2017-12-28 07:31:00

Jengeni utamaduni wa kusikiliza kwa makini, ili mtende kwa haki!


Baba Mtakatifu Francisko katika mchakato wa mawasiliano yake na watu mbali mbali duniani anapenda kutumia lugha ambayo ni nyepesi kuweza kueleweka na watu wengi zaidi, licha ya tofauti zao za kitamaduni, makundi ya kijamii na mahali wanapotoka watu hawa au hata wakati mwingine dini, imani na mifumo yao ya kiitikadi. Anapenda kutumia lugha ya watu wa kawaida katika kuwasiliana, hali inayojenga daraja la watu kutana kumsikiliza kwa makini! Maneno kama: tafadhali, asante na samahani; au tafadhali nikumbukeni na kunisindikiza katika maisha na utume wangu kwa njia ya sala ni maneno ya kawaida yanayoonesha unyenyekevu wa hali ya juu kabisa kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko. Lakini haya ni maneno ambayo pia yanatumika ndani ya familia, maeneo ya kazi na katika mawasiliano kati ya watu mbali mbali!

Hii ni lugha ambayo Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuitumia hata pale anapokuwa anatoa mafundisho mazito ya imani kuhusu: huruma na upendo wa Mungu Baba ambaye kamwe hachoki kusamehe na kusahau; Yesu anavyowapenda waja wake kwa upendo ule usiokuwa na mawaa wala makunyanzi; ni mwingi w ahuruma na mapendo, daima yuko tayari kuwasubiri wale wote wanaomwendea kwa moyo wa toba na majuto, ili kuwaonjesha huruma na upendo wake unaofumbatwa katika Sakramenti ya Upatanisho. Papa Francisko anapenda kumwonesha Bikira Maria kuwa ni Mama wa Mungu na Kanisa; Mama mpendelevu, mwema na msikivu, daima yuko tayari kuwasilikiza watoto wake wanaokimbilia tunza na ulinzi wake wa kimama.

Maneno ya Baba Mtakatifu ni kiungo kinachowaunganisha wengi na hakuna anayetengwa na kubaguliwa na huruma wala upendo wa Mungu! Waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanapaswa kutambua kwamba, wanapendwa na kuthaminiwa na Kristo Yesu, licha ya dhambi na udhaifu wao wa kibinadamu. Baba Mtakatifu licha ya kuzungumza na makundi makubwa ya watu, lakini zaidi ushuhuda wa maisha na utume wake kwa kujisadaka kwa ajili pamoja na maskini, umekuwa na mvuto wa hali ya juu kutoka kwa watu sehemu mbali mbali za dunia, wanaotamani kukutana na kuzungumza naye katika safari ya maisha yao!

Hii ni hotuba elekezi iliyotolewa hivi karibuni na Monsinyo Dario Eduardo Vigano’, Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Mawasiliano mjini Vatican katika semina iliyoandaliwa na Taasisi ya Sophia kutoka Loppiano kwa kushirikiana na Mtandao wa rasilimali watu Barani Ulaya kwa kuongozwa na kauli mbiu “Dhana ya kusikiliza katika mchakato wa mawasiliano ya Kanisa la Papa Francisko”. Anasema, Baba Mtakatifu Francisko ni kiongozi anayependa majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kuheshimiana na kuthaminiana na kusikilizana ili kujenga jukwaa la watu kukutana.

Majadiliano kadiri ya Papa Francisko ni jukwaa la upendo ambalo licha ya tofauti zinazoweza kuwepo, lakini linasaidia kuweka msingi wa kutafuta: maendeleo, ustawi na mafao ya wengi na kwamba, majadiliano ni zawadi ya Mungu kwa binadamu! Watu kweli wanapaswa kushikamana na kutembea kwa pamoja, huku wakisaidiana kwa hali na mali, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Familia ya Mungu haina budi kujenga utamaduni wa kusikiliza kwa dhati kilio cha maskini, wakimbizi na wahamiaji, watoto yatima na wale wote wanaonyanyaswa na kudhulumiwa haki zao msingi, tayari kuwajibu kwa wema, upendo na ukarimu. Kusikiliza kwa makini ni kuachana na tabia ya ubinafsi unaoendelea kuwatubukiza walimwengu wengi katika majanga ya maisha!

Kusikiliza ni kuguswa na mahitaji msingi ya jirani zako anasema Monsinyo Dario Eduardo Vigano’. Athari za mtikisiko wa uchumi kitaifa na kimataifa ni matunda ya dhambi ya asili inayojikita katika ubinafsi, uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka kwa kusahau upendo na mshikamano; utu na heshima ya binadamu anayepaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika sera na mikakati ya uchumi na maendeleo endelevu! Kumbe, umefika wakati kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kwa kuheshimu na kudumisha utu wa binadamu na mahitaji yake msingi sanjari na kuondokana na mambo yote yanayopelekea uvunjwaji wa haki msingi za binadamu.

Baba Mtakatifu kwa namna ya pekee kabisa, anawataka viongozi wa Kanisa kujenga utamaduni wa kuwasikiliza watu wa Mungu waliodhaminishwa kwao na Mama Kanisa. Umefika wakati wa kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikiliza na kusikilizana kwa makini; kama anavyofanya Mwenyezi Mungu pale ambapo waamini wanamkimbilia kwa moyo wa sala. Watu wajifunze kusikiliza huku wakiwa wamefumba midomo yao kwani haiwezekani kusikiliza vyema wakati unazungumza. Mwenyezi Mungu ni mfano bora wa kuigwa katika kusikiliza na kujibu mahitaji ya watu wake kwa wakati muafaka.

Ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano kati ya watu, kuna haja ya kudumisha utamduni wa kusikiliza; unapokosekana kinzani, mipasuko na migogoro ya kijamii itaendelea kuwaka moto sehemu mbali mbali za dunia. Utamaduni wa kusikiliza unasaidia kujenga mfumo mpya wa kufikiri, kuamua na kutenda unaowapambanua wanafunzi na mwalimu wao, ambaye kimsingi ni Kristo Yesu. Kumbe, anasema Monsinyo Dario Eduardo Vigano’ kuna haja ya kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikiliza na kusikilizana kwa makini, ili kusaidia mchakato wa maboresho ya mahusiano ya watu katika jamii, kwa kujikita na kuambata Heri za Mlimani, mafundisho makuu ya Kristo Yesu kwa wafuasi wake, kiini cha maisha, mchakato wa watu kukutana, kusikilizana na kushirikishana! Ili kufanikisha azma hii, kuna haja pia ya kuwa na mwelekeo wa kijumuiya, mahali pa kumwilisha na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili katika uhalisia wa maisha ya watu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.