Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Tafakari \ Makala

Caritas Africa mintarafu asili ya Kanisa na huduma endelevu!

Caritas Africa inapenda kujielekeza katika mchakato wa huduma makini na endelevu kama asili na utambulisho wa Kanisa kati ya Watu wa Mataifa. - AFP

27/12/2017 07:32

Kanisa katika ulimwengu mamboleo na  maendeleo ya sayansi na teknolojia linapaswa kuwa ni shuhuda na chombo cha huruma na upendo wa Mungu unaomwilishwa katika  matendo ya huruma kiroho na kimwili. Haya ni mambo msingi katika mchakato mzima wa uinjilishaji mpya na wa kina Barani Afrika, unaojikita katika huduma makini: kiroho na kimwili kama ushuhuda wa maisha na kielelezo cha imani tendaji.

Askofu mkuu Martin Musonde Kivuva wa Jimbo kuu la Mombasa na Mwenyekiti wa Caritas Kenya katika mahojiano maalum na Radio Vatican, "Vatican News" huko Dakar, Senegal, amefafanua mchakato wa huduma ya Caritas Africa unavyopania kuifanya kuwa kweli ni chombo cha upendo na huduma ya maendeleo endelevu ya binadamu, kielelezo makini cha ushuhuda wa maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika. Upendo wa Mungu ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa na kwamba, upendo wa kibinadamu unapata utimilifu wake katika upendo wa kimungu unaogusa, unaoganga na kuponya mahangaiko ya binadamu kwa mafuta ya huruma na divai ya matumaini. Kanisa linapenda kukazia huduma ya upendo inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha na utume wake na kwamba, upendo wa Kimungu unalikamilisha na kuliwezesha Kanisa Barani Afrika kusimama kwa miguu yake katika huduma.

Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa Barani Afrika, Caritas Africa, kuanzia tarehe 18 - 21 Septemba, 2017 imeadhimisha mkutano wake mkuu huko Dakar, Senegal kwa kuongozwa na kauli mbiu “Kuratibu huduma ya upendo Barani Afrika: Wajibu wa Maaskofu”. Waraka wa “Huduma ya upendo” uliochapishwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI na Waraka wa “Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu uliochapishwa na Baba Mtakatifu Francisko zimekuwa ni nyaraka elekezi katika mkutano wa Caritas Africa mintarafu mwanga wa Injili na Mafundisho Jamii ya Kanisa.

Caritas Africa, katika Tamko la Dakar Senegal, 2017, inapania kujifunga kibwebwe katika mchakato wa maboresho ya utawala bora mintarafu huduma za kijamii, kwa kujiwekea sera makini na kuwatumia watu waliobobea katika huduma. Caritas Africa inapania pia kuweka Mafundisho Jamii ya Kanisa; misingi ya ukweli na uwazi katika kuratibu na matumizi ya rasilimali ya Kanisa kwa ajili ya huduma ya maskini kuwa ni sehemu ya malezi Seminarini na kwenye nyumba za kitawa. Caritas Africa inataka kuratibu kikamilifu huduma yake kwa Bara la Afrika kwa kushirikiana na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Majimbo katika ujumla wake ili kujenga umoja wa Kikanisa na huduma ya maendeleo endelevu ya binadamu; kuimarisha umoja na mshikamano na wadau mbali mbali wa maendeleo ili kujenga utamaduni wa amani na maendeleo ya kweli yanayofumbatwa katika utambulisho wa Kanisa Katoliki kwamba, huduma ya upendo ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa kwa watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

27/12/2017 07:32