2017-12-22 09:14:00

Bikira Maria, kielelezo cha usikivu, utii, imani na matumaini!


Ndugu yangu mpendwa! Antifona ya mwanzo ya Dominika ya nne ya Majilio inalifafanua fumbo zima la la Umwilisho ambalo ni utimilifu wa Ukombozi wa mwanadamu. “Dondokeni, enyi mbingu, toka juu, mawingu na yammwage mwenye haki; nchi ifunuke, na kumtoa mwokozi”. Dominika hii ambayo inatutafakarisha tendo hilo adhimu katika imani yetu inanuia kutukumbusha ujio wa Kristo hapa duniani na kuufanya tena hai uwepo huo na hivyo kuingia katika sherehe za Noeli tukiwa na mioyo iliyo tayari kumpokea Mwokozi. Mkombozi wa wanadamu ni Kristo ambaye ni nafsi ya pili ya Mungu. Yeye anashuka kutoka juu mbinguni na kutujia sisi wanadamu. Uwepo wake unadhihirika kwa kujimithilisha na sisi. Hivyo ni zawadi itokayo juu mbinguni inayoshuka chini mithili ya mvua na kuidhihirisha kazi yake ya ukombozi katikati ya jamii.

Injili ya Dominika hii inatupatia habari ya kupashwa habari Maria juu ya ujio huo. Sifa hizo za mwokozi zinazoelezewa na antifona ya mwanzo ya Dominika hii zinaonekana wazi kabisa. Kwanza inawekwa wazi kwamba huyu Masiha ni kutoka juu na ni Mwana wa Mungu: “Roho Mtakatifu atakujia juu yako, na Nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu”. Huu si mpango wa mwanadamu bali ni mpango wa Mungu. Ni mawingu yanammwaga huyu mwenye haki, hakika ni tendo la upendo wa Mungu kwetu.

Pili nchi inapaswa kufunuka ili kumtoa Mwokozi anayetumwa kwetu. Hili linafunuliwa katika utii wa Mama Maria. Yeye alikuwa tayari na kujibu: “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema”. Kwa utii wake Mama Bikira Maria tunaletewa Mkombozi wa Ulimwengu. Mpango huu wa Mungu wa kumkomboa mwanadamu unahitaji utayari wetu. Mungu anauheshimu uhuru wa mwanadamu. Hivyo hamshurutishi kumpokea Mwokozi bali anamtaka “afunuke na kumtoa Mwokozi” yaani awe tayari kumdhihirisha Mwokozi aliyemwilika ndani mwake.

Sifa hizi mbili ni za muhimu kuelekea katika sherehe ya Noeli. Katika Dominika hii tunakumbushwa kuitambua nafasi ya kwanza ya Mungu katika kazi ya Ukombozi. Yeye ndiye mhandisi wa kazi hiyo. Mfalme Daudi katika somo la kwanza ametaka kumjengea nyumba Mwenyezi Mungu. Ni wazi aliliona hitajiko hilo kwani haikuwa stahili kwa yeye kukaa katika nyumba nzuri na maridadi wakati Mungu ametayarishiwa kibada au hema kuwa makazi yake: “Angalia sasa, mimi ninakaa katika nyumba ya mierezi, bali sanduku la Mungu linakaa ndani ya mapazia”. Lilikuwa ni wazo jema na la kuungwa mkono kwani ukuu Mungu ulijidhihirisha kwa Daudi. Lakini Mungu anamwambia kuwa si Yeye atayefanya kazi hiyo njema bali Mwenyezi Mungu atamuinua mwingine kutoka katika ukoo wake kuijenga nyumba hiyo.

Mwenyezi Mungu anajitambulisha kuwa Yeye ndiye anayejua kipi kilicho chema na cha kufaa na hivyo sisi wanadamu tunaalikwa kukipokea kwa utii. Nathani anamfikishia Daudi mpango wa Mungu anayemwambia: “Je, wewe utanijengea nyumba, nikae ndani yake? Hapa anakumbushwa kwamba mjenzi ni Mungu mwenyewe na anachokianzisha Yeye ndicho kile kinachodumu milele: “Bwana atakujengea nyumba, na nyumba yako, na ufalme wako, vitathibitishwa milele mbele yako. Nacho kiti chako kitafanywa imara milele”. Uaguzi huu ni wa ujio wa Kristo ambaye atamjengea Mungu nyumba ya kweli na yenye kudumu. Ujio wako unamkomboa mwanadamu na dhambi na kuifanya nafsi yake kuwa makao stahiki na yenye kudumu ya mwenyezi Mungu. Yeye ambaye anahesabika katika jamaa ya Daudi ndiye utimilifu wa uaguzi huo unaosema kwamba “nitainua mzao wako nyuma yako, atakayetoka viunoni mwako, nami nitaufanya imara ufalme wake”.

Utii wa Mama Bikira Maria kwetu sisi kwetu sisi ni kielelezo na njia ya kuifuata kusudi Neno hilo la Mungu linalodondoka kutoka mawinguni limchepushe Kristo Mkombozi wetu katikati ya jamii ya mwanadamu. Ni dhahiri kwamba, hali halisi ya kijamii ilimvuta na hivyo kushawishika kuhoji ni vipi mambo hayo yatendeke kwake wakati bado hajamjua mume. Ujumbe wa malaika unapomhakikishia kuwa kazi hiyo si kadiri ya mwanadamu bali ni kadiri ya Mungu anaitikia na kwa utii wake tunampata Mkombozi wa ulimwengu. Ni uthibitisho wa ukuu wa Neno la Mungu ambalo ili kulipokea inahitajika neema ya pekee ndani mwetu. Ili kulipokea Neno hilo mmoja anapaswa kuwaza na kuongozwa na mwangaza kutoka juu.

Kwa maneno mengine ukaribu wetu na Mungu kwa njia ya sala na sakramenti unatuweka katika mazingira stahiki ya kulipokea Neno la Mungu. Malaika Gabrieli anapomtokea Bikira Maria anamtaja kama aliyejaa neema. Hii inamaanisha kuwa ni yeye ambaye anao muunganiko na Mungu. Hakuna anayeweza kuwa katika hali ya neema bila kuwa na ukaribu na Mungu. Neema ni misaada ya kimungu ambayo inatupeleka katika kutenda mema. Misaada hii inatujia pale tunapotoa nafasi na kuwa tayari. Maisha ya Mama yetu Bikira Maria yalijaa fadhila ya kumcha Mungu na ndiyo maana Malaika akaongezea zaidi akisema “Bwana yu pamoja nawe”.

Hapa tunaona hitajiko muhimu kwa ajili ya kukipatia nafasi hichi kinachoshuka kutoka mawinguni kuchipuka katika nchi, yaani ndani ya mioyo yetu na kumtoa Mwokozi. Maandalizi yetu kuelekea Sherehe ya Noeli yatufae kwa kutufanya kuwa karibu na Mungu. Sherehe hii kubwa si ya kutupita kama tukio la kihistoria bali inapaswa kuchipusha na kuufanya tena hai uwepo wa ukombozi wetu ndani ya nafsi zetu. Hivyo pamoja na kuwa na maandalizi yetu ya mahitaji ya kimwili mfano nguo, chakula na kadhalika, tunapaswa kutoa kipao mbele kwa maandalizi ya kiroho. Ndiyo maana tunasisitiziwa kupokea sakramenti ya Kitubio ili kwayo tuweze kundolewa dhambi ya kuwa katika hali ya Neema. Na zaidi ni Sakramenti ya Ekaristi Takatifu ambayo inatuunganisha na Kristo na kuwa Kiongozi wetu kuelekea katika ukombozi. Sherehe ya Noeli imekaribia. Ukombozi wetu unatushukia kutoka juu. Tujiweke tayari ili Yeye anayezaliwa kwa ajili yetu atufanye upya katika nafsi zetu, katika familia zetu na kwa jamii nzima ya mwanadamu. Tuiandaye mioyo yetu ili tuwe ni mahali stahiki pa kumjengea mwenyezi Mungu nyumba ya kudumu.

Mimi ni Padre Joseph Peter Mosha, 

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.