu wema!

Askofu Mkuu Beatus Kinyaiya ameyasema haya wakati wa mahubiri yake kwenye Ibada ya Misa Takatifu wakati wa Sherehe ya Noeli sanjari na uzinduzi wa Parokia mpya ya Mtakatifu Petro, Mtume, “Swaswa kwa wasomi”, Jimbo Kuu la Dodoma na kumsimika Padre Antipas Shayo kuwa Paroko wa kwanza wa Parokia hii. Askofu Mkuu Kinyaiya amevitaka vyama vya kitume Parokiani hapo kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa, hususan katika mchakato mzima wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili, ili kweli iweze kuwa ni Parokia bora na mfano wa kuigwa na Parokia nyingine Jimbo kuu la Dodoma.

Katika Sherehe ya Noeli, Askofu Mkuu Kinyaiya alitoa Sakramenti ya Ubatizo kwa watoto 55, waliozaliwa kwa maji na Roho Mtakatifu. Watoto hawa wameondolewa dhambi ya asili ambayo kimsingi ni utupu na ukosefu wa neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Akawaimarisha wakristo 15 kwa Sakramenti ya Kipaimara, tayari kuwa ni mashuhuda wa Kristo na Kanisa lake; askari shupavu wa imani na maadili. Alibariki Ndoa Takatifu kwa familia nne ambazo zimetakiwa kuiga mfano wa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu kwa kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya kifamilia. Familia moja, imeadhimisha kumbu kumbu ya miaka 40 ya Ndoa Takatifu, mfano bora wa kuiga kwa vijana wa kizazi kipya kwamba, inawezekana kufanya maamuzi magumu katika maisha kwa kujikita katika unyenyekevu, uvumilivu, upendo. Askofu Kinyaiya amebariki Pango la Bikira Maria pamoja na sanamu ya Mtakatifu Petro, Mtume, visakramenti kwa ajili ya waamini wa Parokia mpya ya Swaswa kwa wasomi!

Na Rodrick Minja,

Jimbo kuu la Dodoma.








All the contents on this site are copyrighted ©.