Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Vatican \ Hotuba

Mbinu mkakati wa uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda makini!

Waamini wanapaswa kushikamana na Kristo Yesu katika sala na huduma kama kielelezo cha ushuhuda wa imani tendaji! - L'Osservatore Romano

28/12/2017 07:51

Familia ya Mungu nchini Ufilippini inaendelea kujikita katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa imani tendaji, wenye mvuto na mashiko katika maisha ya watu kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu ni chachu ya maisha mapya ndani ya Kanisa. Huu ni muda muafaka wa kukazia mambo msingi katika maisha na imani kwa Kristo na Kanisa lake. Ni mwaliko kwa waamini kujishikamanisha na Kristo Yesu anayeganga na kumwokoa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti na hivyo kumkirimia fursa ya kuwa ni mwana mteule wa Mungu.

Haya ni kati ya mambo yaliyopewa uzito wa pekee hivi karibuni na Askofu mkuu Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji mpya, wakati wa kongamano la kitaifa kuhusu Uinjilishaji mpya nchini Ufilippini, tukio ambalo limehudhuriwa na umati mkubwa wa familia ya Mungu nchini Ufilippini, lakini wengi wao walikuwa ni vijana wanaojengewa matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Amekazia umoja na mshikamano kati ya watu wa familia ya Mungu nchini Ufilippini kama nyenzo msingi katika mchakato wa ushuhuda wenye mvuto na mashiko katika utekelezaji wa ari na mwamko wa maisha na utume wa kimissionari ndani na nje ya Ufilippini.

Kuwa wakristo katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia ni kazi pevu, kwani inahitaji: umoja na mshikamano wa dhati dhidi ya utandawazi usiojali wala kuguswa na mahitaji ya jirani, kama anavyo kaza kusema Baba Mtakatifu Francisko. Kongamano hili ka kimisionari limehudhuriwa pia na Kardinali Luis Antonio Tagle, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis pamoja na Askofu mkuu Bernardito Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, ambaye kwa asili ni mzaliwa wa Ufilippini.

Askofu mkuu Rino Fisichella amekazia umoja na mshikamano katika maisha ya sala, ili kupata nguvu ya kuweza kutoka kifua mbele ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayosimikwa katika imani kwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Umoja na mshikamano umwilishwe katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kama kielelezo makini cha Kanisa linalojali na kuguswa na mahangaiko ya watu wa Mungu, kielelezo makini cha uinjilishaji mpya. Jumuiya ya Kikristo inapaswa kuwa ni chemchemi ya furaha, imani, matumaini na mapendo yanayosambazwa kwa jirani zao kwa njia ya ushuhuda! Sala na huduma ya upendo ni nguzo muhimu katika mchakato wa uinjilishaji mpya.

Wakristo kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo wanashiriki: Ukuhani, Ufalme na Unabii wa Kristo unaopaswa kushuhudiwa katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji, vinginevyo, Kanisa linaweza kutumbukia katika kishawishi cha kujitafuta lenyewe. Wakristo wanapaswa kujisikia kweli kuwa ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo Yesu, yaani Kanisa. Kanisa linatumwa kutangaza Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo, chemchemi ya maisha mapya yanayofumbatwa katika matumaini. Ushuhuda wa imani anasema Askofu mkuu Rino Fisichella, hauna budi kumwilishwa katika umoja, upendo na mshikamano wa dhati. Ni ushuhuda unaofumbatwa katika Neno na Sakramenti za Kanisa hususan Sakramenti ya Ekaristi Takatifu inayowakirimia waamini upendo wa Mungu, ili waweze kuwa tayari kujisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Sakramenti ya Upatanisho inawaonjesha waamini huruma na msamaha unaobubujika kutoka katika kiti cha huruma ya Mungu. Ikumbukwe kwamba, maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa yanawazamisha waamini katika maisha ya Kimungu na hivyo kuimarisha uhusiano wao na Kristo Yesu.

Uwajibikaji wa pamoja ni muhimu sana katika mwendelezo wa mchakato wa uinjilishaji mpya unaotangaza na kushuhudia Injili ya upendo na mshikamano; haki na amani; ili kuweza kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi  ya maadui wakuu wa binadamu yaani: umaskini, ujinga na maradhi sehemu mbali mbali za dunia; mambo yanayofisha utu na heshima ya binadamu. Wakristo wawe ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini kwa wale waliokata tamaa, kama kieleleo cha ukatekumeni mpya katika maisha ya Kikristo. Injili ya upendo iwawezeshe waamini kutambua mifumo mipya ya umaskini inayodhalilisha utu na heshima ya binadamu.

Familia ya Mungu nchini Ufilippini ishikamane kwa dhati katika kutangaza na kushuhudia Furaha ya Injili ya Kristo kwa watu wa Mataifa; kwa kushiriki kwa ari na moyo mkuu katika mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu duniani; Ufalme unaosimikwa katika haki, amani, ukweli na upatanisho. Huu ni ufalme unaowaunganisha na kuwashirikisha watu wote, bila kumtenga awaye yote! Wakristo wawe ni mashuhuda na vyombo vya uinjilishaji mpya katika medani mbali mbali za maisha. Watambue kwamba, Kristo Yesu na Ufalme wa Mungu ni hazina iliyofichika, wanayopaswa kuitafuta kwa udi na uvumba, ili waweze kuipata kwani ndiyo chemchemi ya furaha yao ya maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

28/12/2017 07:51