2017-12-21 14:50:00

Askofu mkuu Pizzaballa azungumzia utume wa Kanisa na changamoto zake


Askofu mkuu Pierbattista Pizzaballa, Msimamizi wa kitume wa Upatriaki wa Yerusalemu, katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini Yerusalemu, kuhusu ujumbe wake kwa Noeli kwa Mwaka 2017 amegusia maisha na utume wa Kanisa katika Nchi Takatifu sanjari na changamoto zinazolikabili Kanisa kwa wakati huu huko Yerusalemu! Askofu mkuu Pizzaballa anasema, anaendeleza mchakato wa upyaisho wa maisha na utume wa Kanisa huko Yerusalemu hasa katika shughuli za kichungaji kwa kuunda ofisi ya shughuli za kichungaji itakayojikita katika masuala nyeti kama vile: Injili ya familia ili kuhakikisha kwamba, wanandoa watarajiwa wanajiandaa kikamilifu ili hatimaye, kutoa ushuhuda wenye mvuto na mashiko katika kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa!

Ofisi hii itajihusisha na majiundo awali na endelevu kwa ajili ya vijana wa kizazi kipya, ili kulijengea Kanisa uwezo wa kutembea na kuwasindikiza vijana katika mchakato wa elimu na miito mbali mbali ndani ya Kanisa. Askofu mkuu Pizzaballa anasema, anaendelea kufanya hija za kichungaji kwa kutembelea Parokia mbali mbali pamoja na kuwatia moyo mahujaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaotembelea maeneo matakatifu, kama hija ya kuimarisha imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Matukio yote haya ni muhimu sana katika ujenzi wa mshikamano wa upendo miongoni mwa Wakristo. Mahujaji wanakaribishwa kwa mikono miwili kutembelea Nchi Takatifu kwani kuna amani na utulivu wa kutosha. Kumekuwepo na maboresho makubwa ya mahusiano kati ya Makanisa kwa kuchangia hata katika shughuli za ukarabati wa Makanisa Mahalia!

Kuhusu masuala ya kijamii, Askofu mkuu Pizzaballa anaendelea kufafanua kwamba, kumekuwepo na kinzani kati ya Wakristo na Waislam; uhuru wa kuabudu na kwamba, wamepokea kwa masikitiko makubwa Tamko lililotolewa na Rais Donald Trump wa Marekani kuhusu mchakato wa kuhamisha ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv kwenda mjini Yerusalemu na matokeo yake. Kanisa kwa upande wake, litaendelea kuheshimu Tamko la Umoja wa Mataifa kama lilivyofafanuliwa na Baba Mtakatifu Francisko, ili kukuza na kudumisha amani kwa kutambua kwamba, Yerusalemu ni amana ya Jumuiya ya Kimataifa.

Kumbe, msimamo wowote wenye upendeleo wa kisiasa au kidini unaweza kukinzana na mantiki hii. Ni matumaini ya Askofu mkuu  Pizzaballa kwamba, machafuko yaliyojitokeza hivi karibuni mjini Yerusalemu yataweza kupewa ufumbuzi wa kisiasa, kidini na kitamaduni. Katika hali na mazingira kinzani kama haya kuna haja ya kuwa na siasa na sera zenye mwelekeo sahihi unaoheshimu watu mahalia. Machafuko, vurugu na kinzani ni mambo yanayoendelea kukwamisha mchakato wa ujenzi wa haki msingi za binadamu, amani, ukweli na uhuru wa watu kujieleza na kutembea kwa kuzingatia: sheria, kanuni na taratibu.

Askofu mkuu Pierbattista Pizzaballa, Msimamizi wa kitume wa Upatriaki wa Yerusalemu akitafakari kuhusu Noeli, yaani Sherehe ya Kuzaliwa kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa dunia anasema, Fumbo la Umwilisho ni mchakato wa Mwana wa Mungu kuingia katika historia na maisha ya mwanadamu, kwa kumtangazia furaha kuu. Hii ni furaha ya Mwana wa Mungu aliyetwaa mwili na kuzaliwa kwake Bikira Maria, kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu! Wachungaji kondeni walisikia Habari Njema ya Wokovu, wakaondoka kwa haraka kwenda kumwangalia Mtoto Yesu.

Ukombozi ni chachu inayowataka waamini kufanya mageuzi na kuanza upya hija ya maisha yao kwa kuruhusu mwanga wa Kristo kupenya katika maisha; kwa kugeuza mateso na hali ya kukata tamaa katika amani, furaha na utulivu wa ndani; kwa kuacha ubaya na kuanza kutenda mema; kwa kuondokana na ubinafsi ili kutoa nafasi kwa ajili upendo; kwa kuachana na utamaduni wa kifo, ili kukuza na kudumisha Injili ya uhai. Huu ndio wokovu unaoletwa na Mwenyezi Mungu unaowataka waamini kufanya hija kila siku ya maisha yao! Hii ni changamoto endelevu ya kuhakikisha kwamba, watu wote wanashirikiana kwa dhati, ili kuifanya dunia kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi, ili hatimaye, kuzima kiu ya haki; utu na heshima ya binadamu. Kwa kusimama kidete, kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.