2017-12-25 11:51:00

Papa Francisko: Ujumbe wa Noeli: Sikilizeni kilio cha watoto wadogo!


Kristo Yesu amezaliwa na Bikira Maria mjini Bethlehemu si kwa utashi wa binadamu bali kama zawadi ya upendo wa Mungu Baba aliyeupenda ulimwengu, hata akamtuma Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Hili ndilo tukio linalorudiwa tena na Mama Kanisa anayesafiri katika nyakati, kwani imani ya Wakristo inapyaishwa tena katika Liturujia ya Noeli, yaani, kwenye Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu anapotwaa ubinadamu na kujifanya kuwa mdogo na maskini, ili aweze kumkomboa mwanadamu. Tukio hili linashangaza sana kwani linaonesha huruma ya Mungu Baba Mwenyezi.

Hii ni sehemu ya ujumbe wa Noeli kwa Mwaka 2017 uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 25 Desemba 2017 kwa ajili ya mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, maarufu kama “Urbi et Orbi”. Baada ya Bikira Maria na Yosefu kuuona utukufu wa Mwokovu Yesu, walifuatia wachungaji waliokuwa wanalisha mifugo yao kondeni, mjini Bethlehemu, wakamtambua kwa alama walizoambiwa na Malaika na hatimaye, wakamwabudu. Wachungaji hawa walikuwa ni watu wanyenyekevu na waliokuwa wanakesha, mfano na kielelezo cha waamini wa nyakati zote mintarafu Fumbo la Umwilisho wa Kristo Yesu, kwani hawakukwazwa na umaskini wake, bali kama Bikira Maria, waliamini Neno la Mungu na kutafakari utukufu wake kwa macho ya kawaida. Mbele ya Fumbo la Mwilisho, Wakristo kutoka sehemu mbali mbali za dunia kwa kutumia maneno ya Mwinjili Yohane wanaungama kwamba, “Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba, amejaa neema na kweli”. Yoh. 1:14.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake wa Noeli anakaza kusema, vita bado inaendelea kupamba moto duniani, licha ya maendeleo makubwa yaliyofikiwa na binadamu, hali ambayo inaendelea kuhatarisha maisha ya binadamu, jamii pamoja na uharibifu wa mazingira. Sherehe ya Noeli ni mwaliko kwa familia ya Mungu kutambua Uso wa Mtoto Yesu miongoni mwa watoto mbali mbali duniani, lakini hasa wale ambao hawana nafasi katika jamii mamboleo kama ilivyokuwa kwa Mtoto Yesu.

Baba Mtakatifu anaendelea kuwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumwona Mtoto Yesu kati ya watoto waliko huko Mashariki ya kati wanaoendelea kuteseka kutoka na kinzani kati ya Israeli na Palestina. Siku kuu ya Noeli ni fursa makini ya kuombea amani Yerusalemu na Nchi Takatifu katika ujumla wake, ili kukuza na kudumisha majadiliano yatakayodumisha amani na utulivu kati ya mataifa haya mawili kwa kutambua mipaka yake waliyojiwekea na kutambuliwa rasmi kimataifa! Papa Francisko anawaombea pia viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wenye mapenzi mema wanaopania kusaidia maridhiano, haki na usalama licha vikwazo mbali mbali vinavyojitokeza.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumwona Mtoto Yesu katika nyuso za watoto wa Siria ambao wameathirika sana na vita iliyotimua vumbi nchini humo katika miaka ya hivi karibuni. Hatimaye, sasa iwe ni nafasi kwa Siria kuweza kusimama kidete kulinda utu wa binadamu, kwa kujenga mafungamano ya kijamii dhidi ya udini na ukabila usiokuwa na mavuto wala mashiko! Uso wa Mtoto Yesu, uonekane miongoni mwa watoto wa Iraq ambao wamejeruhiwa sana kutokana na uhasama uliojitokeza nchini humo katika kipindi cha miaka kumi na moja iliyopita! Sura ya Yesu ionekane miongoni mwa watoto wa Yemen ambako vita bado inaendelea kufuka moshi, lakini inaonekana kusahaliwa, hali ambayo ina madhara makubwa kwa wananchi wa Yemen ambao wanateseka kwa baa la njaa na magonjwa ya mlipuko!

Baba Mtakatifu Francisko anaialika familia ya Mungu kumwona Mtoto Yesu kati ya Watoto wa Bara la Afrika, hasa wale wanaoteseka huko Sudan ya Kusini, Somalia, Burundi, DRC, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati na Nigeria. Ni changamoto ya kumwona Mtoto Yesu kati ya watoto wote sehemu mbali mbali za dunia ambako hakuna amani na usalama; watoto ambao wanatishiwa na kinzani na machafuko mapya. Baba Mtakatifu anaiombea Korea ili iweze kupita changamoto inazokabiliana nazo ili hatimaye, iweze kukuza imani kwa ajili ya mafao ya dunia nzima. Anapenda kuwaaminisha wananchi wa Venezuela chini ya ulinzi na tunza ya Mtoto Yesu, ili aweze kuwasaidia kurejea tena kwenye majadiliano kwa ajili ya mafao ya familia ya Mungu nchini Venezuela. Watu wamwone Mtoto Yesu kati ya watoto na familia zao, wanaolazimika kukimbia kutoka Ukraine, ili Mwenyezi Mungu aweze kuwakirimia amani wananchi hawa!

Baba Mtakatifu anawaalika Watu wa Mataifa kumwona Mtoto Yesu kati ya watoto ambao wazazi na walezi wao hawana ajira kiasi cha kuteseka ili kuhakikisha kwamba, watoto wao wanapata usalama na utulivu; bila kuwasahau watoto ambao wamepokwa utoto wao kwa kulazimishwa kufanya kazi za suluba tangu wakiwa wadogo au kupelekwa  mstari wa mbele kama chambo vitani na watu ambao wamekengeuka na kufilisika kiutu! Papa Francisko anaitaka familia ya Mungu kumwona Mtoto Yesu kati ya watoto wanaolazimika kuzikimbia nchi zao katika mazingira magumu na hatarishi, kiasi cha kujikuta wahanga wa wafanyabiashara haramu ya binadamu. Machoni pao, Watu wa Mataifa waone na kuguswa na mahangaiko ya wakimbizi wanaolazimika kuzihama nchi zao hata kwa kuthubutu kuhatarisha maisha ili kuanzisha safari ambazo mara nyingi sana zinawatumbukiza kwenye maafa.

Baba Mtakatifu anawaona watoto wa Myanmar na Bangaladesh ambako ametembelea hivi karibuni wakati wa hija yake ya kitume. Ni matumaini yake kwamba, Jumuiya ya Kimataifa itaendelea kusimama kidete kulinda na kudumisha utu na heshima ya watu wote, hasa makundi madogo madogo yaliyomo kwenye nchi hizi. Kristo Yesu anatambua vyema uchungu wa kutokupokelewa na kukosa mahali pa kuweza kulaza kichwa! Hii ni changamoto kwa familia ya Mungu kutofunga nyoyo kama ilivyokuwa kwenye nyumba za Bethlehemu. Baba Mtakatifu Francisko, mwishoni mwa ujumbe wake wa “Urbi et Orbi” anawaalika waamini kumpokea Mtoto Yesu aliyevikwa nguo za kitoto kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria, Mtakatifu Yosefu na wachungaji mjini Bethelehemu. Wajitahidi kumpokea Mtoto Yesu, upendo wa Mungu uliomwilishwa; wajikite katika neema yake, ili kuuwezesha ulimwengu kuwa na utu na stahiki kwa watoto wa leo na wale wa kesho!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.