2017-12-16 09:15:00

Ujumbe wa Papa katika ufunguzi wa Mkutano wa Kiekumene Loppiano


Mazungumzo na urafiki kindugu kati ya wakatoliki na waorthodox ndiyo misingi ya matunda ya mkutano uliofanyika miaka 50 iliyopita kati ya Patriaki wa Kiekumene Athenagoras na Chiara Lubich. Ndiyo maelezo yaliyomo  katika Telegram ya Baba Mtakatifu Francisko aliyotuma katika Taasisi ya Chuo Kikuu cha Sophia cha Wafokolari huko Loppiano Firenze, Italia, kwa Kardinali Giuseppe Bettori, Askofu Mkuu wa Firenze, wakati wa tukio la uzinduzi wa Mkutano wa kimataifa wa Kiekumene  wenye kuwa na nia ya kuwaenzi Patriaki wa Kiorthodox na Mwanzilishi wa Wafokolari. Anawapongeza juu ya kufanya kumbukumbu hiyo ya mkutano na kuwatakia matashi mema  ili  kwamba Chuo Kikuu cha Sophia kwa kufuata karama ya ufunguzi wa Roho, wanaweza kuendelea kuwa sehemu ya makutano na mazungumzo kati ya tamaduni na dini tofauti.

Wazo la mkutano wa Kiekumene   katika Chuo Kikuu  cha Sofia cha Wafokolari lilianzishwa tarehe 26 Oktoba 2015, likiwa ni kwa mara ya kwanza, Chuo hicho kinapokea tuzo ya kwanza ya Shahada kwa ajili ya Utamaduni wa muungano wa Kipatriaki wa kiekuemene wa Costantinople Bartholomew.
Naye Mwenyekiti  wa Wafokolari, Maria Voce, amesema, mpango wa Taaluma hiyo unawakilisha kipindi muhimu cha mahusiano ya kiekumene ambayo yapo kati ya Makanisa dada wa Mashariki na Magharibi na kufungua matarajio ya mshangao katika utafiti unaojikitia kuheshimu mazungumzo, ambayo bado yanahitaji kuwa zawadi ya pamoja katika  ngazi ya tafakari kitaalimungu na muungano wa maandili ya binadamu.

Halikadhalika naye  Patriaki Bartholomew ametuma ujumbe wake  akionesha  furaha yake ya kuanzishwa tukio hilo lenye  mada ya “Patriaki wa Athenagora na Chiara Lubich:viongozi wa umoja”. Anaongeza kusema kuwa ni mkutano wa kinabii kati ya mashujaa wakubwa leo hii katika njia ya kiekumene.Anathibisha pia kwamba, mahusiano ya urafiki na ushirikano na Patriaki wa kiekuemene ulianza Juni 1967 ambapo Chiara alikutana na Athenagoras kwa mara ya kwanza. Wakati wa Mkutano wa kwanza alisema, ni jambo zuri kukutana na kutambuana na kwamba, wameishi  hivi kiupweke bila kuwa ndugu, bila dada kwa miaka mingi na kama yatima. Karne kumi za kwanza za ukristo zimekuwa ni mafundisho ya Kanisa na kwa ajili ya maandalizi ya Kanisa.Na  karne kumi zilizofuta  zikawa za kutengana na mivutano, lakini  karne ya tatu ni ya upendo.

Katika ujumbe pia Patriaki  Bartholomew anasisitiza kuwa, haikuwa tukio la bahati mbaya tendo la Chiara na Athenagora kukutana,bali ilikuwa ni neema ya Mungu ambaye aliweka muhuri kati ya Patriaki wao wa kiekumene na Shirika la Kitume la Wafokolari katika muungano wa upendo kikristo, urafiki wa dhati na mshikamano kindugu ambao unaendelea hadi nyakati hizi na zaidi.

Sr Angela Rwezaula
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican

 








All the contents on this site are copyrighted ©.