Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Mahubiri

Papa Francisko: hudumieni wakimbizi na maskini wa nyakati hizi!

Matumaini makubwa ya kuzaliwa kwa Mtoto Yesu ni kiini cha ujumbe wa Mkesha wa Noeli, Fumbo la kuzaliwa kwa Kristo Yesu, Mwana wa Baba wa milele. - REUTERS

25/12/2017 11:30

Wakati ulipotimia, Bikira Maria alijifungua mtoto wake na kumlaza katika Pango la kulishia wanyama, kwa sababu walikosa nafasi kwenye nyumba ya wageni. Mtoto Yesu aliyezaliwa ni Mwanga wa Mataifa ambaye ujio wake umeleta mabadiliko makubwa katika historia ya mwanadamu na kwamba, sasa amekuwa ni chemchemi ya matumaini. Bikira Maria pamoja na Mtakatifu Yosefu walilazimika kuwaacha watu wa nyumba na makazi yao, ili kwenda kuhesabiwa, licha ya matatizo na changamoto zote zilizokuwa mbele yao, lakini ndani mwao walikuwa na matumaini makubwa kutokana na mimba ya mtoto wao. Hiki ndicho kiini cha ujumbe wa Mkesha wa Noeli!

Walishangazwa sana walipofika mjini Bethlehemu na kukuta kwamba, watu wa mahali hapa hawakuwa wamejiandaa kumpokea na hivyo hawakuwa na nafasi kwa ajili yao! Hapa wakakumbana na changamoto, lakini Bikira Maria akaikabili na hatimaye, akajifungua, Mtoto mwanaume, Immanueli, yaani Mungu pamoja nasi! Alikuja kati ya watu wake, lakini, walio wake hawakumpokea hata kidogo! Lakini hata katika mazingira kama haya, Mtoto Yesu akapata nafasi na huo ukawa ni mwanzo wa mageuzi makubwa yaliyoletwa na Mwenyezi Mungu. Bethlehemu ukatengeneza nafasi kidogo, kwa wale wote waliokuwa wamepoteza ardhi, makwao, ndoto na hata kwa wale wote waliokata tamaa kutokana na watu kujifungia katika ubinafsi wao!

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Ibada ya Misa Takatifu, Mkesha wa Noeli, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 24 Desemba, 2017. Katika nyayo za Maria na Yosefu, hata leo hii ulimwenguni kuna familia mbali mbali zinazolazimika kuhama nchi zao ili kutafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Ni familia zinazopambana na changamoto mbali mbali za maisha, lakini daima zikiwa na cheche za matumaini kwa kesho iliyo bora zaidi, ni watu wanaotafuta hifadhi ya maisha dhidi ya akina Mfalme Herode katili, wanaotaka kujitajirisha hata kama ni kumwaga damu ya watu wasiokuwa na hatia.

Bikira Maria na Yosefu hawakupata nafasi na wao wakawa watu wa kwanza kumkumbatia Neno wa Mungu anayewapatia watu wote hati ya utambulisho wa uraia. Mtoto Yesu katika umaskini na udogo wake anatangaza na kushuhudia kwamba, mamlaka ya kweli yanafumbatwa kwa namna ya pekee na wale wanao waheshimu na kuwasaidia maskini na wanyonge katika maisha. Habari Njema ya kuzaliwa kwa Mwokozi Yesu, ilitangazwa na Malaika kwa wachungaji waliokuwa wanachunga mifugo yao kondeni.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, hawa ni watu waliokuwa wanaishi pembezoni mwa jamii kutokana na hali yao pamoja na mazingira ya kazi zao. Hawa ni watu ambao hawakuweza kupata fursa ya kujitakasa mintarafu kanuni, sheria na taratibu za dini yao, hivyo ni watu waliotambulikana kuwa ni wachafu, kiasi kwamba, hawakuweza kujificha hata kidogo! Hawa ni watu waliopaswa kutengwa na kuogopwa na jamii; walikuwa ni wapagani kati ya waamini; walihesabiwa kuwa ni wadhambi kati ya wenye haki; “watu wa kuja” kati ya raia wema! Hawa wapagani, wenye dhambi na wageni, ndio waliotangaziwa na Malaika Habari Njema ya kuzaliwa kwa Mwokozi, Kristo Yesu. Hiki ndicho kiini cha furaha ya Mkesha wa Noeli, ambayo waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, wanahamasishwa kuwashirikisha jirani zao, kuisherehekea na kuitangaza.

Hii ni furaha ambayo Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo ameweza kuwakumbatia wapagani, wadhambi na wageni, changamoto kwa watu wote kuwakaribisha watu kama hawa! Baba Mtakatifu anakaza kusema, imani katika Mkesha wa Noeli, inawasukuma waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumtambua Mwenyezi Mungu anayejifunua katika hali na mazingira ambamo si rahisi sana kutambua uwepo wake. Huyu ni Mwenyezi Mungu anayetembea katika barabara za miji mbali mbali, ni mgeni ambaye si rahisi sana kuonekana ingawa yuko katika hali na mazingira mbali mbali.

Imani ya Mkesha wa Noeli, inawasukuma waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kutoa sura mpya ya kijamii kwa kujenga na kudumisha mahusiano mapya na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, watu ambao wanajisikia kwamba, hawana nafasi katika ulimwengu mamboleo. Noeli ni muda muafaka wa kufanya mageuzi kutoka kwenye nguvu ya woga usiokuwa na mvuto wala mashiko na kuwa ni nguvu ya upendo inayotoa mwelekeo mpya wa upendo unaomwilishwa katika jamii. Huu ni upendo unaosimikwa katika ujasiri kati ya kinzani na mipasuko ya kijamii, ili kuugeuza na kuwa ni “Mji wa Mkate, nchi yenye ukarimu. Mtakatifu Yohane Paulo II anawakumbusha waamini kutokuwa na woga bali wamfungulie Kristo malango ya maisha yao!

Kwa njia ya Kristo Yesu, aliyezaliwa, Mwenyezi Mungu anawajia watu wake na kuwapatia uwezo wa kuwa ni wadau katika mapambano ya maisha yanayowazunguka. Anajitoa ili aweze kuinuliwa na kukumbatiwa miongoni mwa wageni, maskini, walio uchi, wagonjwa pamoja na wafungwa. Mwenyezi Mungu anawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni chemchemi ya matumaini kwa watu waliokata tamaa kutokana na baadhi ya watu kuwafungia malango katika maisha yao. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, kwa njia ya Mtoto Yesu, Mwenyezi Mungu anawawezesha waamini kuwa wadau wa ukarimu kwa jirani zao. Kilio cha Mtoto Yesu, kiamshe dhamiri za watu ambazo haziguswi tena na mahangaiko ya wengine, ili kufungua macho na kuwaona wale wote wanaoteseka! Huruma na upendo wake, uwasukume watu kuwatambua na kuwathamini watu wote wanaobisha hodi katika malango ya miji mbali mbali duniani; watu wanaoingia katika historia na maisha yao, ili hatimaye, kuwa kweli ni chemchemi ya matumaini, huruma na mapendo kwa watu wote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

25/12/2017 11:30