2017-12-19 14:24:00

Dhamana na wajibu wa Askofu mkuu Dal Toso: Utume na Sala!


Kardinali Ferdinando Filoni Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, mwishoni mwa Juma, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amemweka wakfu Askofu mkuu Giampietro Dal Toso, aliyeteuliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Katibu Mwambata, Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu na Rais wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa na hivyo, kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Askofu mkuu Protase Rugambwa, aliyeteuliwa hivi karibuni kuwa Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu!

Kardinali Filoni amemtaka Askofu mkuu Dal Toso, kuhakikisha kwamba, anakuwa kweli ni mchungaji makini kwa shughuli za utume wa kimisionari unaotekelezwa na Mama Kanisa kwenye Makanisa mahalia, ili kwamba, Habari Njema ya Wokovu iweze kutangazwa na kuwafikia watu wote mahali walipo! Utume aliokabidhiwa na Mama Kanisa utamwezesha Askofu mkuu Dal Toso kukumbana uso kwa uso na hali halisi ya maisha na utume wa Makanisa mahalia; changamoto, furaha, faraja na mahangaiko ya wakleri katika huduma kwa familia ya Mungu.

Kutokana na changamoto hii, Kardinali Filoni amemtaka Askofu mkuu Dal Toso kuwa ni ndugu ya Maaskofu atakaokutana nao katika maisha na utume wake. Ajitahidi kuhakikisha kwamba, anawasaidia katika utume wao wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu; dhamana wanayoitekeleza katika mazingira, ya umaskini, hali ngumu ya maisha na wakati mwingine, katika hali ya hatari kubwa. Askofu mkuu Dal Toso, anapaswa pia kuwa ni rafiki ya Maaskofu, mintarafu maelekezo yaliyotolewa na Kristo Yesu mwenyewe kwa wafuasi wake; hasa kwa kuonesha huruma, upendo na mshikamano wa dhati, ili kuendelea kutekeleza mchakato wa umisionari.

Askofu anayo dhamana ya kusali kwa ajili ya kuwaombea watu wote, kwa kutambua kwamba, kimsingi yeye ni mtu wa Mungu, aliyeteuliwa kati ya watu kwa ajili ya huduma, ili kuhakikisha kwamba, anakuza na kudumisha Ibada na Uchaji wa Mungu, mambo msingi katika kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Utume huu, umwezeshe kuwa kiongozi mkarimu, akitambua kwamba, Kristo Yesu ndiye anayewaita waja wake na kuwaweka wakfu ili kuendeleza kazi ya ukombozi! Wakleri wanatambua kwamba, wito ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu na wala si kwa ajili ya masitahili yao binafsi, kumbe, wanapaswa kuwa ni watu wa shukrani, tayari kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao, chemchemi ya amana za maisha ya kiroho!

Wito huu anasema Kardinali Filoni ni mwendelezo wa historia ya mapendo ambayo inapata chimbuko lake katika Daraja Takatifu na kwamba, Mama Kanisa anayo dhamana ya kuhakikisha kwamba, analea na kupalilia miito ili iweze kuzaa matunda yanayokusudiwa, yaani toba na wongofu wa ndani, kama sehemu ya mchakato wa utume, umissionari na uinjilishaji. Kristo Yesu ndiye Kuhani mkuu na kwamba, Uaskofu ni utimilifu wa Daraja Takatifu, tayari kujisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.