2017-12-23 08:29:00

Jifunzeni maisha kutoka katika shule ya Bikira Maria


Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, ambayo kwa sasa baada ya mageuzi makubwa ya vyombo vya mawasiliano ya jamii itajulikana kama “Vatican News” katika tafakari ya Neno la Mungu. Leo tunaadhimisha jumapili ya nne na ya mwisho katika kipindi hiki cha majilio. Ahadi ya kuzaliwa kwetu mkombozi inakaribia na katika maandiko matakatifu siku ya leo Mungu anazidi kuithibitisha ahadi hiyo. Katika somo la kwanza, kutoka kitabu cha pili cha Samweli, Mungu anamwahidia mfalme Daudi kuwa atamjengea nyumba na atamuinua mzao wake kuwa mfalme na kiti cha ufalme wake kitakuwa imara milele. Hii ni ahadi inayomwashiria Kristo. Atajulikana kama mwana wa Daudi na atakirithi kiti cha Ufalme cha Daudi na atauanzisha ufalme ule ambao hautakuwa na mwisho.

Katika somo la Injili, Mungu anathibitisha ahadi zake za kale kwa kumtuma malaika Gabrieli kumpasha Maria habari ya kuzaliwa huyo mkombozi. Maria anaupokea ujumbe wa malaika na kwa njia yake Kristo, Neno wa Mungu anatwaa mwili. Tangu mwanzo wa kipindi cha majilio Kanisa limetuandaa kwa njia ya maandiko matakatifu, mazoezi ya kiroho lakini pia kwa njia ya wahusika mbalimbali - Yohane Mbatizaji, Mt. Yosefu na Mama Bikira Maria. Baada ya kumtafakari Yohana Mbatizaji katika dominika ya pili na ya tatu, leo tunawekewa mbele yetu Mama Bikira Maria, mama aliye na nafasi ya pekee katika historia ya ukombozi na mwenye nafasi ya pekee katika safari ya ukombozi ya kila mmoja wetu. Ndiye ambaye tafakari yetu ya leo itajikita kwake na kuona namna anavyotusaidia kujiandaa kwa matumaini kupokea ukamilifu wa ahadi ya Mungu yaani kumpokea Kristo masiha na mwana wa Daudi.

Bikira Maria alikuwa na nafasi ya pekee katika kumleta duniani Neno wa Mungu, mkombozi wetu Yesu Kristo. Kama wayahudi wengine, yeye naye alikuwa akisubiri kwa hamu ukamilifu wa ahadi ya ujio wa mkombozi masiha. Alisubiri hivyo bila kujua kwamba ni kwa njia yake masiha angekuja duniani. Hivyo alikuwa akiendelea na maisha yake kama watu wengine. Kwa jinsi hiyo alipata mchumba aliyeitwa Yosefu na walifuata taratibu zote za kuishi uchumba kadiri tamaduni za kiyahudi. Katika Injili ya leo tunaona kuwa akiwa katika kipindi hicho cha uchumba, Mungu anamtuma malaika Gabrieli kumpasha habari kuwa mkombozi anayetazamiwa atatwaa mwili ndani yake kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Kwetu sisi tunaosoma maandiko haya wakati huu tunaweza kuona ni kitu rahisi tu na Bikira Maria angeupokea ujumbe huo bila wasiwasi wowote. Ni pale tu tunapojiweka katika nafasi yeke na katika mazingira yake tunagundua si rahisi kiasi hicho. Huu haukuwa ujumbe mdogo na rahisi, si tu katika kuupokea bali hata katika kuuelewa. Na jambo hilo halikuwahi kusikika hata mara moja tangu kuumbwa kwa ulimwengu.

Katika mazungumzo kati ya malaika na Bikira Maria tunaweza kubaini hatua zifuatazo: Neema, Wito, Mashaka na Kujikabidhi. Tunaona  kwanza malaika anamwambia “salamu uliyepewa neema”. Mungu akiisha kumchagua Maria, anajitambulisha kwake kwa kumjalia neema. Baada ya salamu hiyo malaika anamjulisha wito anaoitiwa, wito wa kuwa mama wa mkombozi “tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume na jina lake utamwita Yesu”. Wito huu ulifuatiwa na hatua ngumu upande wa Bikira Maria, hatua ya mashaka, mashaka yaliyochanganyika na hofu na sintofahamu kubwa. Maria akauliza “litakuwaje neno hili?” Katikati ya mashaka haya anajikabidhi kwa Mungu akisema “mimi ni mjakazi wa Bwana na iwe kwangu kama ulivyosema”.

Kwa jibu lake “na iwe kwangu kama ulivyosema” tukampata mkombozi. Mtakatifu Bernard anasema ulimwengu mzima ulisimama kwa muda kusubiri jibu la Maria ili ujue kama utakombolewa au la. Mungu alitaka Umwilisho utanguliwe na ukubali huru wake yeye aliyeteuliwa tangu milele awe Mama.Tofauti na Eva aliyetumia uhuru wake kutotii sauti ya Mungu bustanini Eden, Maria alitumia  uhuru wake kutii. Tofauti na Eva ambaye alikosa kuamini, Maria aliamini. Na tofauti na Eva ambaye kwa njia yake kifo kiliingia ulimwenguni, kwa njia ya Maria uzima umeingia ulimwenguni. Ndiyo maana kwa haki kabisa Maria anaitwa Eva mpya na Mama wa walio hai (Rej. LG 56). Yote haya kwa jibu lake “na iwe kwangu kama ulivyosema”. Kwa njia ya Maria, mwenyezi Mungu ameanzisha awamu mpya katika historia ya ukombozi wa mwanadamu. Ni awamu inayomweka Kristo katikati ya kazi ya ukombozi wa ulimwengu na awamu ambayo yeye mwenyewe anagonga katika moyo wa mwanadamu ili amkomboe na ili amtumie kama chombo cha kuendeleza kazi hiyo ukombozi kwa wengine.

Katika maisha ya kila mwanadamu, tunaweza bado kuziona hatua hizo nne ambazo Mungu anatupitisha ili tuweze kuufikia wokovu wetu na wokovu wa wengine. Kwanza hutujalia Neema; neema kubwa na neema ndogo ndogo. Kati ya neema anazotujalia, kubwa zaidi ni uhai na imani. Lakini pia hutujalia neema za kutuwezesha kupita salama katika hatua mbalimbali za makuzi na maisha kwa ujumla tukimuelekea yeye. Katika hatua ya pili hutujalia wito. Kwa kadiri alivyomuumba kila mtu kwa makusudio maalumu, humjalia wito ili aweze kuyatimiza makusudio hayo na hatimaye arudi kwake kwenye heri ya milele. Ndani ya wito mama, yaani wito wa kuwa watakatifu, Mungu humwita kila mmoja wetu katika hali fulani ya maisha (upadre, utawa, ndoa) na pia katika huduma kwa watu wake. Hatua hizi mbili, neema na wito, mara kwa mara huambatana na nyakati za mashaka, giza na  kutokuelewa ni nini hasa makusudio ya Mungu katika maisha yetu. Bikira Maria anatuonesha kuwa ili kufikia wokovu wetu na wa wengine tunahitaji kuvuka kutoka hatua hii ya mashaka na hatua ya giza katika maisha yetu. Hatua ambayo hatuoni mbele na tunahisi tumepotea au tumepotezwa. Anatufundisha namna ya kuvuka ni kwa kujikabidhi kwa Mungu kwa matumaini yote.

Bikira Maria amejaa neema. Katika maisha yake yote ameshirikiana na neema ya Mungu. Hakuichafua kwa doa la dhambi na kwa njia hii yote ambayo Mungu aliyaanzisha ndani mwake aliyafikisha katika ukamilifu kwa kumpaliza mbinguni na kumvika taji ya umalkia wa mbingu. Anatufundisha nasi kushirikiana na neema anazotujalia Mungu maishani mwetu ili yale anayokusudia Mungu ndani mwetu yatimie na ili kazi anayoianzisha katika maisha yetu aifikishe katika ukamilifu.

Bikira Maria aliupokea wito wake kiuaminifu. Tangu mwanzo aliitwa kuwa Mama wa Mungu. Tangu wakati alipopokea wito huo aliuishi kiaminifu. Baadaye tunaona katika Maandiko Matakatifu alitekeleza wajibu wake wa kimama kwa mwanaye Yesu na katika kuitunza nyumba yake. Katika maisha Mungu aliyotuitia (upadre, utawa, ndoa) na katika huduma mbalimbali kwa watu anazotujalia (uongozi, uuguzi, ualimu, ufundi, biashara, kilimo nk) Bikira Maria anatufundisha uaminifu. Mt. Paulo katika waraka wake wa kwanza kwa wakorinto anakumbusha kuwa “kinachotakiwa kwa mtu aliyekabidhiwa kazi ni kuwa mwaminifu” (1Kor. 4:2) naye Mt. Mama Theresa wa Calcutta alisema daima “Mungu hakutuita tukazanie mafanikio katika maisha bali tuwe waaminifu katika maisha”.

Katika kuupokea wito wake Bikira Maria alipata mashaka. Tumesikia akamuuliza malaika “litawezekanaje jambo hili...? Hakukomea katika mashaka yake, hakupenda kubaki hapo wala yeye mwenyewe kujidai anajua kila kitu na kwa akili yake mwenyewe anaweza kutatua kila kitu. Hata pale ambapo akili yake haikuelewa, alijiaminisha kwa Mungu na kwake akaweka tumaini lake. Mt. Thomas wa Akwino anasema imani huanza pale akili inapokoma. Kwa maana kwamba pale ambapo akili na ufahamu wetu vinashindwa kufumbua mambo tunayopitia au mambo yanayotusibu, basi hapo ndipo imani hupata nafasi ya kudhihirika. Baba wa kanisa, Tertulian alisema “naamini kwa sababu ni upuuzi” akimaanisha kuwa kuna wakati yale mambo tunayopaswa kuyashikilia kwa imani tunapotaka kuyapima kiakili au kwa uzoefu wetu wa kibinadamu huonekana ni ya upuuzi kabisa. Anayetanguliza imani hubaki nayo lakini anayetanguliza akili na uzoefu wake pekee huyapuuzia.

Ni wangapi kati yetu katika mashaka au giza la maisha huishia kupoteza mwelekeo wa neema na wito walioitiwa na Mungu? Wangapi wapatapo misukosuko ya kiimani au kimaisha huishia kuhama dini, hufukuza wenzi wao wa ndoa, hutelekeza familia, huacha maisha ya wakfu na hata wengine kuondoa maisha yao au ya wengine? Tumwone na tujifunze kutoka kwa Mama Maria ambaye alijikabidhi kwa Mungu na ndipo mwanga wa wokovu ulipotokea kwake na kwa ulimwengu mzima. Hii ndiyo shule ya Mama Bikira Maria ambayo kanisa linatupitisha tunapomngojea mkombozi Masiha azaliwe kwetu. Anatufundisha kushirikiana na neema, anatufundisha kupokea wito kwa uaminifu na anatufundisha kujikabishi kwa Mungu katika nyakati za mashaka ili ukombozi anaotuletea Kristo Masiha utufikie, na kwa njia yetu uwafikie wengine.

Tumsifu Yesu Kristo.

Padre William Bahitwa.








All the contents on this site are copyrighted ©.