Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Tafakari \ Makala

Katekisimu ya Kanisa Katoliki ni chombo cha imani na Uinjilishaji mpya

Katekisimu ya Kanisa Katoliki ni muhtasari wa: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha ya adili na Maisha ya sala; ni chombo madhubuti cha kufundishia imani na maadili! - AFP

27/12/2017 07:53

Katekisimu ya Kanisa Katoliki ni amana, urithi na utajiri wa imani; matunda ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican na chombo cha kusaidia mchakato wa ukuaji na ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, chachu ya utakatifu wa maisha yenye mvuto na mashiko katika azma nzima ya uinjilishaji. Katekisimu ambayo ni muhtasari wa Imani ya Kanisa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, Kanisa na Mambo ya nyakati. Ni muhtasari wa adhimisho la Fumbo la Pasaka katika Sakramenti za Kanisa, Sakramenti za Kristo, Sakramenti za wokovu, imani na uzima wa milele. Lengo ni kumtukuza Mwenyezi Mungu na mwanadamu kutakatifuzwa.

Katekisimu ni muhtasari wa dira na mwongozo wa Maisha ya Kikristo unaofumbatwa katika Amri kumi za Mungu zinazopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha: kwa kuonesha upendo kwa Mungu na jirani, kama mhutasari wa Mafundisho makuu ya Kristo Yesu. Katekisimu ni muhtasari wa Maisha ya Sala kama ilivyokuwa kwenye Agano la Kale na Sala kuu ya Baba Yetu kama ilivyofundishwa na Kristo Yesu kwa kubeba mafundisho mazito katika maisha na utume wake. Hii ni kazi iliyovaliwa njuga na Mtakatifu Yohane Paulo II kama chombo muhimu sana cha maisha na utume wa Kanisa katika kukabiliana na changamoto mamboleo.

Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Uinjilishaji Mpya katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 ya Katekisimu ya Kanisa Katoliki anakaza kusema, hii ni kazi ya Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa, inayowawezesha waamini kusoma alama za nyakati, ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo. Katekisimu hii imekwisha kutafsiriwa katika lugha mbali mbali duniani, ikiwemo pia na lugha ya Kiswahili, iliyochapishwa kunako mwaka 2000.  Katekisimu ya Kanisa Katoliki inafumbata utajiri mkubwa wa: Maandiko Matakatifu, Mababa wa Kanisa, Mafundisho ya Mitaguso Mikuu, Mchango na mafundisho ya waalimu wa Kanisa, Watakatifu na viongozi wa Kanisa. Katekisimu iliidhinishwa rasmi kwa Waraka wa Papa Yohane II “ Fidei depositum” yaani “Amana ya Imani” uliosindikiza kuchapishwa kwa Katekisimu ya Kanisa Katoliki, hapo tarehe 11 Oktoba 1992 na kuanza kutumika rasmi kama kitabu cha kufundishia: imani na maadili ya Kanisa Katoliki tarehe 15 Agosti 1997. 

Kardinali Christoph Schonborn, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Vienna, Austria, anasema jambo ambalo linapewa kipaumbele cha kwanza katika Katekisimu ya Kanisa Katoliki ni umoja wa imani unaobubujika kutoka katika Ubatizo unaofafanuliwa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, changamoto na mwaliko kwa familia ya Mungu kujenga umoja, udugu na mshikamano katika kukiri, kuungama na kushuhudia imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Mama Kanisa kama anavyosema Mtakatifu Ireneus wa Lion. Licha ya tamaduni, lugha ya mapokeo ya watu mbali mbali, lakini Kanisa limekazia imani moja katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, chemchemi ya kazi ya ukombozi.

Kardinali Christoph Schonborn anawahimiza waamini kulinda, kutangaza na kushuhudia imani yao kwa njia ya matendo yenye mvuto na mashiko! Ujana wa imani, unaliwezesha Kanisa kuendelea kujipyaisha na kuwa kijana daima. Imani ni moja, lakini inaweza kumwilishwa kadiri ya mazingira ya watu kama zilivyo pia Injili pacha, au mchango wa Mababa wa Kanisa katika Mafundisho tanzu ya Kanisa! Utawakuta akina Toma wa Akwino na Mtakatifu Bonaventura, wakielezea imani yao kwa Kristo na Kanisa lake kadiri ya mazingira yao. Umoja katika imani ndicho kigezo msingi ambacho kilitumiwa kuandika Katekisimu ya Kanisa Katoliki kama amana ya imani; mafundisho ya Kanisa katika imani na maadili.

Kardinali Christoph Schonborn anakaza kusema, Katekisimu ya Kanisa Katoliki ilihakikiwa na mabingwa pamoja na wataalam wa Sayansi ya Maandiko Matakatifu, kiasi kwamba ni Hati ambayo imetengezwa vyema kama kitabu cha kufundishia imani na maadili. Mwongozo kuhusu ufafanuzi wa Maandiko Matakatifu unafuata ule ulioelekezwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, “Dei Verbum” yaani “Ufunuo”: Mwenyezi Mungu katika Maandiko Matakatifu ameongea kwa njia ya wanadamu na kwa mtindo wa kibinadamu, lakini yanapaswa kusomwa na kufafanuliwa kwa msaada wa Roho Mtakatifu.Katekisimu ya Kanisa Katoliki inarutubishwa kwa Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya Kanisa. Kardinali Christoph Schonborn anaendelea kufafanua kwamba, kuna haja pia ya kuzingatia mchango uliotolewa na watakatifu wanaolipamba Kanisa, kwa ushuhuda wa maneno yao, kama kielelezo cha ushuhuda wa imani tendaji, imani ambayo imemwilishwa katika matendo.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Cesare Nosiglia, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Torino, Italia anasema mchakato wa uinjilishaji na katekesi ni sawa na Chanda na pete, ni mambo yanayokamilishana. Ni nyenzo zinazomsaidia mwamini kufungua hazina ya moyo wake ili kumfahamu na kumtumikia Mwenyezi Mungu aliyefunuliwa kwa njia ya Kristo Yesu. Katekesimu ni mchango wa Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, kama sehemu ya mchakato wa kupyaisha maisha na utume wa Kanisa. Katekisimu ni chombo makini cha uinjilishaji na ufundishaji wa kweli za kiinjili na kiimadili; kwa kuendelea kuwa aminifu  na chombo cha neema ya Mungu. Mama Kanisa amekabidhiwa dhamana na wajibu wa kuwarithisha watu amana na utajiri wa imani na maadili na kwamba, Roho Mtakatifu ni kiini cha Uinjilishaji. Katika kumbu kumbu ya Jubilei ya Miaka 25 ya Katekisimu ya Kanisa Katoliki, Baba Mtakatifu Francisko ameandika utangulizi katika Toleo la Mwaka 2017 linalotoa pia ufafanuzi wa kitaalimungu , kwa kila kifungu cha Katekisimu ya Kanisa Katoliki, utajiri mkubwa katika imani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

27/12/2017 07:53