2017-12-26 13:59:00

Papa Francisko: Mt. Stefano, shahidi aliyeungana na Kristo Yesu!


Baada ya maadhimisho ya Sherehe ya Noeli, Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 26 Desemba, anaadhimisha Siku kuu ya kuzaliwa kwa Mtakatifu Stefano, Shahidi wa kwanza mbinguni, Siku kuu ambayo ina uhusiano wa pekee kabisa na Sherehe ya Noeli. Katika Liturujia ya Sherehe ya Noeli, Mwinjili Yohane anatangaza kwamba, “Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu”. Stefano, Shahidi aliwachanganya sana wakuu wa watu wake kwani alikuwa wamesheheni imani na Roho Mtakatifu; alikuwa na imani thabiti kiasi cha kuungama uwepo mpya wa Mungu kati ya watu wake. Alifahamu fika kwamba, Hekalu la Mungu alikuwa ni Kristo Yesu, Neno wa Mungu aliyekuja kukaa kati ya watu wake na kujifanya kuwa sawa na binadamu katika mambo yote isipokuwa hakutenda dhambi.

Stefano Shahidi, alishutumiwa kwa kuhubiri kuhusu kubomolewa kwa Hekalu la Yerusalemu na kusema kwamba, wao wenyewe wamemsikia kwa masikio yao akisema huyo Yesu Mnazareti atapaharibu mahali hapa, na kuzibadili desturi walizopewa na Musa. Hii ni tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumanne, tarehe 26 Desemba 2017 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, maadhimisho ya Kumbu kumbu ya kifodini cha Mtakatifu Stefano Shahidi. Kwa hakika, ujumbe wa Kristo Yesu haukuwafurahisha viongozi wa kidini waliokuwa wamegubikwa na malimwengu, kiasi hata cha kusuta dhamiri zao.

Ujio wa Kristo Yesu, ulikuwa ni changamoto ya kufanya toba; kubadilisha mitazamo kwa kuacha kufikiri na kutenda kwa mazoea kama ilivyokuwa hapo awali. Stefano, Shahidi alijishikamanisha na ujumbe wa Yesu tangu mwanzo hadi kifo chake. Mwishoni mwa maisha yake alisali akisema, “Bwana Yesu pokea roho yangu”, akapiga magoti akalia kwa sauti kuu “Bwana, usiwahesabie dhambi hii”, akiisha kusema haya akakata roho. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufafanua kwamba, huu ni mwangwi  wa uaminifu unaobubujika kutoka katika maneno yaliyotamkwa na Kristo Yesu alipokuwa pale juu ya Msalaba “Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu” na “Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo”. Maneno ya Stefano, Shahidi yameweza kutamkwa kwa vile Mwana wa Mungu amezaliwa, akateswa, akafa na kufufuka kwa ajili ya binadamu. Kabla ya matukio haya, maneno haya yasingaliwezekana kutamkwa!

Mtakatifu Stefano, Shahidi anamwomba Kristo Yesu aweze kuipokea roho yake. Kristo Yesu aliyefufuka kwa wafu ni Bwana na  Mwombezi pekee kati ya Mungu na binadamu, si tu wakati ambapo mwanadamu anakabiliana na kifo bali katika mzunguko mzima wa maisha, kwani bila Yesu, mwanadamu hawezi kutenda lolote. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kusali mbele ya Pango la Mtoto Yesu kwa kusema: “Bwana Yesu, naiweka roho yangu mikononi mwako, ipokee” kwa sababu maisha ya binadamu ni mazuri ikiwa kama yataambatana na  Injili. Yesu ni mwombezi na mpatanishi kati ya Mungu na binadamu; ni chemchemi ya upendo, anayewawezesha watu kujenga umoja na ndugu zao kwa kuondokana na kinzani, chuki na kinyongo. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumwomba, Kristo Yesu, aliyezaliwa kwa ajili yao, awasaidie kuwa na imani kwa Mwenyezi Mungu na upendo kwa jirani; mwelekeo unaogeuza maisha na kuwa ni mazuri zaidi, kiasi cha kuzaa matunda! Bikira Maria, Mama wa Mkombozi na Malkia wa Mashahidi, awasaidie kumpokea Yesu kama Bwana wa maisha yao, ili hatimaye, waweze kuwa ni mashuhuda wake jasiri, tayari kujisadaka kwa ajili ya uaminifu kwa Injili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.