2017-12-20 11:30:00

Majadiliano ya kiekumene: Umoja, ushuhuda na huduma makini kwa maskini


Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani imekuwa ni fursa ya kukuza, kuimarisha na kudumisha mchakato wa majadiliano ya kiekuemene miongoni mwa Makanisa mintarafu mwanga na furaha ya Injili inayowawajibisha kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu katika uhalisia wa maisha ya Wakristo. Haya yamo katika Tamko la Makanisa lililotolewa hivi karibuni na Makanisa mbali mbali ya Kikristo kama sehemu muhimu sana ya kuhitimisha maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani, ambayo pia, Kanisa Katoliki limeshiriki kikamilifu kwa uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko ambaye amekazia umuhimu wa kudumisha mchakato wa uekumene wa huduma miongoni mwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii!

Makanisa ya Kikristo yameamua kujikita zaidi katika mchakato wa majadiliano ya kiekumene yanayofumbatwa katika umoja unaoonekana, ushuhuda wenye mvuto na mashiko katika kutangaza Habari Njema ya Wokovu sanjari na kukabiliana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, mambo yanayotikisa utu, heshima, ustawi na maendeleo ya wengi! Makanisa yanatambua dhamana, wito na utume wake katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji inayopaswa kujengwa katika hali ya kuaminiana, kuthaminiana na kushirikiana kwa dhati, ili kudumisha umoja na udugu wa maisha na utume wa Kikristo duniani!

Wakristo wanakumbushwa na Baba Mtakatifu Francisko kwamba, mchakato wa majadiliano ya kiekumene, unafumbatwa katika hija ya pamoja miongoni mwa Wakristo; kwa kutambua kwamba, Wakristo wote wanategemeana na kukamilishana katika maisha na utume wao ulimwenguni! Baraza la Makanisa Ulimwenguni linatambua hatua kubwa ambayo imetekelezwa na Makanisa mbali mbali ya Kikristo katika majadiliano ya kiekumene. Makanisa yameandika kurasa mpya za matumaini kwa Tamko kuhusu Kuhesabiwa Haki; Hati ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu Uekumene “Unitas Redintegratio”, ambayo imekuwa kweli ni msingi wa majadiliano ya kiekumene hatua muhimu katika mchakato wa umoja kamili miongoni mwa Makanisa.

Mkutano kati ya Wakatoliki na Waanglikani uliofanyika kunako mwaka 1931 ulianza kuweka “cheche za msingi wa matumaini” miongoni mwa Wakristo! Baraza la Makanisa Ulimwenguni linakuwakumbusha Wakristo kwamba, wanapaswa kujikita katika uekumene wa huduma, kwa ajili ya kuwasaidia watu wanaoteseka kutokana na sababu mbali mbali duniani, wengi wao wakiwa ni wakimbizi na wahamiaji; wazee, wagonjwa; watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi. Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Baba Mtakatifu Francisko amekazia kwa namna ya pekee kabisa “Matendo ya huruma: kiroho na kimwili” kama yanavyodadavuliwa na Mwinjili Mathayo sura ya 25, changamoto kwa Wakristo kuhakikisha kwamba, wanayamwilisha kama sehemu ya majiundo yao ya awali na endelevu katika maisha ya Kikristo. Yote haya yasaidie kujenga na kudumisha umoja, upendo, mshikamano na udugu miongoni mwa familia ya Mungu inayojitambulisha kwa njia ya huduma makini. 

Katika miaka ya hivi karibuni, Baraza la Makanisa Ulimwenguni linakiri kwamba, Wakristo wa Makanisa mbali mbali wameanza kushirikiana kwa karibu sana, ikilinganishwa na miaka 50 iliyopita. Hii inatokana na ukweli kwamba, Mapokeo, Tamaduni na Tunu msingi za Makanisa haya zimeheshimiwa kama sehemu ya utajiri wa maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo! Hii ndiyo chemchemi ya furaha ya Injili inayopaswa kutangazwa na kushuhudiwa na Wakristo sehemu mbali mbali za dunia sanjari na kukabiliana na changamoto mamboleo, huku wakiwa wameungana kwa pamoja katika huduma kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 500 ya Mageuzi ya Kiluteri Duniani, imekuwa pia ni fursa ya kuangalia kashfa ya utengano miongoni mwa Wakristo kwa jicho kavu pasi na “kupepesa pepesa macho”. Bado kuna haja ya kuendeleza majadiliano ya kiekumene kuhusu utume, kwa kufanya rejea katika amana ya Mapokeo na Maandiko Matakatifu, ili siku moja kadiri ya mapenzi ya Mungu, Wakristo wote wawe chini ya mchungaji mmoja, Kristo Yesu, ili kumtangaza na kumshuhudia kwa ari na nguvu zaidi katika ulimwengu mamboleo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.