2017-12-27 13:49:00

Baba Mtakatifu Francisko amtembelea Papa mstaafu Benedikto XVI


Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumwomba, Kristo Yesu, aliyezaliwa kwa ajili yao, awasaidie kuwa na imani kwa Mwenyezi Mungu na upendo kwa jirani; mwelekeo unaogeuza maisha na kuwa ni mazuri zaidi, kiasi cha kuzaa matunda! Bikira Maria, Mama wa Mkombozi na Malkia wa Mashahidi, awasaidie kumpokea Yesu kama Bwana wa maisha yao, ili hatimaye, waweze kuwa ni mashuhuda wake jasiri, tayari kujisadaka kwa ajili ya uaminifu kwa Injili na huduma makini kwa jirani zao, lakini hasa kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Kipindi cha Noeli ni muda wa sala, kwa Kristo Mfalme wa Amani, ili aweze kuwakirimia amani idumuyo! Baba Mtakatifu anakaza kusema, Fumbo la Umwilisho lipate nafasi katika maisha ya kila mwamini, ili kweli moyo wa kila mwamini, uweze kugeuka kuwa ni Pango ambamo, Mtoto Yesu anazaliwa, ili kuwapelekea Watu wa Mataifa, amani na upendo wake usiokuwa na mipaka kwa watu wa nyakati hizi. Waamini wawe ni vyombo vya furaha na upendo kwa jirani zao kwa kutakiana heri na baraka kwa Sherehe ya Noeli, kwani wanatambua kwamba, Immanueli, yaani Mungu yu pamoja nao! Baba Mtakatifu katika maadhimisho ya Sherehe za Noeli na Mwaka Mpya 2018 alimtembelea Papa Mstaafu Benedikto XVI, kwenye makazi yake yaliyoko kwenye Monasteri ya “Mater Ecclesiae” iliyoko mjini Vatican. Mazungumzo yao yamedumu takribani nusu saa, kadiri ya taarifa zilizotolewa na Msemaji mkuu wa Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.