2017-12-28 13:49:00

Askofu mkuu Justin Welby: Onesheni ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji


Waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa kujenga na kudumisha utamaduni wa upendo, huduma na mshikamano na wakimbizi pamoja na wahamiaji wanaolazimika kuzikimbia nchi zao ili kutafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi, licha ya changamoto na vikwazo mbali mbali vinavyoendelea kujitokeza kati ya Watu wa Mataifa! Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu, walilazimika kukimbilia uhamishoni Misri ili kuokoa maisha ya Mtoto Yesu yaliyokuwa hatarini. Hata leo hii, bado kuna mamilioni ya watu wanaolazimika kuzikimbia nchi zao ili kutafuta uhuru, ustawi na maendeleo endelevu yanayogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili!

Hii ni sehemu ya ujumbe wa Noeli kwa Mwaka 2017 kutoka kwa Askofu mkuu Justin Welby, Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikani duniani. Anasema, Mwaka 2017 unaoyoyoma kwa kasi, umeshuhudia ukatili mkubwa wa baadhi ya viongozi wa kisiasa, uliowatumbukiza wananchi wao katika mateso, majanga makubwa ya maisha kutokana na kutafuta umaarufu usiokuwa na tija wala mashiko! Kuna baadhi ya viongozi waliopewa dhamana ya wananchi wamegeuka kuwa ni wezi na mafisadi wakubwa wa mali ya umma, kiasi cha kusahau ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Ni mwaka ambao umesheheni matukio mbali mbali ya kigaidi ambayo yameendelea kupandikiza mbegu ya kifo, chuki na uhasama kati ya watu! Vyama vya upinzani vimeendelea kupandikiza sera na siasa za hofu dhidi ya wananchi wao. Vitendo vyote hivi vinakwenda kinyume cha utu na heshima ya binadamu. Askofu mkuu Justin Welby anawataka waamini kujenga hofu ya Mungu kwa kuwaheshimu na kuwajali jirani zao, ambao wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Upendo kwa Mungu na jirani ni changamoto inayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia kwa kuondokana na hofu, woga na maamuzi mbele.

Huu ndio mwelekeo sahihi unaoletwa na Kristo Yesu, Mwanga wa Mataifa; ufunuo wa uso na huruma ya Mungu kwa binadamu. Wakristo pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanapaswa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya  mwanga wa Mtoto Yesu, aliyezaliwa Bethlehemu kwa maneno, lakini hasa kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kielelezo makini cha uinjilishaji mpya. Katika maisha ya Bikira Maria, Mama wa Mungu, waamini wanakutana na mwanga katika mapito yao, Injili ya uhai, kwani amekuwa ni Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili na upendo unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya binadamu wote.

Askofu mkuu Justin Welby, Kiongozi mkuu wa Kanisa Anglikani duniani anakaza kusema, Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu anawakirimia walimwengu uhuru wa kweli unaofumbatwa katika upendo unaong’aa katika maisha ya mwanadamu. Waamini kwa namna ya pekee wanahamasishwa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya uhai, uhuru wa kweli na upendo usiokuwa na mipaka kwani wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kukombolewa kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.