2017-12-22 11:22:00

Noeli kiwe ni kipindi cha matumaini kwa wananchi wa Sudan ya Kusini


Familia ya Mungu, Sudan ya Kusini inapitia kipindi kigumu sana katika maisha na historia yake. Wananchi wanaendelea kuteseka kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe isiyokuwa na “kichwa wala miguu” kutokana na ukabila, uchu wa mali na madaraka! Kipindi cha Majilio na hatimaye, Sherehe ya Noeli ni kipindi cha matumaini, changamoto kwa wananchi wa Sudan ya Kusini kusitisha vita na kuanza kujipatanisha, tayari kuandika ukurasa mpya wa historia na maisha ya watu yanayofumbatwa katika matumaini ya Sudan ya Kusini mpya.

Hii ni sehemu ya ujumbe wa Noeli kwa mwaka 2017 kutoka kwa viongozi wa Makanisa Sudan ya Kusini kwa ajili ya familia ya Mungu nchini humo! Kuzaliwa kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu, kusaidie kufukuzia mbali giza la dhambi na mauti, ili kuwakirimia watu mwanga wa imani, matumaini na mapendo. Kuanzia mwaka 2013 Sudan ya Kusini ilijikuta inatumbukia tena kwenye vita ya wenyewe kwa wenyewe, lakini Baraza la Makanisa Sudani ya Kusini, limekuwa mstari wa mbele kupandikiza mbegu ya matumaini kwa familia ya Mungu Sudan ya Kusini.

Baraza la Makanisa Sudan ya Kusini katika ujumbe wake wa Noeli linasikitika kusema kwamba, wananchi wanakabiliwa na hali ngumu sana ya maisha kutokana na kuyumba kwa uchumi sanjari na ukosefu wa huduma makini za kijamii. Watu wanaendelea kupoteza maisha kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara. Mpasuko wa Sudan ya Kusini ni matokeo ya ukabila usiokuwa na mashiko wala mguso kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wa Sudan ya Kusini. Kumekuwepo na vitendo vya uvunjifu wa amani, uporaji wa mali za watu pamoja na ubakaji, mambo ambayo kimsingi yana dhalilisha utu na heshima ya binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Inasikitisha kuona kwamba, watu wanajichukulia sheria mikononi mwao! Hakuna tena utawala wa sheria, kwani watu wanakamatwa na kufungwa bila kufuatwa sheria, kanuni na taratibu za nchi! Hapa mambo yanakwenda kombo, wanasema viongozi wa Makanisa Sudan ya Kusini. Wananchi wanaona kwamba, viongozi wana wasaliti, kwani badala ya kusimamia ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wengi wa Sudan ya Kusini, wao wamekuwa wakilumbana kuhusu mafao yao binafsi. Umefika wakati kwa wananchi wa Sudan ya Kusini kuanza mchakato wa haki, amani na upatanisho wa kitaifa. Baraza la Makanisa Sudan ya Kusini linaendelea kufafanua kwamba, liko tayari kuwa ni jukwaa la upatanisho, haki na amani katika ngazi mbali mbali!

Ili kufanikisha mchakato huu, kuna haja kwa familia ya Mungu nchini Sudan ya Kusini kujikita katika mambo makuu manne: kwanza kabisa ni uragibishaji wa amani kwa kuondokana na vita pamoja na uvunjifu wa haki msingi za binadamu. Pili ni kujenga Jukwaa litakalokuwa huru kuanzisha mchakato wa upatanisho kitaifa kwa njia ya majadiliano yanayofumbatwa katika ukweli, uwazi, umoja na mshikamano wa kitaifa! Tatu, kuna haja ya kuanzisha mchakato wa upatanisho utakaosaidia kuganga na kuponya madonda ya vita, chuki na kinzani ambazo zimekuwepo miongoni mwa wananchi wa Sudan ya Kusini. Huu ni mchakato unaohitaji elimu na wongofu wa ndani. Nne ni kuendelea kuimarisha miundo mbinu itakayosaidia kuimarisha misingi ya ukweli na uwazi; kwa watu kufahamiana na kujijengea uwezo wa kusimamia tunu msingi za maisha ya kijamii!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.