2017-12-28 15:01:00

Ujumbe wa Maaskofu Katoliki Tanzania: Iweni wakala wa haki na amani!


Wapendwa wana wa Familia ya Mungu, Malaika waliotangaza kuzaliwa kwa Mkombozi kwa wachungaji usiku wa Noeli ya kwanza, walihitimisha tangazo lao la habari njema ya furaha kuu kwa utenzi wa sifa na kumtukuza Mungu:“Atukuzwe Mungu juu; na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia” (Lk.2:14).Yesu Kristo ni kweli Mfalme wa amani – alimpatanisha mwanadamu na Mungu kwa kuuchukua mzigo wa dhambi za wanadamu, aliamuru watu wapatane kabla hawajathubutu kuisogelea altare kwa ajili ya kutolea sadaka na kuabudu, na maisha yake yote hapa duniani yalipambwa kwa matendo ya amani ikiwamo kusamehe, kuponya, kufariji, na kufundisha au kuelimisha. Matendo hayo yote yanapaswa kuwa endelevu wakati wote na popote. Kila mwenye kuguswa na sherehe za Noeli anapaswa kuwa wakala wa matendo hayo ya amani.

A. MUNGU PAMOJA NASI

1. Alifanyika mwili, akakaa kwetu

Noeli ni sherehe kubwa sana kwetu sote kwa sababu ni sherehe ya kukumbuka ya kuzaliwa kwake Bwana, Yesu Kristo, Mkombozi wetu. Tunapoisali Kanuni ya Imani, tunainama kwa heshima tunapotamka maneno haya: “Akatwaa mwili kwa uwezo wa Roho Mtakatifu kwake yeye Bikira Maria, akawa mwanadamu”(Rej. Kanuni ya Misa kadiri ya Misale ya Kiroma). Katika imani nyingi za jadi, Mungu alifikiriwa kuwa mbali sana na wanadamu. Kutokana na umbali huo ilitakiwa kupanda ngazi nyingi ili kumfikia. Ngazi hizo zilikuwa za namna gani? Ngazi hizo zilikuwa washenga mbalimbali. Tofauti na imani za jadi, jambo la pekee sana katika imani ya Kikristo ni hili:Mwana wa Mungu alitwaa mwili, akakaa kati ya wanadamu (rej. Yn.1:14). Kwa hiyo wanadamu waliweza kumwita Mungu wao “Imanueli, yaani, Mungu pamoja nasi” (Mt. 1:23). Ni bahati iliyoje kuwa na Mungu anayekaa na watu wake. Kutokana na bahati hiyo, yatupasa kusherehekea kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Yesu kwa furaha, ngoma na vifijo.

Papo hapo inatupasa kuzingatia ukweli unaombatana na tukio hilo, nao ni huu: Mungu alimteua Maria wa Nazareti achukue mimba na kumzaa mtoto mwanaume na hilo lilitendeka kwa uwezo wa Roho Mtakatifu (rej. Lk. 1:35). Kwa uteuzi huo Maria wa Nazareti alipewa jukumu kubwa sana na hivyo anastahili kuenziwa sana katika kipindi cha kuadhimisha sikukuu ya kuzaliwa kwa Mkombozi wetu, Yesu Kristo. Lakini ni jambo la kusikitisha sana kusikia watu wakitoa maneno ya kashfa na dhihaka dhidi ya Maria Mama wa Yesu. Maneno hayo ni kama: “Maria ni mwanamke tu kama wanawake wengine; Maria ni kama bahasha tu iliyobeba barua (Yesu) baada ya kuiondoa na kuisoma barua, bahasha haina umuhimu tena; au Maria alikataliwa na mwanae aliyemwambia ‘Mwanamke nina nini nawe?’” Maneno ya kashfa na kubeza kama haya yanatolewa hasa na watu wenye mlengo fulani tofauti na imani ya Kanisa Katoliki. Katika salamu hizi za Noeli ya mwaka 2017 napenda kwanza kutafakari juu ya mchango mkubwa wa Maria wa Nazareti katika suala la ukombozi wa wanadamu, na hatimaye niwasilishe salaam na matashi mema ya sherehe.

2. Mchango mkubwa wa Mama Bikira Maria: Mchango wa kwanza wa Maria wa Nazareti ulikuwa kutoa kibali chake kwa ombi aliloletewa kwa njia ya Malaika Gabrieli. Alikubali kwa kusema, “Tazama mimi ni mjakazi wa Bwana na iwe kwangu kama ulivyosema” (Lk 1:38). Tunaweza kusema kibali hicho kilifungua mlango wa wokovu wetu. Tujiulize,“kama mlango huu usingelifunguliwa mambo yangekuwaje?” Kibali cha Maria wa Nazareti lazima kipewe uzito unaostahili. Hakulazimishwa kusema, “na iwe kwangu kama ulivyosema”! Kama tunasema kwa sauti kubwa na majigambo kuwa tumempokea Yesu kama Mwokozi na Mkombozi wetu binafsi, tutawezaje hapo hapo kumdharau yule aliyekubali kuchukua mimba na kumzaa Mwokozi na Mkombozi huyo? Wahenga walitufundisha: “Ukipenda uyoga penda na kichuguu.”

Mchango wa pili wa Maria wa Nazareti ulikuwa kulinda uhai wa mtoto Yesu. Muda mfupi baada ya kuzaliwa kwake, uhai wa Yesu ulikuwa hatarini. Kiongozi mwanasiasa, Mfalme Herode, alipata habari kuwa alizaliwa Mfalme wa Wayahudi. Taarifa hiyo ilipokelewa na mtawala Mroma kama tishio kwa utawala wa Roma. Mfalme Herode alichukua hatua ya “kuwaua watoto wote wanaume waliokuwako huko Bethlehemu na viungani mwake mwote, tangu wenye miaka miwili na waliopungua” (Mt 2:16). Mungu alimwelekeza Yusufu amchukue Maria na mwanae wakimbilie Misri, wakae huko hata atakapokufa Herode. Huo ulikuwa mwanzo wa maisha magumu ya Yesu Kristo.

Lakini pia kwa mchango huo wa Mama Maria kwa kushirikiana na Yusufu, wa kulinda uhai wa mtoto Yesu, tunakumbushwa na kukaziwa kuwa Familia ni mahala pa kuishi utakatifu wa maisha; mahala ambapo uhai – zawadi kutoka kwa Mungu – inapokelewa vizuri na kulindwa dhidi ya hatari nyingi zinazoizingira. Kwa hiyo Familia inao wajibu ambao hauna mbadala wa kujenga na kukuza utamaduni wa uhai dhidi ya njia mbalimbali za kuungamiza. Tunapinga na kulaani vikali kila aina ya mbinu na jitihada zinazofanywa na asasi na taasisi mbalimbali za kimataifa na kitaifa, mashirika mbalimbali ya umma na binafsi, mamlaka mbalimbali za serikali, lakini pia mtu mmoja mmoja katika kuendekeza maangamizi ya uhai au utamaduni wa kifo – uundwaji na utumiaji wa sera, sheria na taratibu zisizo rafiki kwa utamaduni wa uhai, utumiaji wa mpango wa uzazi usio rafiki kwa utamaduni wa uhai, utoaji mimba, ushoga, utoaji elimu ya utamaduni wa kifo mashuleni na taasisi zingine za mafunzo na malezi.

Katika mwelekeo huo huo, kufuatia dhambi ya mwanadamu, uhusiano unaounganisha ulimwengu na Mwenyezi Mungu umeharibika. Na kwa sababu hiyo binadamu anadhani kuwa hana uhusiano wa karibu na mazingira anamoishi, na kwa hiyo haangalii uhai wa mazingira – anaharibu misitu, vyanzo vya maji; anatumia teknolojia zisizo rafiki kwa uhai wa mazingira. Kumbe kwa jitihada za Mama Maria na Yusufu katika kuulinda uhai wa Mkombozi wa ulimwengu – watu na mazingira wanamoishi – katika fursa hii ya maadhimisho ya Noeli, tunakumbushwa wajibu wetu wa kutetea uhai wa mazingira. Kristo alikuja kuuhuisha ulimwengu ulioharibiwa. Ujio wake ulileta uhai mpya na mazingira mapya ulimwenguni; zawadi hiyo kwetu sharti iwe endelevu kwa kuujali utamaduni wa uhai wa watu na ule wa mazingira.

Mchango wa tatu wa Maria kwa Yesu Kristo ni ushirikiano wake na Yusufu katika kumlea mtoto Yesu kadiri ya misingi ya dini ya kiyahudi, yaani, kumtahiri siku ya nane na kumpa jina (Lk 2:21), kumtolea Hekaluni (Lk 2:22 – 24), kumpeleka Yerusalemu kuhiji alipofikia umri wa miaka 12. Na mchango wa nne ni ule wa Maria kufuatilia kwa makini mwenendo wa kazi ya Yesu hata akashiriki mateso yake hadi mlimani Golgotha. Hapo alikabidhiwa pia jukumu muhimu la kuwa mama wa wanafunzi wake Yesu na hatimaye alishuhudia kifo chake.

3. Himizo

Ndugu wana wa Familia ya Mungu, hakuna sababu ya kutikiswa katika imani yetu kuhusu nafasi ya Mama Maria. Yeye amechangia kwa ukubwa sana wakovu wetu:

· Alikubali kuchukua mimba ya mtoto Yesu kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.

· Alisalimisha uhai wa mtoto Yesu ulipotishiwa kuangamizwa.

· Alimlea mtotoYesu kiimani, na katika mila na desturi zenye tija.

· Alishiriki mateso yake na aliupokea wajibu wa kuwatunza wanafunzi wa Yesu.

Hizo ni sababu tosha za kutufanya waamini wa Yesu Kristo wote tumshukuru, tumpende na tumheshimu Mama Maria.

Wapendwa wana wa Familia ya Mungu; tunaposheherekea kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Bwana wetu Yesu Kristo, yatupasa kuukumbuka mchango wa Maria katika sherehe hiyo. Halikuwa lengo langu kuwaondoa toka sherehe ya kuzaliwa Yesu Kristo na kuwapeleka kwenye sherehe ya Bikira Maria. La hasha! Ni lengo langu kusisitiza kuwa: hatuwezi kumsifu na kumtukuza Yesu Kristo na papo hapo kumbeza Mama wa Yesu Kristo kiasi cha kumwona Mama huyo kuwa ni kama bahasha tu. Hiyo ni kashfa kubwa sana dhidi ya Mama Maria na ni ufukara katika ufahamu wa nafasi ya Mama Maria katika mpango mzima wa Mungu wa kumkomboa mwanadamu. Yeye mwenyewe alikiri aliposema, “Bwana amenitendea makuu” (rej. Lk.1:49). Sisi ni nani hata tumdharau huyo aliyetendewa makuu na Bwana Mungu wetu?! Yeye alibarikiwa kuliko wanawake wote (rej. Lk. 1:42). Ni nani sisi hata tuseme Maria alikuwa mwanamke wa kawaida kama wanawake wengine tu au bahasha tu ya kuchukulia barua?!

B. ZAWADI YA AMANI

1. Yesu ameleta amani

Kama tulivyopata kuwausia hapo awali mada inayotawala katika maadhimisho haya ya Noeli ni ujio wa kwanza wa Yesu Kristo, Mkombozi wa ulimwengu. Ujio wake ulitangazwa kuwa ni tukio linaloleta amani ulimwenguni, na kwa watu wote. Yesu alipozaliwa, malaika aliwapasha habari wachungaji akisema,“msiogope kwa kuwa mimi ninawaletea habari njema ya furaha kuu itakayokuwa kwa watu wote” (Lk. 2:10). Hiyo ilikuwa habari ya kuzaliwa Mwokozi wa ulimwengu, ndiye Kristo Bwana. Kisha jeshi la malaika lilimsifu Mungu na kusema, “Atukuzwe Mungu juu mbinguni, na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia” (Lk 2:14). Ujio wa Yesu ulileta zawadi siku ya Noeli. Zawadi kubwa sana tunayoweza kupeana ni AMANI ambayo ni zao la UPATANISHO. Katika adhimisho la Misa Takatifu kuna ule mwaliko unaotamkwa “mpeane amani” ndipo washiriki hupeana amani kwa kushikana mikono au kwa ishara nyingine. Sisi sote ni wakala wa matendo ya amani, na hivi ni wajibu wetu kuyashirikisha hayo kwa wenzetu daima. Kwa hiyo, na kipekee, katika maadhimisho yote ndani ya kipindi chote cha Noeli, tendo la kupeana amani lichukue uzito wa pekee. Duniani iwe amani, katika jumuiya iwe amani, katika familia iwe amani, kati ya watu wawili iwe amani, ndani ya moyo wa kila mtu iwe amani.

Yesu alipozaliwa, nchi yake ilikuwa chini ya utawala wa Roma. Amani ilitakiwa kati ya Waroma na Waisraeli, ndiyo maana Yesu hakuanzisha wala kuunga mkono mapambano ya kivita dhidi ya Waroma. Kulikuwa na uadui mkubwa kati ya waisraeli wa Yudea na Galilaya dhidi ya Wasamaria. Yesu alikataa kushusha moto juu ya Wasamaria hata kama Wasamaria walikataa kumpokea Yesu katika kijiji chao(rej. Lk 9:51- 56). Yalikuwa makundi yenye uhasama kati yao. Wafarisayo dhidi ya Watoza ushuru, Wazelote dhidi ya Wasadukayo. Yesu hakujihusisha na kundi lolote katika kulichukia kundi jingine. Isitoshe, ulimwengu wa dini ya Waisraeli uliwagawa watu katika makundi makuu mawili: taifa la Mungu (Waisraeli wenyewe) dhidi ya mataifa mengine. Tofauti hiyo ilielezwa pia kwa lugha nyingine kama anavyopambanua Mtume Paulo: Waisraeli – watu walio karibu na Mungu, watu wenye tumaini, watu waliotahiriwa; na watu wa mataifa mengine – watu walio mbali na Mungu, watu wasio na tumaini, watu wasiotahiriwa (rej. Efe. 2:11-13).

Yesu aliyetangazwa kuwa mleta amani duniani kote, ndiye aliyeyaunganisha matabaka haya mawili. Ujumbe wa malaika kwamba duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia unafanyiwa tafakari nzuri na Mtume Paulo katika waraka wake kwa Waefeso anapoandika, “Lakini sasa, katika Kristo Yesu, ninyi mliokuwa mbali hapo kwanza mmekuwa karibu kwa damu yake Kristo. Kwa maana yeye ndiye amani yetu, aliyetufanya sisi sote tuliokuwa wawili kuwa mmoja; akakibomoa kiambaza cha kati kilichotutenga. Naye akiisha kuondoa ule uadui kwa mwili wake; ndiyo sheria ya amri zilizo katika maagizo; ili afanye hao wawili kuwa mtu mpya mmoja ndani ya nafsi yake, akafanya amani” (Efe. 2:13-15).

2. Salaam na matashi mema ya Noeli.

Ndugu wana wa Familia ya Mungu, kwa niaba ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, nawatakia maadhimisho mema ya kumbukumbu ya ujio wa kwanza wa Yesu Kristo, Mkombozi wa ulimwengu. Sisi viongozi wenu wa dini, hali kadhalika viongozi wetu wa serikali na kwa namna ya pekee Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dr. John Pombe Joseph Magufuli, viongozi wa vyama vya siasa, kwa pamoja wakati huu wa maadhimisho ya sherehe za Noeli, tunakumbushwa na tunaalikwa tena kuwa wakala wa matendo ya amani nambari moja, na hata tuweze kuwaambukiza uwakala huo kwa wale tunaowasimamia na kuwaongoza, ili amani itawale katika nchi yetu na pengine ulimwenguni. Huo ni wajibu mkubwa sana unaodai sala zenu ninyi waamini na wananchi wote kwa ajili yetu sisi viongozi wenu. Amani ianze kutawala katika moyo wa kila mmoja wetu, itawale kati ya wawili, watatu na, hatimaye kwa jamii kubwa ikiwamo Taifa letu la Tanzania.

Hitimisho

Yesu Kristo mwenyewe, Mungu-aliyefanyika-mtu, awabariki sana nyote; awajalieni pia furaha tele katika ahadi yake ya kuwa wale watakaokuwa wapenda amani na wapatanishi, na wale watakaowasaidia wenzao katika uhitaji, hao wanasubirishiwa kwa mapokezi makuu katika utakatifu na utukufu wa milele mbinguni. Kwa hiyo, kuipokea amani ya Kristo na kuitendea kazi haki, kunafaa na ni muhimu kwa ajili ya kuwa na muda mtakatifu na maisha matakatifu katika ulimwengu wa sasa na ujao.

Neema na amani ya kuzaliwa kwake Kristo Bwana wetu iwe nanyi daima, na Mwaka Mpya 2018 wenye baraka na mafanikio tele. Amina.

Askofu John Chrisostom Ndimbo,

Askofu wa Jimbo Katoliki Mbinga.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.