Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Katekesi siku ya Jumatano

Papa Francisko afafanua maana ya Sherehe ya Noeli katika maisha!

Papa Francisko afafanua maana, historia na umuhimu wa Sherehe ya Noeli katika maisha ya binadamu! - AP

27/12/2017 13:33

Maana ya Sherehe ya Noeli, yaani kuzaliwa kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwenguni, kumejionesha kwa namna ya pekee, katika Liturujia iliyopambwa kwa tafakari ya kina ya Neno la Mungu na nyimbo ambazo zimewawezesha waamini kuishi imani yao katika Fumbo la Umwilisho, kiasi cha kujisikia kwamba leo katika mji wa Daudi amezaliwa, kwa ajili yenu, Mwokozi, ndiye Kristo Bwana. Baba Mtakatifu Francisko katika katekesi yake ya kufunga Mwaka 2017, Jumatano tarehe 27 Desemba 2017 amejikita zaidi katika  Sherehe ya Noeli, akifafanua maana na umuhimu wake katika historia nzima ya maisha ya mwanadamu.

Baba Mtakatifu anasema, inasikitisha hasa Barani Ulaya, kuona maana ya Noeli inatoweka katika jamii kwa kisingizio cha heshima kwa waamini wa dini nyingine! Lakini hiki ni kisingizio cha kutaka kusukumizia imani pembezoni mwa maisha ya kijamii, kwa kuondoa rejea ya kuzaliwa kwa Kristo Yesu katika Sherehe za Noeli. Anakaza kusema, Fumbo la Umwilisho ndilo tukio muhimu sana katika Sherehe ya Noeli, kwani hakuna Noeli bila Kristo Yesu, kwani Yeye ndiye kiini cha sherehe zote hizi zinazopambwa kwa mwanga, muziki, nyimbo, tamaduni na mahanjumati ya watu mahalia. Ikiwa kama Kristo Yesu ataondolewa kwenye Sherehe ya Noeli, mwanga utazimika na mambo yote yanakuwa ni ubatili mtupu!

Kwa njia ya mbiu inayotangzwa na Kanisa, hata waamini leo hii kama ilivyokuwa kwa wachungaji wanaosimuliwa kwenye Injili, wanaongozwa kwenye kuutafuta Mwanga wa kweli ambao ni Kristo Yesu, aliyefanyika mwili na kujifunua katika hali ya kushangaza sana: akazaliwa na Bikira Maria, msichana aliyekuwa hafahamiki sana, lakini akabahatika kuleta Mwanga wa Mataifa na kuulaza katika Pango la kulishia wanyama; kwa msaada wa mchumba wake, Mtakatifu Yosefu! Ulimwengu hakuwa na habari kuhusu tukio hili kubwa katika historia ya mwanadamu, lakini Malaika mbinguni walikuwa wanaimba Utukufu kwa Mungu Juu Mbinguni na Amani Duniani.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, hivi ndivyo Mwana wa Mungu anavyojidhihirisha hata leo hii kati ya Watu wa Mataifa, kama zawadi kwa binadamu aliyezama katika giza na ndoto nzito. Hata leo hii, bado binadamu anapendelea giza badala ya mwanga kwa kuogopa kwamba, matendo yake ya giza yataanikwa hadharani na hatimaye, kushuta dhamiri yake. Ndiyo maana, binadamu anataka kuendelea kukaa gizani badala ya kuongoka na kubadili matendo yake mabaya. Kristo Yesu kwa njia ya maisha yake amewafundisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema jinsi ya kupokea zawadi ya Mungu katika maisha yao, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa wale wote wanaokutana nao katika hija ya maisha yao ya kila siku.

Hii ndiyo maana, anasema Baba Mtakatifu katika Sherehe ya Noeli, watu wanapeana zawadi na kwamba, zawadi kubwa kwa Wakristo ni Kristo Yesu, ili kwa njia ya mfano wake, hata waamini waweze pia kuwa ni zawadi kwa ajili ya jirani zao! Mtakatifu Paulo katika Waraka wake kwa Tito anasema, “Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia, tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa” . Neema na Uso wa Mungu vimefunuliwa kwa njia ya Kristo Yesu, aliyezaliwa na Bikira Maria kama mtoto mwingine yeyote, lakini huyu ni “Mtoto aliyetoka mbinguni” kwa Mwenyezi Mungu. Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho wa Neno wa Mungu, Mwenyezi Mungu amemfungulia mwanadamu njia ya maisha mapya inayofumbatwa katika upendo na wala si katika ubinafsi!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, katika Sherehe ya Noeli, historia ya maisha ya mwanadamu inaweza kuonekana; historia ambayo imeandikwa na wakuu wa dunia hii, inatembelewa kwa namna ya pekee na historia ya Mungu inayowashirikisha wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hawa wanakuwa ni walengwa wa kwanza wa kupokea wokovu unaoletwa na Kristo Yesu ambaye anapenda pia kujenga mahusiano ya pekee na watu wadogo, wanyenyekevu wa moyo na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Huu ni urafiki endelevu unaoboreshwa na matumaini kwa kesho iliyo bora zaidi.

Watu hawa wana wakilishwa na wachungaji, waliobahatika kuona Mwanga mkuu uliowaongoza moja kwa moja kwenda kumwona Mtoto Yesu. Hawa ndio watu ambao kwa nyakati mbali mbali, Mwenyezi Mungu anataka kujenga nao ulimwengu mpya, usiokuwa na ubaguzi, nyanyaso na umaskini. Hii ni changamoto kubwa kwa waamini wakati huu wa Kipindi cha Noeli kufungua akili na nyoyo zao ili kupokea neema. Kristo Yesu ni zawadi ya Mwenyezi Mungu kwa binadamu, ikiwa kama wataipokea kwa moyo wa shukrani, ili hatimaye, hata wao waweze kuwa ni zawadi kwa jirani zao, na hasa zaidi kwa watu wasio onewa huruma na ambao wana puuzwa. Kwa njia hii, Mtoto Yesu ataendelea kuzaliwa katika maisha ya kila mmoja wao na kwa njia yao ataendelea kuwa ni zawadi ya wokovu kwa wanyonge na wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 

 

27/12/2017 13:33