2017-12-26 14:53:00

Patriaki Cyrill wa Moscow asema: zawadi kubwa ya Noeli ni moyo wako!


Ni jambo la kawaida kusikia mateso na mahangaiko ya watu kutokana na vita, ghasia, kinzani, majanga asilia pamoja na vitendo vya kigaidi. Pamoja na nguvu zote za giza, lakini upendo unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu bado ni mkubwa kwa walimwengu wote. Hii ni sehemu ya ujumbe wa Noeli kutoka kwa Patriaki Cyrill wa Kanisa la Kiorthodox la Moscow na Russia nzima katika maadhimisho ya Noeli kwa Mwaka 2017. Anasema, upendo wa binadamu, tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kifamilia zinaendelea kudumishwa licha ya changamoto nyingi ambazo mwanadamu anakumbana nazo katika ulimwengu mamboleo. Hii inatokana na ukweli kwamba, imani kwa Mwenyezi Mungu ni kiini cha vinasaba vya maisha ya binadamu. Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, kumekuwepo na dhuluma kubwa dhidi ya Kristo na Kanisa lake. Wimbi la ukanimungu linaendelea kuongezeka kila kukicha pamoja na watu kukengeuka. Lakini, Kanisa linaendelea kubaki ni mahali ambapo familia ya Mungu inaweza kukutana na Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu.

Fumbo la Umwilisho ni tukio ambalo limeleta mageuzi makubwa katika historia ya maisha ya binadamu, kwa kuwawezesha watu waliokuwa na kiu kukutana na Mwenyezi Mungu kwa njia ya Neno wa Mungu, Mwana wa Baba wa milele aliyefanyika mwili na kukaa kati ya watu! Kristo Yesu ni Nafsi ya Pili ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, ni Mungu kweli na Mtu kweli, aliyezaliwa bila kuumbwa, mwenye Umungu sawa na Baba! Amezaliwa hapa duniani, ili aweze kuwa ni daraja ya huruma, upendo na neema ya Mungu kwa binadamu, ili hatimaye, kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti sanjari na kuweka msingi wa amani ya kweli inayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Patriaki Cyrill anaendelea kudadavua ujumbe wa Noeli kwa kusema kwamba, Mamajusi kutoka Mashariki ya mbali, walimletea Mtoto Yesu zawadi muhimu sana kama sehemu ya utambulisho wake: manemane, uvumba na dhahabu. Leo hii, Wakristo wanapaswa kujiuliza swali la msingi, Je, wanampelekea zawadi gani Mtoto Yesu kutoka katika undani wa maisha yao kama utambulisho wao? Zawadi kubwa ambayo waamini wanaweza kumtolea Mwana wa Mungu aliyezaliwa ni moyo wao, yaani sadaka ya maisha yao bila kujibakiza hata kidogo; kwa kujiweka wakfu kwa ajili ya Mungu na huduma makini kwa jirani.

Lengo ni kuhakikisha kwamba, waamini wanaondoa makwazo yote yaliyomo ndani mwao, ili kutoa nafasi kwa Mwenyezi Mungu kutawala maisha yao na hatimaye, kuondokana na ubinafsi ambao umekuwa ni chanzo cha majanga makubwa katika maisha ya binadamu wa nyakati zote. Ni fursa ya kuwashirikisha wengine huruma na upendo unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwa kuwajali na kuwahudumia, kwani wote hawa wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kukombolewa na Kristo Yesu aliyezaliwa mjini Bethelehemu. Ni changamoto kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kutambua na kuthamini uwepo wa Mungu katika maisha yao, tayari kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo.

Patriaki Cyrill wa Moscow na Russia nzima anasema, Mwaka 2017, Russia imeaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 ya Mapinduzi ya Oktoba 1917, ambayo yalipelekea majanga makubwa katika historia ya wananchi wa Russia; huo ukawa ni mwanzo wa dhuluma na nyanyaso za kidini! Lakini ni kipindi ambacho pia Kanisa limebahatika kupata mashuhuda wa imani, waliosadaka maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, wakaandika historia ya Kanisa kwa njia ya damu yao. Mwenyezi Mungu akawafunulia wanadamu hazina ya huruma na upendo wake na huo ukawa ni mwanzo wa kuchipua tena kwa Upatriaki wa Moscow na Russia nzima. Tangu wakati huo, Kanisa likabahatika kupata: viongozi waliokuwa na ari na mwamko wa kichungaji; wenye ujasiri, hekima na busara; wachamungu na watakatifu. Kwa njia hii, familia ya Mungu nchini Russia, ikaweza kuvuka kipindi kigumu katika historia, maisha na utume wake. Patriaki Cyrill wa Moscow na Russia nzima anahitimisha ujumbe wake wa Noeli kwa Mwaka 2017 kwa kuwatakia waamini na watu wote wenye mapenzi mema heri na baraka kwa mwaka 2018, uwe ni mwaka wa amani na maendeleo endelevu ya binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.