2017-12-23 08:49:00

Ujumbe wa Noeli kwa Mwaka 2017 kutoka kwa Askofu mkuu Muheria, Kenya


Wakati uliopangwa na Mwenyezi Mungu, Mwana wa pekee wa Baba, Neno wa milele, yaani Neno la sura yenye uwamo mmoja wa Baba alifanyika mwili, akachukua asili ya binadamu, bila kupoteza asili ya Kimungu. Kristo Yesu ni Mungu kweli na Mtu kweli katika umoja wa nafsi yake ya Kimungu, kwa sababu hiyo ndiye peke yake mpatanishi kati ya Mungu na watu! Ni asili na chemchemi ya umoja, upendo, mshikamano na udugu. Kristo Yesu ana asili mbili, ya Kimungu na ya Kibinadamu, zisizochanganywa, bali zinazoungana katika Nafsi ya Mwana wa Mungu. Kristo Yesu akiwa Mungu kweli na mtu kweli ana akili ma utashi wa kibinadamu katika ulinganifu kamili chini ya akili na utashi wake wa Kimungu ambao anao katika ushirika na Roho Mtakatifu. Fumbo la Umwilisho kwa hiyo, ni muungano wa ajabu wa asili ya Kimungu na asili ya kibinadamu ndani ya Nafsi moja ya Neno wa Mungu! Hivi ndivyo Kanisa linavyosadiki na kufundisha!

Askofu mkuu Anthony Muheria wa Jimbo kuu la Nyeri, Kenya ambaye pia ni Msimamizi wa Kitume Jimbo Katoliki la Kitui, katika salam zake za matashi mema ya Sherehe ya Noeli kwa Mwaka 2017 anasema, maisha na utume wa Kikristo unaweza kufafanuliwa kwa mwaliko wa kwenda kumtazama Kristo Mfalme wa Amani aliyelazwa kwenye Pango la kulishia wanyama. Ni mwaliko wa kwenda kumwangalia Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, ili kuzungumza na kumwabudu, sanjari na kumtolea maisha yote kama sadaka safi inayopendeza mbele ya Mungu. Mtoto Yesu aliyezaliwa kati ya watu wake, anahitaji kuonjeshwa upendo.

Wachungaji kondeni waliokuwa wa kwanza kuhabarishwa kuhusu kuzaliwa kwa Kristo Yesu Mkombozi wa ulimwengu, walialikwa kwa namna ya pekee kabisa, kufurahi na kwenda mbio ili kutazama zawadi ambayo Mwenyezi Mungu alikuwa amewakirimia binadamu anasema Askofu mkuu Muheria. Hii ni changamoto kwa familia ya Mungu Jimbo kuu la Nyeri na Kenya katika ujumla wake, kuonesha umoja na mshikamano wa upendo, mwaliko wa pekee katika maadhimisho ya Sherehe ya Noeli.

Inawezekana kabisa kwamba, kuna baadhi ya waamini wamefunga malango ya nyumba zao kiasi cha kushindwa kumkaribisha Kristo Yesu kutokana na sababu mbali mbali za maisha, lakini Noeli ni kipindi cha kumfungulia Kristo Yesu, malango ya maisha kama walivyofanya wachungaji mjini Bethlehemu! Waamini waoneshe ujasiri wa kumkaribisha Kristo Yesu anayekuja kwao kwa njia ya: Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na Jirani, kama utekelezaji wa unabii.

Askofu mkuu Anthony Muheria ameitaka familia ya Mungu Jimbo kuu la Nyeri kuenzi na kuunga mkono kazi kubwa zilizotekelezwa na wamisionari wa mashirika ya kitawa na kazi za kitume sehemu mbali mbali za Kenya. Hawa ni mashuhuda na vyombo vya huruma, upendo na huruma ya Mungu, waliosadaka maisha yao kwa ajili ya kupandikiza mbegu ya imani, matumaini na mapendo; mambo yanayopaswa sasa kuanza kutoa matunda yake kwa njia ya umoja, upendo na mshikamano wa dhati kwani leo hii, familia ya Mungu nchini Kenya, imebahatika kuwa na idadi kubwa ya wakleri, watawa na waamini walei, wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafanikio ya familia ya Mungu, Jimbo kuu la Nyeri, nchini Kenya. Jimbo kuu la Nyeri, liko katika mchakato wa kipindi cha mpito, ili kuweza kulipyaisha zaidi kwa kusoma alama za nyakati, tayari kutoa ushuhuda wenye mvuto na mashiko katika maisha na utume wake!

Askofu mkuu Anthony Muheria wa Jimbo kuu la Nyeri, Kenya katika salam zake za Noeli kwa Mwaka 2017 anapenda kuwashuruku wamissionari wote waliojisadaka kwa ajili ya kupandikiza mbegu ya Ukristo nchini Kenya. Kwa namna ya pekee kabisa, anawashukuru Askofu William Dunne na Askofu mkuu Boniface Lele waliosimama kidete kuhakikisha kwamba, wanajenga na kuimarisha msingi wa Jimbo kuu la Nyeri kwa njia kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu! Heri na Baraka kwa Noeli na Mwaka Mpya 2018.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.