2017-12-21 14:18:00

Mshikamano wa Maaskofu na Wakristo Mashariki ya Kati!


Kardinali Vincent Nichols, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Wales, kwa niaba ya Maaskofu wenzake, amewaandikia barua Wakristo huko Mashariki ya Kati ili kuwaonesha mshikamano wao wa dhati kutokana na Tamko la Rais Donald Trump wa Marekani wa kuhamishia Ubalozi wao kutoka Tel Aviv kwenda mjini Yerusalemu, jambo ambalo limechafua amani, maisha, utu na heshima ya wakazi wa Nchi Takatifu. Yerusalemu ni mji unaoheshimiwa na Wayahudi, Wakristo na Waislam na kwamba, ni mji ambao unatoa makazi kwa wananchi wa nchi mbili tofauti yaani Israeli na Palestina! Haki na amani ni mambo msingi yanayopaswa kuwaongoza pia viongozi wa kisiasa na kiserikali wanapofanya maamuzi magumu katika medani mbali mbali za maisha!

Tamko la Rais Trump la kutambua Yerusalemu kuwa ni Makao Makuu ya Israeli linapingana na Tamko la Umoja wa Mataifa, hali ambayo imesababisha mpasuko, kinzani na machafuko huko Mashariki ya Kati. Ni matumaini ya Maaskofu kwamba, uamuzi wa Benjamin Netanyahu, Waziri mkuu wa Israeli, utaheshimu Makubaliano yaliyofikiwa na Jumuiya ya Kimataifa kwa kuheshimu pia uhuru wa Palestina, sanjari na kuendeleza mchakato wa kudumisha haki, amani na maridhiano miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali huko Mashariki ya Kati.

Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Wales linapenda kuonesha wasi wasi wake mkubwa kutokana na Muswada wa Sheria wa Ardhi inayomilikiwa na Kanisa katika Nchi Takatifu. Muswada huu unatoa mamlaka makubwa kwa Serikali kuweza kutaifisha ardhi inayomilikiwa na Kanisa, jambo ambalo ni kwenda kinyume cha haki msingi na uhuru wa kuabudu kwani kitendo hiki ni sawa na kuishambulia Jumuiya ya waamini ambao kimsingi ndilo Kanisa.

Kardinali Nichols, anapenda kuchukua fursa hii, kuwaalika viongozi wa kidini na kisiasa kutoka sehemu mbali mbali za dunia kuungana na Maaskofu wa Uingereza la Wales kupinga muswada huu unaotishia uhuru wa kuabudu katika Nchi Takatifu. Wanamshukuru kwa namna ya pekee kabisa, Patriaki Theophil III kwa kupaaza sauti yake, ili kuwatetea Wakristo katika Nchi Takatifu. Kipindi cha Noeli, kiwe ni wakati muafaka kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuwakumbuka na kuwaombea Wakristo huko Mashariki ya Kati, katika kipindi hiki kigumu kinachowapambanisha na changamoto za maisha katika maisha na utume wao kama Wakristo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.