Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Tafakari \ Tafakari ya Neno la Mungu

Sherehe ya Familia Takatifu: Leleni watoto wenu katika upendo na utu!

Familia ni Kanisa dogo la nyumbani ni shule ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kidugu! - ANSA

28/12/2017 14:34

Mpendwa msikilizaji wa Vatican News!, Tukiwa katika Oktava ya Sherehe ya Noeli, Mama Kanisa anatualika kusherehekea sikukuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Kanisa linatuwekea mbele yetu mfano wa familia hii ya Nazarethi kama taswira ya familia bora ambayo kwayo tunachota hazina kubwa kwa ajili ya kuziimarisha familia zetu. Leo tunaalikwa kuziombea familia zote ulimwenguni ili ziweze kujimithilisha na Familia takatifu ya Nazarethi na kwa namna hiyo kuimarisha tunu ya familia, kuinua umoja wa kidugu na kuuhifadhi udugu.

Masomo ya Sikukuu hii yanatupatia sifa muhimu za familia ambazo kwazo ni ukombozi kwa mwanadamu. Tunaziona wazi wazi haki za kila mwanafamilia na kwa upande wa pili tunauona wajibu wa kila mwanafamilia. Watoto wanapewa wajibu wa kuwatii na kuwatunza wazazi wao. Hili ni tendo la shukrani ni kujikusanyia baraka kutoka kwa Mungu. Kuwasaidia na kuwatunza wazazi kunawafanya waingie katika uzee wao wakiwa na hali ya furaha. Kwa upande mwingine Wazazi wanaonywa kutokuwaudhi watoto na kuwakatisha tamaa. Maonyo na maelekezo muhimu na ya lazima yanuie katika kujenga. Ni kituko kwa mzazi kunuia kumkomoa mtoto wake. Kwa wazazi inapendekezwa kuwa utii na kupendana kati yao. Anayependa atatii na anayetii atapenda. Hivyo angalizo la kitume la Mtume Paulo linawataka wote kujivika fadhila za utii na upendo.

Kwa nafasi ya Mwaka huu ninawaalika tutafakari Malezi ya watoto wetu na umuhimu wake kwa ajili ya uadilifu wa jamii nzima. Tutaongozwa na nukuu toka Injili ya leo isemayo: “Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu, amejaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake”. Nimesukumwa kulifafanua wazo hili kutokana na changamoto zinazoonekana katika jamii yetu ya leo. Mmomonyoko wa maadili katika jamii yetu ya leo ni dalili tosha kwamba kuna mushkeri katika sekta ya malezi. Malezi ya tangu utotoni yanamjengea mmoja dhamiri safi ambayo itamuongoza katika utakatifu. Lakini mmoja anapokosa malezi mema kwake inakuwa ni mfereji wa kumtiririshia katika dimbwi la maovu.

Uovu wa kijamii mamboleo unachotwa kutoka chanzo chake cha mfumo unaobarikiwa na jamii husika. Dhamira ya kijamii kwa ujumla inakosa ladha ya Mungu kiasi ambacho hata namna zetu za kimalezi zinavutwa na kuelekezwa katika mrengo huo. Watoto wetu wanakuwa na kuongezeka kimo na hekima lakini si katika Mungu bali katika ulimwengu huu. Katika muktadha huu wa kiulimwengu ni vigumu sana mmoja kukua katika dhamiri njema. Hatuwezi kuvuna zabibu kutoka katika mchongoma. Leo hii tunawalea watoto wetu katika namna ya kubembeleza zaidi kuliko makanyo. Mtoto anapokosea haoneshwi uchungu na ubaya wa kosa lake. Leo hii mtoto anapokanywa na mzazi wake anadiriki kujibizana naye na mzazi wake anaona ni sawa tu. Hapa kuna kitu kimepotea.

Wanasaikolojia na hata wanataalimungu wengi wanakubaliana na mtindo wa malezi ya kukanya na kulazimisha kwa watoto. Hii haimaanishi kuwanyima uhuru wao na kuondoa hadhi yao, bali ni njia ya kuwapeleka katika kujenga dhamiri komavu zinazojengeka katika ukweli. Akili na uelewa wa mtoto anapokuwa mdogo unahitaji kuongozwa kuelekea ukomavu. Tusijidanganye kwa kudhani kwamba malezi ya peremende na keki ndiyo yanaonesha upendo wa dhati kwa mtoto. Upendo wa kweli ni katika kuwaambia na kuwaelekeza katika njia ya ukweli. Wahenga wanatuambia kwamba “mtoto umleavyo ndivyo akuavyo”. Tukimlea katika ukweli atakuwa mkweli lakini tukimlea katika uwongo naye pia atakuwa mwongo kimaadili na matokeo yake ni anguko kwa jamii nzima.

Malezi mema ya watoto yanaonekana kwa nafasi ya kwanza pale tunapo waunganisha na Mungu. “Zilipotimia siku za kutakasika kwao, kama ilivyo torati ya Musa, walikwenda naye hata Yerusalemu, wamweke kwa Bwana”. Kuunganisha maisha ya mtoto na mwenyezi Mungu ni kumuunganisha na ukweli. Bila Mungu kila mmoja anatembea katika njia yake na kujifanya kuwa Bwana wa yote. Matokeo yake ni mgawanyiko wa kijamii. Kila mmoja kujiona yu mtawala katika ufalme wake aliojijengea. Yosefu na Maria wanadhihirisha jinsi walivyo karibu na Mungu na wanamrithisha mtoto wao kwa kufanya kilicho desturi kwao. Hawakutenda kama wajisingiziavyo wazazi wengi wa leo wakisema “mwache akue ataamua mwenyewe afanye nini juu ya imani yake”. Huu ni upotofu mkubwa na tunawakosea haki watoto wetu. Tunaoujasiri wa kuwafundisha na kuwaelekeza taratibu za kidunia lakini mambo yamuhusuyo Mungu tunasingizia kwamba wajiamulie wenyewe.

Kwa nafasi ya pili malezi mema yanaonekana katika mahusiano ndani ya familia. Mtume Paulo anaonesha katika somo la pili fadhila muhimu zinazopaswa kutamalaki ndani ya familia. Mtume Paulo anasema: “jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama Bwana alivyowasamehe Ninyi, vivyo na Ninyi”. Baba na mama wanapodumu katika fadhila hizo wanakuwa ni kioo na kielelezo kwa maisha mema ya mtoto wao. Watoto hujifunza kwa haraka kupitia matendo ya wazazi. Ni vigumu kumfunza mtoto upendo, huruma au msamaha ili hali ninyi wazazi mnaishi katika hali ya magomvi, kutukanana na kununiana kila wakati. Hapa tunawapatia huzuni na hata kupoteza ladha na maana ya maisha ya familia. Tunasababisha anguko la ubinadamu wetu.

Tunapoiua familia tunauua utu wa mtu. Familia ya mwanadamu inasalia kuwa ni taasisi pekee na ya muhimu ya kujifunza tunu za utu. Tunaweza kujidanganya kujifunza mambo haya katika vitabu na taasisi nyingine kama shule lakini tukabakia zaidi katika nadharia. Ndani ya familia tunajifunza upendo wa kindugu na upendo wa kujitoa kwa ajili ya wengine kimatendo zaidi. Watoto ndani ya familia wanajifunza tunu ya usawa na hivyo kujaliana. Hakuna ambaye anakuwa bora kuliko mwenzake. Wote wanapokea upendo sawa kutoka kwa wazazi wao. Wazazi nao wanatufundisha upendo wa kujitoa kwa ajili ya wengine. Ni upendo usiojibakisha, upendo ambao unanuia kumpatia auheni mwingine. Huu ni upendo unaweza kumithilishwa na upendo wa Kristo, aliyetoa nafsi yake kuwa kifidio kwa dhambi zetu.

Malezi mema kwa watoto wetu ni ukombozi wa mwanadamu. Tuzifananishe familia zetu na Familia Takatifu ya Nazarethi ili kwa njia ya malezi yetu watoto wetu “waendelee kukua, kuongezeka nguvu, kujaa hekima, na neema ya Mungu iwe juu yao”. Tukumbuke kwamba “samaki mkunje angali mbichi” kwani akikomaa atavunjiaka. Nawatakieni nyote sikuku njema ya familia zetu.

Mimi Padre Joseph Peter Mosha, Vatican News!

28/12/2017 14:34