Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Vatican \ Hotuba

Papa Francisko anawataka wafungwa kuandika ukurasa mpya wa maisha yao!

Papa Francisko anawataka wafungwa kumfungulia Kristo Yesu malango ya maisha yao ili kuandika upya historia ya maisha yao! - ANSA

29/12/2017 16:34

Baba Mtakatifu Francisko amewatumia salam na matashi mema ya Noeli na Mwaka Mpya 2018 wafungwa wote wanaotumikia adhabu zao kwenye Gereza kuu la Latina, lililoko mjini Roma. Amewapatia pia baraka wafungwa pamoja na familia za ona kamwe wasikate tamaa katika maisha, bali wawe na ujasiri wa kuanza tena kuandika kurasa safi za maisha yao, baada ya kumaliza kutumikia vifungo vyao! Noeli ni muda muafaka wa kufungua akili na nyoyo kwa ajili ya kumkaribisha Mtoto Yesu, tayari kuondokana na chuki pamoja na uhasama; hali ya kukata kulipiza kisasi na badala yake, kuanza kujenga utamaduni wa haki, amani, upatanisho na msamaha unaobubujika kutoka katika sakafu ya maisha yao!

Huu ni ujumbe uliotolewa na Monsinyo Yoannis Lahzi Gaid, katibu muhtasi wa Baba Mtakatifu Francisko. Noeli iwe ni fursa ya kutoka katika giza la maisha na kuanza kutembea katika mwanga wa imani, matumaini na mapendo; kwa kukumbatia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo hasa kwa watoto wadogo kama alivyofanya Mfalme Herode, kiongozi anayekumbukwa kutokana na ukatili wake! Viongozi wa mataifa wanapaswa kujenga moyo wa unyenyekevu kwa kuondokana na kiburi cha kudhani kwamba, wao ni miungu wadogo.

Viongozi waondokane na uchu wa mali na madaraka kwa kujikita katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Noeli kiwe ni kipindi cha furaha, haki, amani, upendo na mshikamano kati ya watu na wala si mzigo mzito wa “kubebeshwa Mnyamwezi”. Hiki ni kipindi cha imani na matumaini yanayowawezesha waamini kutembea katika mwanga wa Injili ya Kristo. Hata katika maisha yao ndani ya gereza, waendelee kukesha na kusali; kutubu na kumwongokea Mungu, ili waweze kuwa ni watu wapya zaidi. Matumaini kamwe hayana kuta wala vizingiti katika maisha ya waamini. Huu ni mwaliko wa kujifunza kutoka katika Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu.  Ni watu waliokumbana na changamoto mbali mbali za maisha, lakini wanakasimama kidete kwa kumtegemea na kumtumainia Mwenyezi Mungu.

Waamini wanakumbushwa kujenga na kudumisha fadhila ya unyenyekevu, upole na uchaji wa Mungu, ili waweze kukutana na Neno wa Mungu aliyefanyika mwili na kukaa kati ya watu wake! Fumbo la Umwilisho liwe ni chemchemi ya huruma, upendo na mshikamano na maskini sehemu mbali mbali za dunia; liwasidie watu kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na maridhiano kati ya watu! Monsinyo Yoannis Lahzi Gaid, Katibu muhtasi wa Baba Mtakatifu Francisko amewatakia wafungwa wote heri na baraka ya Noeli na Mwaka Mpya 2018.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

29/12/2017 16:34